Sep 4, 2018

Je, unajua kuwa kila msanii ni wa kipekee?



KAMA wewe ni msanii, iwe wa uimbaji, uigizaji, uchoraji, uchezaji muziki, uchekeshaji, uandishi n.k., amini usiamini hakuna mtu ambaye ana kila kitu ulicho nacho wewe.

Hata kama binadamu ni wawili wawili, basi anaweza akatokea mtu mmoja tu kati ya watu maelfu ndiyo akakufanana kwa vitu vingi: sura, rangi, uzungumzaji, uwezo wa sanaa, mvuto n.k.

Kitu ambacho pengine hukijui ni kwamba mamilioni ya watu duniani wametafuta msanii kama wewe, mwenye sifa kama zako ili wamtumie kwenye matangazo, kwenye video za muziki, kwenye filamu, kwenye mfululizo wa sinema au michezo ya kuigiza maarufu kama series n.k.

Huu ni ulimwengu wa taarifa kuelekea burudani



ULIMWENGU wa sasa unakwenda kwa spidi kubwa sana na magurudumu yake ni teknolojia ya mitandao.

Dunia ya sasa imepita kwenye ulimwengu wa maarifa, sasa ipo kwenye ulimwengu wa taarifa ikikimbia kwa spidi kubwa kwenye ulimwengu wa burudani. Watu hupenda kuburudishwa zaidi ya kuelimika.

Burudani ni muhimu kwa kuwa inawaleta watu pamoja na ni njia nzuri ya familia nzima kujumuika pamoja. Inawatoa watu kutoka kufikiria changamoto za maisha na kuwaburudisha huku ikiwaondolea msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha.

Kwa kawaida, burudani ni kufurahi, kuchangamka na kufurahisha. Burudani inaweza kuwa muziki, matamasha, simulizi, filamu, michezo, ngoma na maonesho ya jadi.

Mwandishi wa Marekani ambaye pia ni mjasiriamali, na mwalimu, Tony Robbins anabainisha kuwa, “Hatupo katika kizazi cha taarifa na maarifa. Tupo katika kizazi cha burudani na starehe.”

Sep 1, 2018

Sanaa hustawisha fikra



SANAA ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji, ina lugha pana ambayo hakuna lugha yoyote nyingine yenye upana kama huo.

Hii si lugha ya sayansi, wala lugha ya kawaida, wala lugha ya mawaidha yenye upana kama wa lugha ya sanaa. Inapaswa ipewe umuhimu na pafanyike juhudi za kuhakikisha muundo wa kujivunia wa sanaa unatumiwa.

Bila ya kuwepo sanaa, matamshi ya kawaida hayawezi kupata nafasi yake katika akili ya mtu yeyote yule. Sanaa ni ala na nyenzo nzuri sana ya kufikisha na kupanua fikra sahihi.

Aug 17, 2018

Tuviendeleze vipaji ili viitangaze nchi kimataifa



KILA mtu aliyezaliwa na mwanamke anacho kitu cha pekee alichojaaliwa kuwa nacho. Kitu hiki si umbile lake, elimu yake, umaarufu wake, usomi wake, cheo chake katika jamii, au utajiri wake wa vitu na fedha; la hasha, bali ni kipaji chake.

Kipaji ni uwezo wa kiasili ulio ndani ya mtu katika maumbile, nafsi na roho yake. Kipaji kinatoka ndani yake. Ni tunu au zawadi toka kwa Mungu ambayo hakuna anayeweza kutunyang’anya au kutuibia mpaka tutakapokufa.

Fedha na magari vyaweza kuibiwa, nyumba inaweza kuanguka, kubomoka, kubomolewa au hata kuungua, lakini vipaji hubakia kuwa nasi daima.

Kipaji ni karama. Ni zawadi anayokirimiwa mtu kutoka kwa Mungu. Kipaji hiki hukua katika ufanisi na matumizi ikiwa kitakuzwa na kuendelezwa na kimenuiwa kutumika kwa niaba ya vingine, si kwa ajili ya ubinafsi bali kwa faida ya wengine na si yake wenyewe.

Tunapomuomboleza King Majuto tusisahau somo alilotuachia

Wachekeshaji mahiri nchini ambao kwa sasa ni marehemu, King Majuto na Sharo Milionea

WIKI iliyopita tasnia ya vichekesho na wapenda burudani tulipata pigo kwa msiba uliogusa na kuwashtua watu wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa sanaa ya vichekesho, kutokana na kifo cha King Majuto.

King Majuto ambaye jina lake halisi aliitwa Amri Athuman alikuwa msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki, na gwiji wa vichekesho ambaye umahiri wake ulikuwa wa aina yake.

Majuto alifariki dunia wakati akipokea matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, majira ya saa 2 usiku wa Jumatano Agosti 8, 2018 akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Baada tu ya kifo chake watu maarufu ndani na nje ya Tanzania walituma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya kijamii, miongoni mwao akiwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Tumeitupa misingi ya michezo kwa binadamu



MICHEZO si tu kwamba ina faida kubwa sana kwa mwanadamu na nchi, pia ni chombo cha kuwasilisha tunu msingi katika kuboresha ubinadamu na katika ujenzi wa jamii ya amani na ya kindugu.

Kwa kauli hiyo yatari tunapata wazo kuu juu ya michezo kwa ujumla ya kwamba michezo imekuwa na lengo kuu msingi tangu zamani za kale la kujenga undugu na amani.

Kama mchezo ni chombo cha kuwasilisha tunu ya binadamu mwenyewe, kujieleza mwenyewe, kukubalika mwenyewe na kujikubali, inamaana kwamba nchi yoyote haiwezi kutambulikana na utaifa wake bila kuwa na utamaduni wao, na mojawapo ya viungo vya utamaduni huo vinavyounganisha katika dunia hii ni michezo.

Aretha Franklin: Malkia wa Soul aliyeishi maisha ya ‘mateso ya kimyakimya’



MUZIKI ni chombo ambacho kimewavutia wanadamu. Katika kutumia nyimbo, waimbaji wameweza kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii zao.

Muziki umekuwa ukitumika kama njia mojawapo ya kujifundisha utamaduni na aghalabu hutumiwa katika kumwelezea mtu, mazingira yake na jinsi anavyoweza kuyatumia na kuyatunza vilivyo.

Kama chombo ambacho hutumiwa kuelezea historia ya jamii, muziki hutumiwa kupasha ujumbe maalumu kwa wanajamii hasa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hutumiwa hasa kuelezea historia, imani, itikadi na kaida zajamii.

Nyimbo kama zao la mazingira ya jamii, zinaweza kufananishwa na mtoto ambaye hufinyangwa na mambo mengi katika historia ya jamii yake.
Hata hivyo, muziki ni zaidi ya taaluma kama zilivyo taaluma zingine za sheria, uhandisi, udaktari, usimamizi wa fedha, biashara na kadhalika. muziki ni kipawa ambacho mtu hutunukiwa na Mungu.

Aug 12, 2018

King Majuto atabaki kuwa nembo ya tasnia ya ucheshi nchini



WASANII wakongwe na mahiri nchini wa sanaa ya maigizo, hususan wa vichekesho wanazidi kupukutika, na kuwaacha wasanii wachanga wakiwa katika mkanganyiko.

Nawakumbuka wasanii ambao walikuwa mahiri sana katika sanaa ya maigizo na vichekesho enzi za uhai wao na sasa hatupo nao ni pamoja na Ibrahim Raha (Mzee Jongo), Fundi Said (Mzee Kipara), Rajab Kibwana Hatia (Mzee Pwagu) na Ali Said Keto (Pwaguzi).

Wengine ni Hamis Tajiri (Janja au Meneja Mikupuo) Tunu Mrisho (Mama Haambiliki), Branco Minyugu, Bartholomew Milulu (Masawe), Said Ngamba (Mzee Small), Said Maulid Banda (Max) na wengine.

Wasanii hawa waliifanya sanaa ya maigizo, hususan ucheshi (comedy) kujizolea umaarufu mkubwa nchini na hivyo kuwafanya vijana wengi nchini kuingia kwenye sanaa ya vichekesho.

Tuitumie fursa ya burudani kukuza uchumi na kuongeza ajira

Diamond Platnumz akitumbuiza


“HATUPO katika kizazi cha taarifa na maarifa. Tupo katika kizazi cha BURUDANI na STAREHE.” Tony Robbins.

Tony Robbins ni mwandishi wa Marekani, mjasiriamali, mwalimu na anajulikana kwa matangazo yake kwenye runinga, semina na vitabu, ikiwa ni pamoja na ‘Unlimited Power’ na ‘Awaken the Giant Within’.

Burudani ni biashara inayokua kwa kasi sana barani Afrika zaidi ya kawaida. Sekta ya burudani imejaa fursa nyingi sana kupita kawaida. Yeyote atakayeamua kuichunguza sekta hii kwa makini atashangaa fursa zilizojaa.

Kila siku mamilioni ya watu duniani wanahangaika kutafuta sehemu za kustarehe, vitu vya kujistarehesha na kujiburudisha, michezo na matamasha ya kufurahisha.

Tujitafakari upya kwenye Bongo Fleva

Wanamuziki Profesa Jay (kushoto) na MwanaFA


MUZIKI kama chombo ambacho hutumiwa kuelezea historia ya jamii, hupasha ujumbe maalumu kwa wanajamii, hasa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hutumiwa kuelezea historia, imani, itikadi na kaida za jamii.

Kwa kawaida nyimbo ni zao la mazingira ya jamii. Zinaweza kufananishwa na mtoto ambaye hufinyangwa na mambo mengi katika historia ya jamii yake.

Hii inamaanisha kwamba muziki hauibuki katika ombwe tupu na hauwezi vilevile kujiundia mazingira yake yenyewe. Mabadiliko na maendeleo ya muziki yamekuwa yakifuatana na historia ya watu wenyewe.

Umuhimu wa muziki unadhihirika katika matumizi ya nyimbo katika wakati maalumu kama njia mojawapo ya kuanzisha mabadiliko katika tabia za jamii au mtu binafsi.

Hatuwezi kuitenganisha sekta ya sanaa na utalii


TANZANIA ni moja ya sehemu bora kabisa duniani ambazo msanii atafurahia kutengeneza filamu yake au kupigia picha za video kwa muziki wake, historia, utamaduni na wanyamapori.

Kuna hali ya hewa nzuri na watu wakarimu ambao wako tayari kumkaribisha mgeni katika mtazamo wa Kitanzania.

Imekuwa inashangaza kuona wasanii wetu wanakwenda kufanya video zao Afrika Kusini na Kenya, wakati Tanzania inashika nafasi ya pili duniani, nyuma ya Brazil, kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku nchi ya Afrika ya Kusini ikishika nafasi ya 14.

Tupaze sauti dunia ijue kuhusu michoro ya Tingatinga


SANAA ya ufundi ambayo inajumuisha uchoraji, upakaji rangi picha, ufinyanzi, uchongaji na utengenezaji wa mapambo mbalimbali ya asili ni utamaduni ambao, kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, ilianza nchini Tanzania.

Sanaa ya uchoraji ilianzia nchini Tanzania takribani miaka 5,000 iliyopita na uthibitisho halisi ni michoro iliyopo katika mapango ya Kondoa Irangi.

Kwa miongo kadhaa, Tanzania imejulikana kwa umahiri wa uchoraji wa picha licha ya kuwa Watanzania wenyewe wametajwa kujiona kuwa siyo walengwa husika wa sanaa hii.
Sanaa ya uchoraji ni lugha ambayo ina ulingo mpana na kila msanii ana lugha yake na wapo wasanii ambao wanafanana katika mfumo wa sanaa wanayofanya na wengine hawafanani kabisa.

Apr 27, 2018

Sanaa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi


Sanaa za Tanzania
KATIKA ulimwengu wa kimaada unaodhibitiwa na fikra za kupenda dunia, thamani za utamaduni (sanaa ikiwemo ndani yake) huwa hazipewi nafasi na siku zote utajiri wote wa sanaa unapimwa kwa fedha.

Suala muhimu katika ulimwengu huo ni fedha, kwa hivyo kila kitu kinapimwa thamani yake kwa kuangalia kitaingiza kiasi gani cha fedha.

Utaona inatazamwa elimu fulani itaingiza fedha kiasi gani, inaangaliwa kazi fulani ina uwezo wa kuingiza kiasi gani cha fedha na vitu kama hivi. Lakini hali haiko hivyo katika upande wa utamaduni.

Hapana, kwani elimu ni njia ya kuwa na maisha bora, na sanaa ni chombo cha kuwa na ustawi katika maisha.

Muungano wetu na utamaduni wetu


JANA Aprili 26, Tanzania iliadhimisha miaka 54 ya Muungano tangu nchi zilizoitwa Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuzaa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania. Nchi hizi mbili yaani Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja) ziliungana Aprili 26, 1964.

Jahazi linalowabeba Watanzania limeweka historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi.

Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Tanzania ni nchi, watu wake mmoja mmoja huitwa Mtanzania na kwa ujumla wao wanaitwa Watanzania, hivyo kuunda taifa la Tanzania.

Apr 25, 2018

Tuzuie teknolojia isikwapue haki za wasanii



Wakati Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) ikizidi kuimarika na kuchukua nafasi ya njia kongwe za mawasiliano, tasnia ya ubunifu nayo inajikuta kwenye changamoto ya kuakisi mabadiliko hayo ya wakati.

Tasnia ya ubunifu (Sanaa) ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji; ambapo wabunifu (wasanii) wanayo dhamana ya kueneza ujumbe na elimu kwa jamii.

Tasnia hii ni mjumuiko wa hakimiliki bunifu ambazo zinapaswa kulindwa ili jamii iendelee kunufaika na kazi hizi za ubunifu, ambazo sasa zimeenea duniani kote.

Apr 18, 2018

Kusambaza video chafu, wasanii wanaelekea kubaya

Wasanii Nandy na Bill Nass katika clip ya video chafu iliyoenea mtandaoni


Hamisa Mobeto
INASHANGAZA sana! Katika kipindi ambacho Sheria za mitandaoni zimetungwa ili kudhibiti matumizi ya mitandao hiyo, ndipo mdudu mbaya sana wa video chafu kaingia katika tasnia nzima ya burudani.

Kabla ya huu mtindo mpya wa video zinazodhalilisha utu tumekuwa tukishuhudia jinsi wasanii wa kike wanavyokuwa nusu watupu kitu kinachosemwa eti ndiyo maendeleo (kupiga hatua), na pengine inabainishwa kuwa hiyo ndiyo dalili ya kuwepo kwa mafanikio katika tasnia hii.

Sakata la Diamond, Nandy:Tusipojipanga dunia itatupanga

Wanamuziki Nandy na Bill Nass katika pozi
Diamond Platnumz
KAMA mtafiti, mchambuzi, mdau wa sanaa na mwananchi wa nchi hii nimekuwa nikiitahadharisha jamii yangu kuhusu vita vinavyoendelea duniani kati ya mataifa makubwa na mataifa machanga.

Lakini hivi si vita kama vile vinavyoendelea huko Syria, wala si vita vya kupinga ugaidi n.k. la hasha! Bali ni vita vya kiutamaduni, vya kutawalana kiakili.

Vita vya utamaduni huenezwa kupitia vyombo vya habari ikiwemo mitandao, televisheni, redio, magazeti, sinema, muziki n.k. ambavyo ni jukwaa muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika.

Apr 13, 2018

Tuwafundishe watoto umuhimu wa michezo ya pamoja



MICHEZO ni chombo cha kuwasilisha tunu msingi katika kuboresha ubinadamu na katika ujenzi wa jamii ya amani na ya kindugu.

Michezo ina faida kubwa sana kwa mwanadamu, siyo kwa wachezaji tu bali hata kwa wanaoshabikia ambao kufurahi kwao huwa ni kinga dhidi ya maradhi, hasa inapokuwa michezo ya ushindani.

Ni wazi kuwa matatizo mengi ya kiafya kwa wanadamu yanaongezeka siku hizi kutoka na mfumo mpya wa maisha tunayoishi ukilinganisha na miaka ya nyuma. Ingawa kwa wale wanaoshiriki michezo mbalimbali mara nyingi imewasaidia kuepuka matatizo hayo.

Apr 12, 2018

Sanaa ina nafasi kubwa katika jamii

Wasanii wa kizazi kipya wanaounda kundi la Tanzania All Stars wakiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara

UHAKIKA wa sanaa – iwe sanaa yoyote ile – ni kipaji kutoka kwa Mungu, ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji.

Ijapokuwa kudhihiri kwa sanaa kunatokana na jinsi sanaa yenyewe itakavyobainishwa, lakini huo si uhakika wote wa sanaa. Kabla ya kubainishwa, kuna hisia na utambuzi na udiriki wa sanaa yenyewe na kwamba mambo yote yanachimbukia hapo.

Baada ya kuonekana, kutambuliwa na kubainishwa uzuri, unyofu na uhakika wa sanaa, hapo ndipo zinapoweza kuzuka maelfu na nukta ndogondogo na nyembamba sana ambazo baadhi ya wakati hawawezi kuziona nukta hizo isipokuwa wasanii wenyewe.

Mar 29, 2018

Nchi za SADC na mkakati wa sanaa kwa maendeleo

Ramani inayoonesha nchi za SADC



MAPEMA Machi mwaka huu kuliandaliwa Tamasha la Kusherehekea Wanawake wa SADC Katika Sanaa ya Maigizo na Dansi lililofanyika mjini Johannesburg.

Wanawake wa Zambia katika kikundi cha dansi walitumia michezo ya maigizo kwa ajili ya maendeleo kwa kuhamasisha wanakijiji kupanda zaidi ya miti 5,000 na kujenga majengo matatu ya madarasa kwa kipindi cha miaka mitatu katika Jimbo la Kusini mwa Zambia.

Tamasha hilo liliandaliwa na "Southern Africa Theatre Initiatives (SATI)" na lilikuwa na lengo la kuonesha jukumu la wanasanaa wanawake wa nchi za SADC kuungana na kuleta mabadiliko katika kanda.

“Wanasanaa wanawake wanapuuzwa pamoja na kazi kubwa wanayofanya kuunganisha na kuendeleza jumuiya. Wanachohitaji ni kutambua na kupatiwa msaada tu,” alisema Mpo Molepo, katibu wa SATI.

Filamu ya Gifted Hands: Inaonesha jinsi maisha yako yanavyoweza kuwa somo kwa wengine

Filamu ya Gifted Hands
KILA mmoja ana ndoto zake katika maisha yake. Wengine wana ndoto kubwa za kubadilisha ulimwengu huu, huku wengine wakiwa na ndoto za kuishi maisha ya kupata mahitaji yao ya msingi tu.

Lakini wote hawa wanahitaji kuzitimiza ndoto zao; ila katika safari ya kutimiza ndoto hizi kuna vikwazo na mambo mbalimbali ambayo huwazuia watu wasiziishi ndoto zao na kuishia kulaumu na kulalamika, hasa uzeeni.

Wewe je, una ndoto? Je, ndoto yako ni ya namna gani? Je, umewahi kujiuliza kwamba ufanye nini uweze kuitimiza ndoto yako?

Mar 24, 2018

Tuwe macho, hii ni vita ya utamaduni



MIAKA kadhaa iliyopita niliwasiliana na kampuni ya Sony Pictures yenye makao yake Los Angeles (Culver City) nchini Marekani. Hii ni kampuni kubwa Hollywood ya burudani iliyoanzishwa Agosti 7, 1991 baada ya kujitenga kutoka kampuni ya Columbia Pictures Entertainment.

Kampuni hii inafahamika kwa filamu za The Karate Kid, Ghostbusters, Spider-Man, Men in Black, Underworld, Robert Langdon, The Smurfs, Sniper na nyingine nyingi. Niliwasiliana na Sony Pictures nikiwaomba watafute njia ya kudhibiti filamu za Hollywood zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika Mashariki.

Mar 16, 2018

Zi wapi zama za vikundi vya sanaa?

Kikundi cha Sanaa cha TaSUBa wakifanya vitu jukwaani


DAH! Ama kweli siku hazigandi na maisha hayarudi nyuma! Maisha yakipita yamepita, japo historia ndiyo inayoweza kuturudisha nyuma tupendavyo. Enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadaye Ali Hassan Mwinyi kulikuwa na vikundi vingi vya sanaa, hasa vya sarakasi, maigizo, ngoma, mazingaombwe na kadhalika.

Vikundi hivi vilitoa burudani ya aina yake katika jamii husika, na watu walikuwa wakienda kwenye kumbi mbalimbali, hasa jijini Dar es Salaam na miji mikubwa mwisho wa wiki kupata burudani ya aina yake.

Nakumbuka kulikuwa na vikundi vya sanaa vya DDC Kibisa, Muungano Culture Troup, Makutano Dancing Troup, Ujamaa Ngoma Troup, Mandela Theatre, Bima Modern Taarab, Super Fanaka, Reli Kiboko Yao, JWTZ, Tancut Almasi, UDA, Urafiki n.k.

Mar 15, 2018

The Theory of Everything na maisha ya Prof Hawking

Prof Stephen Hawking enzi za uhai wake

Filamu ya The Theory of Everything
NILIWAHI kusoma riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo iliyoandikwa na Profesa Euphrase Kezilahabi, inayoonesha maisha yaliyopo duniani ni sawasawa na fujo, kwani kila mtu anayekuja duniani huleta fujo zake na baadaye kutoweka.

Fujo hizo zimekuwa zikitofautiana, wapo waliofanya fujo kwa jina la amani, waliofanya fujo kwa kutumia nguvu na wengine wamefanya fujo za kimaandishi, fujo ambazo hazitafutika hadi dunia inafutika…

Nimejikuta nikiikumbuka riwaya hii baada kutafakari kuhusu maisha ya Prof Stephen Hawking, mwanafizikia maarufu duniani aliyefariki dunia jana Jumatano Machi 14, 2018 akiwa na miaka 76.

Mar 12, 2018

Mapokeo ya kazi za sanaa yanavyotuathiri



INGAWA Tanzania kuna zaidi ya makabila 120 na lugha 128 zinazotumika, Watanzania tumeweza kubaki kama tulivyo, Watanzania. Popote pale Mtanzania atakapokwenda atajiita  Mtanzania, akiulizwa zaidi ya hapo, anaweza akataja kabila yake. Ila, Watanzania hupenda zaidi kuwa Watanzania. Ndiyo utamaduni wetu.

Kinachoonekana sasa ni Watanzania kutaka kugawanyika kwa misingi ya kidini, hasa kati ya Wakristo na Waislamu, japo wameishi pamoja vizuri tangu uhuru.

Pamoja na hayo, Sera ya Ujamaa na lugha ya Kiswahili zimechangia sana kutufanya kuwa wamoja. Rangi, ladha, urafiki na uchangamfu ndiyo viungo muhimu vya utamaduni wa Tanzania.

Mar 7, 2018

Filamu ya The Silent Child: Somo kubwa kwa tunaodhani ‘hawawezi’




MARA nyingi nimewashauri wasanii wa Tanzania kutengeneza filamu fupi, kwani soko lake limejengwa katika misingi imara, haliangalii majina ya watu bali misingi na weledi.

Soko kubwa la filamu hizi lipo kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa, kwani matamasha ya filamu ni sehemu nzuri zaidi ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa.

Naam… sanaa ya filamu ni kitu cha ajabu sana. Si kila mtu anaweza kuipenda kazi yako. Ila unachotakiwa ni kusimamia ndoto yako pasipo kukata tamaa. Hasa ukiwa na script nzuri na mipango sahihi.

Mar 3, 2018

Black Panther inapowasuta wazungu kuhusu Afrika



TANGU filamu ya Black Panther itoke, kwa kweli imenifikirisha sana kwa jinsi ilivyojaribu kuiweka Afrika katika nafasi chanya, ikiionesha Wakanda (Afrika) kuwa nchi bora sana.
Kwa jinsi Wakanda ilivyoonekana, maana yake ni kuwa kama Afrika isingetawaliwa na wakoloni na kuachwa kukua yenyewe, ingekuwa mbali sana.

Ukiangalia filamu nyingi za watu weusi, mazingira ya Afrika yanaonekana kuwa ni mabaya sana na machafu, lakini tofauti katika filamu hii, nchi ya kufikirika ya Wakanda ina teknolojia za hali ya juu kuliko hata nchi kubwa za ulaya na Marekani.

Filamu ya Watu Wote ni somo kwa Bongo Movies


JUZI nilipata nafasi ya kujadili jambo na Mpigapicha mkuu wa gazeti la HabariLeo, Fadhili Akida, ambaye alionesha nia ya kutaka kutengeneza filamu fupi, ingawa hakujua soko lake likoje.

Tulijikuta tukiwa katika mazungumzo hayo baada ya mchambuzi maarufu wa filamu nchini, ambaye pia ni mhariri wa uzalishaji wa gazeti la HabariLeo, Beda Msimbe, kuibua hoja kuhusu filamu fupi.

Wakati nikiongea na Fadhili, nilijaribu kumweleza uzoefu wangu kuhusu tasnia ya filamu na kile ninachojua kuhusu sekta hii na soko la filamu fupi. Ni mara nyingi nimekuwa nikiwashauri wasanii wetu kuligeukia soko la filamu fupi, kwani soko hili limejengwa katika misingi imara, kwani haliangalii majina ya watu bali misingi na weledi.

Feb 23, 2018

Tutumie filamu na muziki kutangaza utalii

Mlima Kilimanjaro

KATIKA nchi hii kuna maeneo bora ya upigaji picha, kuanzia Tanzania Bara hadi Zanzibar, kuanzia kwenye mlima mrefu hadi kwenye maziwa yenye kina kirefu kabisa katika Bara la Afrika.Tanzania ni nchi ya maajabu na vivutio: mlima mrefu Afrika (Mlima Kilimanjaro), mbuga bora yenye wanyama wa kuvutia duniani ya Serengeti, yenye stori ya wanyama wanaohama kila mwaka na kurejea.

Bila kuzunguka, hebu tutafakari ni kwa namna gani filamu na muziki vimeweza kuitangaza Nigeria? Tuanzie filamu, tasnia yao ya filamu (Nollywood) imeweza kuwatangaza kwa kiasi gani? Tutapata jibu la haraka kwamba taifa hilo limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala cha chini.