ULIMWENGU wa sasa unakwenda kwa spidi kubwa sana na magurudumu
yake ni teknolojia ya mitandao.
Dunia ya sasa imepita kwenye ulimwengu wa maarifa, sasa ipo
kwenye ulimwengu wa taarifa ikikimbia kwa spidi kubwa kwenye ulimwengu wa
burudani. Watu hupenda kuburudishwa zaidi ya kuelimika.
Burudani ni muhimu kwa kuwa inawaleta watu pamoja na ni njia
nzuri ya familia nzima kujumuika pamoja. Inawatoa watu kutoka kufikiria
changamoto za maisha na kuwaburudisha huku ikiwaondolea msongo wa mawazo
unaotokana na ugumu wa maisha.
Kwa kawaida, burudani ni kufurahi, kuchangamka na kufurahisha.
Burudani inaweza kuwa muziki, matamasha, simulizi, filamu, michezo, ngoma na
maonesho ya jadi.
Mwandishi wa Marekani ambaye pia
ni mjasiriamali, na mwalimu, Tony Robbins anabainisha kuwa, “Hatupo katika kizazi cha taarifa na maarifa. Tupo katika
kizazi cha burudani na starehe.”
Tony Robbins anajulikana kwa matangazo yake kwenye runinga, semina na
vitabu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ‘Unlimited Power’ na ‘Awaken the Giant
Within’.
Burudani ni biashara inayokua kwa
kasi sana duniani zaidi ya kawaida. Sekta ya burudani imejaa fursa nyingi sana
kupita kawaida. Yeyote atakayeamua kuichunguza sekta hii kwa makini atashangaa
fursa zilizojaa.
Kila siku mamilioni ya watu
duniani wanahangaika kutafuta sehemu za kustarehe, vitu vya kujistarehesha na
kujiburudisha, michezo na matamasha ya kufurahisha.
Sekta ya burudani inatengeneza
zaidi ya dola billioni 50 za Marekani kila mwaka. Sekta hii inaongoza katika
kutengeneza ajira kuliko sekta zote barani Afrika.
Kwa maana hii, wasanii na wabunifu wanapaswa kufahamu kuwa
kiini cha mafanikio ya biashara ya burudani au biashara nyingine yoyote duniani
baada ya kuanza kushamiri ni ’connection’.
Wanatakiwa kutafuta connection, hii tabia ya kuendelea kufanya
biashara ya umimi na kujifungia ndani ya boksi kimewafanya wabaki na wateja
walewale na mwisho biashara imedumaa huku wakiamini inakua kwa sababu macho yao
yameishia walipo.
Mawasiliano yana mchango mkubwa sana katika ukuaji na uendelezaji
wa biashara ya burudani, iwe ya filamu, muziki au sanaa nyingine yoyote. Hii
inatokana na kwamba mawasiliano hutumika katika maeneo mengi hususani kwenye
shughuli za kibiashara za kila siku.
Katika kutafuta mawasiliano, taarifa za masoko ni muhimu kwani huu
ndiyo moyo wa biashara yoyote kwa sababu ukuaji wa biashara unategemea soko kwa
kiasi kikubwa.
Kutokana na ukuaji wa teknolojia matumizi ya simu za mkononi na
mtandao wa intaneti vimekuwa ni msaada mkubwa katika kuwafikia wateja wengi na
wadau mbalimbali wa biashara kwa muda mfupi, hivyo matumizi sahihi ya
teknolojia ya mawasiliano yanasaidia ufanisi wa biashara.
Kutokana na ukuaji wa teknolojia wafanyabiashara wengi wanatafuta
masoko kupitia teknolojia ya mawasiliano ambapo kufanya matangazo ya bishara ni
bure au ni kwa bei nafuu.
Hata hivyo, lipo kosa moja ambalo wasanii na hata watu wengine
wamekuwa wanafanya kwenye kazi zao. Wanategemea baraka za watu wengine ili
maisha yao yaende.
Mfano mwanamuziki anapokuwa anategemea vyombo vya habari
kupiga nyimbo zake ndiyo awafikie watu. Inapotokea vyombo hivyo vinakataa
kupiga nyimbo zake, anakuwa ameondolewa kabisa kwenye sanaa.
Siku za hivi karibuni pia wafanyabiashara wamekuwa wanafanya
kosa kubwa sana. Wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kama majukwaa yao,
ambayo wanayatumia kuwafikia wateja wao.
Kiasi kwamba kama mitandao ya kijamii inafungwa yote leo,
wafanyabiashara wengi wataondoka kwenye biashara kabisa, kwa sababu hawana njia
nyingine ya kuwafikia wateja wao.
Wasanii wanapaswa kutofanya kosa hili kwenye kazi zao, wanahitaji
kuwa na jukwaa wanalomiliki wenyewe. Wanahitaji kuwajua mashabiki wa kweli wa
kazi zao, ambao wanaweza kuwafikia hata kama dunia nzima itakuwa imewasusia na
kila wanayemtegemea amewatenga.
Wanahitaji kuwa na connection na mashabiki wa kweli 1,000 ili
kuendesha maisha yao.
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, unahitaji kuwa na
mashabiki wa kweli elfu moja ili kuweza kuendesha maisha yako. Tunaposema
mashabiki wa kweli, ni wale ambao wanakuamini kweli, wale ambao wapo tayari
kufanya chochote kupata kazi zako. Wale ambao wapo tayari kuwaambia wengine
kuhusu wewe, wapo tayari kulipa gharama yoyote kupata kazi zako.
Unahitaji mashabiki hao elfu moja ili uweze kuendesha maisha
yako kwa upande wa kipato. Kwa mfano kama una mashabiki hao elfu moja, na kila
mmoja anakuingizia faida ya elfu moja kwa mwezi, una zaidi ya milioni moja kwa
mwezi, kitu ambacho kitayawezesha maisha yako kwenda.
Lakini pia mashabiki hao elfu moja ndiyo wataitangaza kazi
yako kwa wengine. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi tunazoweza kuweka, kuna
kitu kimoja ambacho hatuwezi kukiathiri, kitu hicho ni ‘bahati’.
Wakati mwingine kuna vitu vinatokea, ambavyo vinakusaidia
kusonga mbele zaidi, ambavyo hukuvifanya wewe vitokee. Kwa mfano mtu mwenye
ushawishi mkubwa anakutana na kazi yako, na kuipenda kisha kuwaambia wale ambao
ana ushawishi kwao na ghafla unakuwa mtu maarufu.
Lakini tunapaswa kugundua jambo moja muhimu kuhusu bahati,
hutapata bahati kwa kuomba ukutane na bahati, badala yake unahitaji kuwa na
maandalizi ya kutosha, ili nafasi inapotokea basi uwe kwenye eneo sahihi.
Huwezi kulazimisha bahati, kadiri unavyokuwa umefanya kazi
bora, na kuitangaza vizuri kwa wale wanaohusika, kisha ukawa na jukwaa la
mashabiki wa kweli, unaongeza nafasi za wewe kukutana na fursa ambayo utaweza
kuitumia na wengine wataona ni bahati.
Njia hii inasaidia kupata wateja wengi hivyo kuongeza mauzo na
hatimaye kukuza biashara yako, hasa katika ulimwengu huu wa sasa wa uchumi
tegemezi.
Vijana wengi wamekuwa wakijikita kwenye kutafuta uhisani au
utegemezi na kujikuta wakiingia katika uovu wa kimaadili na hata kutambulisha
aina mpya ya maadili potofu.
Uchumi tegemezi umewaumiza vijana wengi, hasa wale wa kutafuta
udhamini na uhisani na mwishowe wamejikuta wakiingizwa katika biashara za dawa za
kulevya bila kujitambua na kuishia kwenye mikono ya dola.
Hata hivyo, uchumi tegemezi ni mzuri kwa makundi ya kisanaa
lakini ni vyema kutafuta taarifa sahihi na wala siyo kutafuta uhisani na
udhamini unaotutia matatizoni.
No comments:
Post a Comment