Sep 14, 2011

Kanisa laipotezea ndoa ya Joyce Kiria



 Ndoa ya kwanza ya Joyce kiria na DJ Nelly


Ndoa ya sasa na Henry Kilewo

Mbunge wa Ubungo John Mnyika pia alikuwepo

Zikiwa zimekatika siku kadhaa toka kufungwa kwa ndoa kati ya presenter wa Kipindi cha Bongo Movies kupitia runinga ya EATV, Joyce Kiria na Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Henry John Kilewo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia mchungaji wake mmoja (jina limehifadhiwa), limesema ndoa hiyo haitambuliki.

Akizungumza na gazeti moja Jumatano iliyopita jijini Dar, mchungaji huyo alisema kuwa, ndoa ya Joyce inayotambulika ni ile iliyofungwa Desemba 16, 2008 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambako nakala ya cheti  cha ndoa yake imehifadhiwa.



Mchungaji huyo alisema kufungwa kwa ndoa mpya kwa sababu mahakama ilitoa hati ya talaka ya ndoa ya kwanza baada ya wanandoa kutofautiana, si kigezo cha kuifanya KKKT kuitambua ndoa hiyo.

“Unajua tatizo liko wapi mwandishi? Wengi wanaamini mahakama ikitengua ndoa, basi mpya itakayofungwa ni halali. Ndoa inafungwa kwa ushahidi wa Mungu na si wa mahakama.
“Na wanandoa wakumbuke kuwa, siku ya ndoa huwa wanatakiwa kuapa kama wapo tayari kuishi katika tabu na raha, sasa utakuta mmoja akipata matatizo anadai talaka, wanadhani ni tabu gani inayopita ile ya siku ya kiapo?” alihoji mchungaji huyo wa kanisa moja la Ubungo, Dar.

Joyce alifunga ndoa ya kwanza mwaka 2008 na mchezesha muziki wa radio, Nelson Nkongo ‘Dj Nelly’ lakini mwaka 2010 walitengana kwa kisa ambacho mpaka sasa hakuna kati yao aliyekuwa  tayari kukiweka wazi.

Baada ya hapo, mtangazaji huyo alitinga Mahakama ya Mwanzo Sinza, jijini Dar es Salaam kudai talaka yake ambayo aliipata.

Septemba 4, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, kupitia kwa mkuu wa wilaya ‘Bomani’, Joyce alifunga ndoa nyingine iliyofana vilivyo na kuhudhuriwa na watu kibao, kati yao walikuwemo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye alikuwa mpambe wa bwana harusi.

Source: wahapahapa


No comments: