Jan 16, 2014

Waziri ateua Bodi mpya ya Filamu na Michezo ya Kuigiza



Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amemteua Mheshimiwa Pindi Chana kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Uteuzi huu unatokana na Mamlaka aliyopewa Waziri huyo chini ya kifungu cha 13(i) cha Sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza Na.4. ya mwaka 1976.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo kwa Vyombo vya habari uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wengine wa Bodi umeanza tarehe 3 Desemba 2013.

Jan 8, 2014

Sawa tunaibiwa, je tunaibiwaje?

* Hivi tunamjua mwizi wetu?


Wasanii wa filamu wakionesha kazi bandia za filamu zinazouzwa mtaani


MWAKA uliopita 2013 kwa tasnia ya filamu nchini tuliuaga kwa pilikapilika mbalimbali, mojawapo ikiwa ni mkutano mkubwa wa wadau wa filamu na muziki uliofanyika 30 Disemba 2013 kwa kuandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Cosota, Bodi ya Filamu, Basata, Shirikisho la Filamu (TAFF) na Shirikisho la Muziki (TMF). Pia kulikuwepo maandalizi ya chinichini ya wasanii/watayarishaji kuandaa maandamano makubwa ya kuishinikiza Serikali ichukuwe hatua dhidi ya maharamia wa kazi za sanaa.

Isingekuwa busara za uongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania inawezekana hivi sasa kungekuwa na tafrani, kwani wasanii/watayarishaji hawa walikuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa msambazaji wa filamu kuwa endapo hawatafanya hivyo, yeye atajitoa kusambaza filamu, jambo lililowatia hofu wasanii hawa na aliwapa masharti kuwa ili aendelee kusambaza kazi zao ni lazima wafanye maandamano yenye kulaani na kuishinikiza serikali kabla ya tarehe 1 Januari 2014.

Jan 1, 2014

Tutafute fursa za masoko ya filamu zetu nje ya nchi


Wasanii wakifuatilia jambo kwenye moja ya vikao


MAJUZI nilijikuta nipo kwenye kikao kimoja cha wadau waliojiita wenye uchungu na tasnia ya filamu nchini, nilikuwepo hapo si kama mchangiaji bali kama msikilizaji wakati baadhi ya wadau hao walipokuwa wakijadili kuhusu mfumo unaofaa kwa ajili ya kusambaza na kuuza filamu zetu. Katika kikao hicho ambacho naamini hakikuwa rasmi bali kilichokuja baada ya mjadala mrefu ulioibuliwa kuhusu makato ya kodi ya asilimia tano wanayodai kukatwa na msambazaji wa filamu kwa kisingizio kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagiza kukwatwa kwa kodi hiyo.