Nov 11, 2013

KWA KUANDAA MAFUNZO: Wasanii mkoani Iringa wanapaswa kuigwa


Mmoja wa wasanii mjini Iringa akikabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo na Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba

ILIONEKANA kama masikhara, wengi waliwabeza, hata rafiki zao waliona kuwa walichokuwa wakikifanya ulikuwa ni upuuzi mtupu. Hatimaye siku zikaanza kujongea taratibu, mara wiki, mbili, hadi ukatimia mwezi tangu waanze kuchukua mafunzo yaliyobeba dhana nzima ya kujitambua, kujifunza misingi ya uigizaji, uandishi, uongozaji na utayarishaji wa filamu.

Mafunzo haya ya mwezi mmoja yaliandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Tanganyika Center for Development and Advocacy (TCDA) ya mjini Iringa na kufadhiliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Fredrick Mwakalebela. Taasisi hii ni matokeo ya vijana wawili waliomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani tofauti na kukumbana na changamoto za ajira baada ya kurudi mtaani. Moja ya malengo ya Taasisi hii ni kuwaelimisha vijana umuhimu wa kujiajiri kwa kutumia fursa zilizopo.

Oct 30, 2013

Wasomi wetu na kisa cha ‘Heri mimi sijasema’!


Wasomi kama hawa ni tegemeo katika jamii yetu, wanapokwepa majukumu yao kama wasomi ni hasara kwa taifa

NILIPOKUWA mdogo, moja ya sababu kubwa iliyonifanya nipende sana kwenda shule ni kusoma na kusikia hadithi na visa mbalimbali, ama kwa kuvisoma kwenye vitabu (wakati huo kila shule ilikuwa na maktaba yenye vitabu vya kutosha), au masimulizi kutoka kwa walimu wenye kupenda kufundisha kwa mifano. Hadithi nilizozisikia na kuzisoma zilijaa mafunzo ya kila aina, hadithi kama zile za kina Juma na Roza, Bulicheka na mke wake Elizabeth na Wagagagigikoko, au ile hadithi maaruf ya ‘Heri mimi sijasema’.

Hii ni hadithi iliyohusu vita katika ufalme fulani, ambapo wapiganaji watatu wakiwa vitani waliamua kujificha kwa kujifunika na nyasi, bahati mbaya adui akawa anapita eneo lile na kuwakanyaga bila kujua. Mmoja wa wapiganaji hao akalalamika; “kwanini unawakanyaga wenzio kama nyasi?” Yule adui akashtuka kuwa pale kuna mtu kajificha akamchoma mkuki na kumuua.

Oct 17, 2013

MMOMONYOKO WA MAADILI: Tutumie filamu, nyimbo zetu kuhamasisha uzalendo


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, 
Dk. Fenella Mukangara

Niliwahi kuandika makala hii kuhusu kutumia filamu kuhamasisha uzalendo, nalazimika kuirudia kutokana na sababu fulanifulani ingawa ikiwa imeboreshwa zaidi.

Mwaka huu tarehe 9 mwezi Disemba tunatimiza miaka 52 tangu tuwe huru, huku tukishuhudia jamii ya Kitanzania ikizidi kupoteza maadili, mila na tamaduni zake kila kukicha. Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliundwa mwaka 1962, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alitamka wazi kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa, na nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Oct 10, 2013

UTEKETEZAJI WA KAZI FEKI ZA SANAA: Ni kweli tunasaidia kumpoza msanii aliyeibiwa?



·        Tuzipitie upya sheria zetu za Hakimiliki

Maofisa wa Cosoza wakiteketeza CD na Mikanda ya wizi katika uwanda wa Kikungwi, Wilaya ya Kusini Unguja

“MWANAHARAKATI, kwanza kabisa nakushukuru sana kwa makala yako wiki hii, pili nakubaliana kabisa na wewe kuhusu ulichoandika kuhusu ‘matumizi ya muziki ni muhimu sana kwenye filamu zetu’. Ukweli ni kwamba suala la wasanii wetu kupenda kutumia nyimbo ambazo wala hawajaomba ruhusa kuzitumia ni jambo baya sana. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za Hakimiliki, haina tofauti na ambavyo wao wamekuwa wakilalamika kuibiwa kazi zao, kwani hata wao ni wezi wa kazi za wengine.

Oct 3, 2013

Muziki ni muhimu sana kwenye filamu zetu

  • Watayarishaji wa filamu nchini hawana bajeti ya muziki
  • Wengi huokoteza miziki isiyoendana na maudhui

Kwenye nchi zingine wanamuziki kama hawa (John Kitime), wenye ubunifu huwa wanatumika kunogesha filamu kutokana na midundo ya muziki

WIKI hii nilitembelea ofisi ya watayarishaji wa filamu nchini, John Lister na Paul Mtendah, kwa lengo la kuwajulia hali, niliwakuta wakikamilisha uhariri wa sinema inayotazamiwa kutoka hivi karibuni ya ‘Mke Mchafu’, iliyotokana na mwongozo (script) niliouandika. Nikiri tu kuwa pamoja na kuandika script hiyo, lakini nilijikuta nikiangalia sinema ambayo ni kama vile sikuwahi kuiona hadithi yake kutokana na jinsi sauti na miziki iliyotumika kwenye filamu hiyo jinsi ilivyoleta radha tofauti.

Ingawa nilikuwa na haraka, nilijikuta navutiwa sana kuiangalia sinema kutokana na miziki iliyotumika kwenye sinema hiyo kuendana sana na matukio ya sinema na kukoleza mshawasha wangu wa kutaka kuiangalia hadi mwisho. Niliwadadisi watayarishaji hao kama miziki hiyo ilikuwa imetungwa maalum kwa ajili ya filamu hiyo au imetokea kama ajali (accidentally) tu.

Sep 25, 2013

Fursa muhimu kwa wasanii na wadau wa filamu



Jengo la Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM, kimeandaa kozi ya uandishi wa filamu. Ni kozi ya siku kumi itakayoanza tarehe 1 mpaka 11 Oktoba. Kozi hii imetangazwa magazetini wiki iliyopita. Huu ni ujumbe utakaosaidia kufikisha ujumbe kuhusu fursa hii kwa wadau mbalimbali. Kozi hii itafanyika kwenye jengo la Shule Kuu ya Biashara (UDBS) ikilenga kuwezesha uandishi wa miswada ya filamu kwa kupitia ngazi zote kama vile sanaa ya uandishi wa miswada ya filamu, maandalizi kabla ya kuandika, kanuni za uandishi na usanifu wa mswada wa filamu, na muundo wa andiko la filamu.

Gharama za kozi hii ni Tsh. 300,000 (laki tatu). Gharama hizo ni kwa mafunzo, vifaa, chakula na Certificate ya UDSM.

Bodi ya Filamu: Hatuhitaji kudhibitiwa bali kupimwa

Inye, moja ya sinema zilizoonja makali ya kudhibitiwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini


MAKALA ya wiki iliyopita iliyoonesha kupinga waziwazi uwepo wa Bodi ya sasa ya Ukaguzi wa Filamu kwa kuwa imerithi sheria za kibaguzi za mkoloni (censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika, imepokelewa kwa mitazamo tofauti sana na wasomaji wangu wengi. Wapo ambao walibainisha kuwa hawajaelewa namaanisha nini hasa na wengine wameonesha kutofautiana nami kabisa katika jambo hili.

Kauli ya: “…Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?” imeonekana kutumiwa na wasomaji wangu kama reference ya kupinga vikali kuwa nataka wasanii waachiwe kufanya watakavyo bila kudhibitiwa jambo linaloweza kuzidisha mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.

Sep 18, 2013

Ili kuongeza ufanisi: tupiganie Bodi Huru ya Filamu

 Kama wadau wa filamu tufikirie kutumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kama haya ya Dar es Salaam ambayo ni njia nzuri sana katika kujitangaza kitaifa na kimataifa


INASEMWA kuwa sekta ya filamu nchini kwa sasa imerasimishwa, jambo ambalo limekuwa haliniingii akilini kwa kuwa sijaona mfumo wowote unaotuashiria kwamba sasa tuko rasmi zaidi ya huu wa kulipa kodi kupitia stika za TRA. Hivi tumerasimishwa kwa Sera ipi hasa?

Sera ni hati muhimu inayoelezea thamani na kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni. Nimewahi kuandika kabla kuwa bila sera madhubuti ya filamu maendeleo katika sekta hii yatabaki kuwa ndoto hata kama viongozi wa serikali watatuahidi mambo makubwa kiasi gani. Lakini kwanini tuendelee kuongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya kupigania uwepo wa sheria?

Sep 5, 2013

Maadili na uandaaji wa filamu katika nchi zinazoendelea



Elizabeth Michael maaruf kwa jina la Lulu katika pozi

IJUMAA ya wiki iliyopita nilialikwa kwenye ofisi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya mazungumzo ya kiofisi, kuhusu mustakabali wa sekta ya filamu nchini, hasa ikizingatiwa kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, chombo cha juu cha wadau wa filamu nchini, kinachopaswa kufanya kazi kwa ukaribu na Bodi ya filamu.

Hapo kwenye ofisi za Bodi, niliongea mengi na watendaji wakuu wa ofisi hiyo, chini ya uenyekiti wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, yaliyotufikisha katika suala la maadili katika filamu zetu ambapo aliwataja baadhi ya wasanii wanaokiuka maadili na hawako tayari kujikosoa hata pale wanapoelekezwa njia sahihi.

Aug 7, 2013

Uongozaji huu wa filamu utaleta maafa makubwa


 Muigizaji wa filamu Tanzania, Maulid Mfaume, aliyevunjika miguu yote kwa kujirusha toka ghorofa ya nne wakati wa upigaji picha

UONGOZAJI wa filamu ni zaidi ya kujua “standby... action... cut!” Uongozaji wa filamu ni tatizo kubwa mno kwenye tasnia ya filamu nchini, ni tatizo kwa kuwa waongozaji wetu wa filamu hudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua “standby... action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji.

Muongozaji wa filamu anawajibika kuutafsiri muongozo wa filamu ulioandikwa kwenye karatasi na kuuhamishia katika picha halisi na sauti kwenye skrini – na anapaswa kuiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa filamu hiyo, na hivyo kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi. Pia anapaswa kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji ni pamoja na kufanya usaili (casting).

Aug 1, 2013

Utamaduni wa Mtanzania: Ni nani wenye dhamana ya kutoa tafsiri sahihi?


  • Walioaminiwa wanatupoteza, sasa hatuna mwelekeo

Huu ndiyo utamaduni wa Kiafrika unaopingana na tafsiri ya wakubwa


“UTAMADUNI wa Mtanzania, are we sure?” nilijikuta nikitupiwa swali na jamaa yangu mmoja kwa utani baada ya kusoma makala yangu moja iliyokuwa na kichwa cha habari: “Kupuuzwa kwa Utamaduni: Hii ndo fursa ya wasanii kuchangia maoni yao kwenye rasimu ya Katiba mpya”.

Nilimtazama kwa mshangao nikiwa sielewi alichokuwa akimaanisha. Alitabasamu na kuketi kando yangu akiwa kashika gazeti, nikalitupia jicho na kuuona ukurasa aliuokuwa akiusoma.

Jul 18, 2013

KUPUUZWA KWA UTAMADUNI: Hii ndo fursa ya wasanii kuchangia maoni yao rasimu ya Katiba mpya


Jaji Joseph Sinde Warioba

BAADA ya uhuru mwaka 1961, iliundwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23 mwaka 1997 mjini Dodoma ikiwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.

Jul 4, 2013

Umuhimu wa Shirikisho la Filamu Tanzania ni kwenye misiba tu?

Linathaminiwa wakati wa misiba ya wasanii tu na kutupwa katika shughuli zingine za kijamii



Sehemu ya umati wa watu katika Tamasha la Filamu jijini Mwanza

Mmoja wa wasanii wa Bongo Movie, Jacob Steven (JB), 
akigawa vyandarua jijini Mwanza

NI asubuhi tulivu ya Jumatano, siku moja tu baada ya kumalizika kwa ziara ya kiongozi mkuu wa taifa linaloongoza duniani la Marekani, Rais Barack Obama, aliyeondoka nchini baada ya ziara yake ya siku mbili. Nikiwa nimekaa sebuleni nikifuatilia kipindi cha televisheni cha ‘Tuongee Asubuhi’ kinachorushwa na moja ya vituo vya runinga hapa nchini, ambapo kulikuwa na mada iliyosema “Nafasi ya filamu katika soko la kimataifa”.

Katika mada hii, walialikwa wasanii wa jijini Mwanza, Hussein Kim, Prosper Kiri na Anita Kajumulo, na Dar es Salaam kulikuwa na Steve Mengere na Mwakilishi wa TBL wa kinywaji cha Grand Malt, Fimbo Butala. Mada hii ilijikita zaidi kulielezea Tamasha la filamu linaloendelea jijini Mwanza chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji cha Grand Malt.

Jun 6, 2013

KUELEKEA 1 JULAI 2013: Hivi tuna uhakika na mfumo wetu wa urasimishaji?

Sina hakika kama kuna nia ya dhati kumkomboa msanii


Wadau wa sanaa wakichangia mawazo yao kwenye Jukwaa la Sanaa linaloendeshwa kila Jumatatu na Basata

FILAMU zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi.


Katika karne hii, teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali vimeitangaza sana tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea. Hata hivyo, filamu nyingi zinazosambazwa kimataifa na kupenya soko la nchi nyingi ni zile zinazozalishwa nchini Marekani na baadhi ya nchi za  Ulaya. Ukweli huu, pamoja na kutambua nguvu ya filamu “inayoyumbisha mioyo na akili za watu” unaamsha wasiwasi kwa walio wengi.

May 30, 2013

Vita ya bidhaa bandia ianze na maudhui






KWA siku za karibuni tumekuwa na mazungumzo ya kina kati Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na taasisi zingine kuhusu mpango-mkakati wa nam,naa ya kudhibiti bidhaa bandia na hafifu (counterfeit and substandard) zinazotishia uhai wa soko la kazi za Kitanzania zikiwemo kazi za sanaa (filamu na muziki).

Siku hizi imekuwa si jambo la ajabu kusikia au kushuhudia bidhaa kama nondo za ubora hafifu, betri, TV, mafeni, breki za gari, dawa nk. Jambo hili limekuwa likituumiza mno na sasa tumelishuhudia kwa kasi likivamia sekta ya sanaa kwa kiwango kikubwa na kutishia uhai wa soko la filamu na muziki, hasa kwenye bidhaa kama DVDs, CDs, Tape, Vifungashio (Packaging system) nk, ambazo zinahusiana moja kwa moja na sanaa la filamu. Inaudhi mno pale unaponunua sinema (DVD) unayotegemea kwenda kuangalia nyumbani lakini unapoiweka kwenye deki unaitazama mara moja tu, ukiirudia unagundua kuwa inakwama, na wakati mwingine hugoma hata kabla haijaangaliwa!

May 16, 2013

KILIO CHA WASANII KUIBIWA: Je, ni kweli msanii muigizaji ana hakimiliki?


Mmoja wa wasanii waigizaji nchini, Issa Mussa maaruf kwa jina la Claude

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema

MAKALA yangu ya wiki iliyopita iliyohusu mikataba ya wasanii imezua maswali mengine kutoka kwa wasomaji wangu, hasa kutokana na maswali kadhaa niliyoyaibua kuhusu ile hoja ya kilio cha wasanii kulia kuibiwa kazi zao. maswali niliyoyaibua ni kama: Je, ni kweli wanaibiwa? Na kama wanaibiwa, huwa wanaibiwaje? Je, ni kweli uharamia (piracy) wa kazi za filamu ndiyo tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu nchini? Kama ni kubwa lipo kwa kiwango gani? Hivi, wasanii wanayafahamu kweli matatizo yao ya msingi?

Baadhi ya wasomaji wamenitaka niyatolee ufafanuzi maswali haya ili hata wao waelewe kwa kina kinachotokea kwani nimezidi kuwaacha gizani. Ndiyo maana wiki hii nimekuja na swali litakalosaidia kutafuta majibu ya maswali haya; je, ni msanii wa filamu ana hakimiliki?

May 9, 2013

Malalamiko ya wizi wa kazi za Sanaa: Tuwe na elimu endelevu kuhusu mikataba


Biashara ya filamu huambatana na matangazo kama inavyoonekana kwenye picha hii

MAPEMA wiki hii nilipata nafasi ya kuhudhuria warsha ya siku tatu ya wadau wa filamu iliyokuwa na lengo la kutafuta njia nzuri ya namna ya kutatua matatizo ya wasanii na wadau wa filamu badala ya tabia iliyojengeka ya kumtafuta mchawi jambo ambalo limekuwa halitusaidii.

Warsha ilitokana na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudai kuibiwa kazi zao huku baadhi ya waliokuwa wakisukumiwa lawama wakiwa ni wamili wa maktaba za video na wenye mabanda ya kuoneshea video. Warsha hii pia ilikuwa na kusudio la kuangalia mzunguko wa biashara ya filamu nchini kuanzia inapotengenezwa hadi kumfikia mtu wa mwisho (mtazamaji). Warsha hii iliandaliwa na taasisi ya MFDI-Tanzania kwa lengo la kuangalia namna ya kutatua tatizo la usambazaji nchini.

Apr 11, 2013

Ili kudumisha maadili: Tuipe kipaumbele Idara ya Utamaduni


Mkurugenzi wa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Prof. Hermas Mwansoko, akiongea
jambo katika moja ya shughuli za Idara yake

BAADA ya uhuru Disemba 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na vijana, mwaka 1962, Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Lakini chakushangaza pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwa maisha ya watu, bado sera ya utamaduni imepewa nafasi finyu katika serikali yetu tangu ilipoanzishwa wizara ya kushughulikia masuala ya sanaa. Katika kipindi chote tangu mwaka 1962, shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi.

Mar 28, 2013

Unauza haki yako ili iweje?


Aliyekuwa Afisa Mtendaji wa COSOTA, Yustus Mkinga

SIKU ya Jumanne ya tarehe 26 Machi 2013, ambayo kwangu ilikuwa siku muhimu sana kwani ndiyo siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu, siku hii nilipata maliko wa kuitwa kwenye kikao cha mazungumzo kati ya COSOTA na Viongozi wa Mashirikisho (Muziki, Stadi za Ufundi, Filamu), niliingia kwenye kikao hiki kwa mujibu wa nafasi yangu ya Ukatibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania.

Mazungumzo yetu yalikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo kumtambulisha Afisa Mtendaji Mkuu mpya wa Cosota, baada ya aliyekuwepo kumaliza muda wake.

Jan 30, 2013

Kwa hili la Idara ya Utamaduni, tasnia hii itaendelea kuyumba


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenela Mukangara

SERIKALI imekuwa ikijinadi kuwa inawajali wasanii ndiyo maana imeamua kuutambua mchango wao kwa kuirasimisha tasnia ya burudani - hasa filamu na muziki – ili wasanii wafaidi jasho la kazi yao, na imekuwa ikionesha kwa vitendo kuwa karibu na wasanii pindi kunapotokea msiba wa msanii maarufu, ingawa bado kuna maswali kadhaa ambayo yanajitokeza na kuleta maswali makubwa zaidi kama kweli inawajali.

Inashangaza kuona kuwa Wasanii ambao Serikali inajigamba kuwajali hadi leo tunapojigamba kuingia kwenye urasimishaji bado hawana sera (ya filamu kwa waigizaji au ya muziki kwa wanamuziki) inayowaongoza katika kufikia mafanikio ya tasnia yao. Pia inashangaza kuona kuwa Idara muhimu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa sanaa nchini, ya Utamaduni limekuwa tatizo jingine kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa nchini.

Jan 23, 2013

Kwanini tuendelee kufuata nyayo badala ya kuongoza?


Ousmane Sembène, gwiji wa filamu barani Afrika

MAMBO ni tofauti kabisa, kile kinachotokea Nigeria ni tofauti na kile kinachotokea Afrika Kusini, Tasnia ya filamu ya Misri inaonekana kuwa na kiwango cha mbali mno ukilinganisha na ile ya Kenya, na nikijaribu kufupisha mambo, ni kweli soko la filamu barani Afrika ni soko tata kidogo. 

Nchini Nigeria, nadhani kilichoanza kutokea kinaweza kuwa mfano kwa hali ya soko hapo baadaye: Nollywood ilianza kama aina fulani hivi ya watu mfano wa wazimu/mhemko wa video za bajeti ndogo, zilizotengenezwa na wafanyabiashara zaidi kuliko watengenezaji wa filamu, na baadaye soko la ushindani likaanza kudai ubora na ndipo tulipoweza kuona filamu nzuri sana zilizokuja kuibuka baadaye kama ile ya Kunle Afolayan ya ‘The Figurine’.

Jan 16, 2013

Mkutano kati ya kamati ya serikali ya urasimishaji wa tasnia za filamu na muziki, wasambazaji na wazalishaji wa bidhaa za sanaa – Peacock Hotel, Januari 14, 2013



Dk. Vicensia Shule, akitoa dukuduku lake kuhusiana na changamoto za urasimishaji


Mkutano huo ulikuwa na ajenda zifuatazo:

i.                    Kufungua mkutano
ii.                  Kutoa muhtasari wa madhumuni ya serikali na hatua zilizofikiwa hadi sasa
iii.                Kuelezea hatua za upatikanaji wa stempu za kodi
iv.                Kupata taarifa ya hali halisi ya upatikanaji wa mashine za kubandika stempu
v.                  Kuzungumzia mikataba kati ya wafanyabiashara na wasanii
vi.                 Kupata maoni ya wazalishaji na kujua tofauti kati ya bidhaa zafilamuna bidhaa za muziki

Jan 3, 2013

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo yatuma rambirambi msiba wa Sajuki


Sadiki Juma Kilowoko (Sajuki) enzi za uhai wake

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, amewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha msanii Juma Kilowoko (Sajuki) kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa leo, jijini Dar es salaam, Wizara ya Habari, Vijana na Utamauni na Michezo imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha msanii huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya filamu hapa nchini.

Jan 2, 2013

Kwanini hatujifunzi kutoka Sekta ya filamu ya Afrika Kusini?


Moja ya kazi nzuri zilizotengenezwa Afrika Kusini

SEKTA ya filamu ya Afrika Kusini ni mahiri, inayokua na kuzidisha ushindani katika anga za kimataifa. Watengenezaji wa filamu wa ndani na wa nje wanatumia fursa mbalimbali zilizopo, maeneo ya kipekee - na gharama nafuu za uzalishaji na kiwango kizuri cha pesa ya Afrika Kusini dhidi ya dola ya Kimarekani, ambacho hufanya kuwepo unafuu wa hadi asilimia 40 katika kutengeneza filamu Afrika Kusini kuliko Ulaya au Marekani na unafuu wa hadi asilimia 20 zaidi kuliko Australia.

Kifo cha Sajuki chaacha simanzi nzito


Sajuki, enzi za uhai wake

Watu wengi wamepokea taarifa ya kifo cha Msanii maarufu wa filamu nchini Tanzania Sadiki Juma Kilowoko au Sajuki kama ambavyo anajulikana na wengi aliyefariki dunia alfajiri ya kuamkia leo katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salam alikokuwa akitibiwa.

Sajuki anajulikana na wengi kwa sinema zake za kashkash alikuwa akiugua maradhi ya muda mrefu mpaka kufikia hatua ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.