Waandishi mahiri wa script Tanzania, Dk.Vicensia Shule na Bishop Hiluka, katika moja ya mikutano ya Bodi ya Filamu |
Ikiwa una matumaini kuwa
siku moja utakuja kufanya kazi ya uandishi wa script kwa ajili ya filamu au
televisheni, basi unahitaji kuwa na ufahamu wa jinsi ya kuandika “spec” script. Spec Script
ni kifupi cha Speculative script, huu ni
uandishi wa filamu wa kubahatisha
(speculation),
ambao kama mwandishi unaandika script yako ukiwa hujui nani atakuja kutumia
script hiyo – hii humaanisha kuwa unaandika
script bure (pasipo kulipwa au kuajiriwa na mtu). Kwa maana
nyingine ni kwamba hakuna mtu aliyekuajiri au anayekulipa kuandika script hiyo.
Unaandika
ukiwa na matumaini ya kuja kuuza kwa mnunuzi yeyote atakayevutiwa
na kisa chako au kuajiriwa kwa ajili ya
kuandika script kwa sababu ya hiyo, lakini ili kuwa na nafasi au uwezekano,
huna uchaguzi bali kuandika spec script.
Ili uwe katika upande ulio salama ‘Spec scriptwriter’ anapaswa kusimamia
misingi na sheria imara za uandishi wa filamu. Mara baada ya scrpt kununuliwa,
ndipo hubadilika na kufanywa kuwa shooting
script, ambayo pia huitwa production
script.
Production script ni toleo maalum la script iliyo tayari
kwa utayalishaji wa filamu, likijumuisha pamoja maelekezo ya kiufundi (technical instructions): kama vile
maelezo ya uhariri wa filamu, upigaji picha na mambo kama hayo.
Kosa kubwa ambalo Spec
scriptwriter au mwandishi mchanga wa filamu anaweza kulifanya ni
kuwasilisha script yake iliyojaa lugha ya kiutayarishaji (production language), ikiwa ni pamoja
na maeneo ambayo kamera inapaswa kuwekwa (camera angles) na maelekezo ya kiuhariri (editing transitions). Inaweza kuwa
vigumu sana kutokuweka aina hii ya lugha katika script yako unapoandika kwa
ajili ya filamu yako mwenyewe. Kwa kuwa, ni hadithi yako, unaandika script
utakayoitumia mwenyewe na unaiona katika namna maalum sana.
Hata hivyo, ukweli utabaki kuwa ukweli tu. Kama unaandika
script ambayo unataka kuiongoza mwenyewe, basi jaribu kwenda katika njia
wanayotumia watengenezaji wengine wa filamu wa kujitegemea (independent filmmakers). Lakini kama
nia yako ni kuandika script utakayoiuza kwenye makampuni au studio kubwa, basi
ni bora usimamie katika mfumo na muundo uliokubalika wa uandishi wa filamu.
Unapoandika (spec script) kwa ajili ya televisheni mara
nyingi hutegemea moja ya mambo mawili: Ni ama
unaandika kutokana na sehemu ya yaliyopo (existing episode) kwenye ‘show’
husika ya televisheni au ni kazi mpya (original piece of work) ya majaribio
(pilot).
Kuandika episode ya vichekesho (comedy) au drama series, njia rahisi ya kufanya ni hii: Kwanza, amua unataka kuwa mwandishi wa televisheni wa aina gani. Je, unavutiwa zaidi na comedy au drama? Ni aina gani ya show unayoifurahia ukiwa kama mtazamaji? Tengeneza orodha ya show zako uzipendazo (favorite) za televisheni. Anza kujiuliza mwenyewe, ni show ipi kati ya hizo inayoweza kuwa ‘fun’ zaidi kuiandikia. Kwa mfano, kama unapenda zaidi ‘CSI’, ‘24 HRS’ au ‘LOST’, basi hufai kuwa mwandishi wa comedy. Lakini kwa upande mwingine, kama unapenda drama zenye mchanganyiko wa vichekesho, kama ‘Desperate Housewives’ au ‘Ugly Betty’, basi uchaguzi mzuri ni kuwa mwandishi wa comedy series.
Unaweza
kuwa mwenye vipaji vingi (multi-talented) kuandika vyote; comedies na drama, na unaweza kupata nafasi ya
kufanya hivyo. Lakini kwa ‘spec scriptwriter’ mpya, ambaye hajajitangaza
akafahamika, ni muhimu sana kama utaelekeza (focus) juhudi yako kwenye jambo moja. Itakusaidia kukuondoa katika
list ya waandishi wapya wenye kiburi na ujinga wanaodhani wanaweza kuandika
katika kila aina ya hadithi (genre), na hivyo kujiharibia.
Ukishafanya
uamuzi kuwa wewe ni mwandishi wa comedy au drama, kinachofuata ni kuamua ni
onesho (show) gani utaliandikia episode. Kwa kufanya hivyo, hebu angalia
orodha ya shows zako uzipendazo. Ni show ipi maarufu zaidi? Ni ipi yenye msisimko (buzz)
zaidi ndani yake?
Unachotakiwa
kufanya hapa ni kuondoa shows ambazo watu wachache (tofauti na wewe) wanaziangalia
au hata kuzifahamu. Fikiria zaidi kuhusu watazamaji wako ni kina nani – watayarishaji
wanaotazamiwa na waandishi wengine. Hivyo, chagua show ambayo wote mtaipenda.
Kuandika episode ya show itakayosisimua
zaidi itafanya watu wakufahamua kwa haraka zaidi na hivyo kujiongezea nafasi
nzuri ya kuaminika.
Kisha anza kujifunza kuhusu muundo
(format) wa show. Unataka kuelewa jinsi show inavyoandaliwa kwa mtazamo (perspective) wa kiuandishi. Kusema ukweli, hutataka tu
kuangalia episodes nyingi uwezavyo, lakini pia utataka kufuatilia baadhi ya scripts
ikiwezekana. Siku hizi zipo wavuti (websites) ambazo script
mbalimbali zimehifadhiwa, ambazo unaweza kuzipakua (download) ili kuangalia.
Lakini kuwa
makini usije kupakua “transcript”. Transcript ni nakala tu isiyo na cha zaidi, yenye mazungumzo yaliyosikika kwenye
movie au michezo ya televisheni. Unatakiwa kupata script halisi inayohusisha
mazungumzo yote, matendo, maelekeo na maelezo.
Mara
upatapo scripts kadhaa, anza kufuatilia jinsi show inavyojengwa (structured). Je, ina hadithi “A” (hadithi
kuu) pamoja na hadithi “B” (hadithi nyingine ambayo kwa kawaida si muhimu sana),
au labda hata hadithi “C” (storyline ndogo ambayo hujifunua kwenye background ya
episode husika)? Unazijua sauti za kila mhusika? Nini kinawafanya wawe wa kipekee? Je, wana maneno fulani wanayosema
au wana ishara au mambo maalum wanayopenda na kuyachukia? Weka maelezo (note) ya kila unachofikiri
kinaweza kuwa na manufaa kwako unapoendelea kundika episode yako uliyoichagua.
Na
unapokuwa tayari kuanza mchakato wako wa furaha (na kutisha) wa kuandika ‘spec
script’ yako, elewa kuwa hakuna njia sahihi au potofu ya kuandika script. Unatakiwa kufanya chochote kitakachoonekana
kufanya kazi kwako. Mimi mara nyingi hupendekeza kuanza na “Outline” ya mambo ya
msingi ya hadithi na kisha polepole ongeza mambo mengine ikiwemo mazungumzo
kwenye kila eneo la tukio (scene) mpaka itakapoanza kuchukua sura halisi. Outline itakusaidia kuweka
hadithi yako kwenye mwelekeo na kuyaonesha mashimo yoyote yanayoweza kuwemo kabla
hujarukia ndani ya mazungumzo.
Outline kwa lugha rahisi ni waraka wenye mistari kadhaa
(inategemea na wingi wa scenes zako), kila mstari hulielezea eneo la tukio (scene) linalopaswa kuwemo kwenye script
yako. Kwa kuwa outline mara
nyingi si ndefu kama ilivyo “treatment”
(kitu kingine kinachohitaji muda zaidi kukielezea), ni vizuri zaidi
kuiandaa kabla hujaanza kuandika script yako. Outline hukusaidia sana kuuona mtiririko wa matukio moja baada
ya jingine unayotaka kuyaandikia script.
Kwa mfano:
1. Eneo: Chumbani – Onyesha mahusiano kati ya binti mdogo
(miaka 12) na mama yake
2. Eneo: Shuleni – Onyesha mazungumzo ya binti huyo na wanafunzi
wenzake kuhusu malezi hafifu anayopewa mama yake
3. Eneo: Ukumbi wa Muziki – Onyesha jinsi mama huyo anavyoonyesha
asivyojali malezi ya bintiye, anacheza muziki hadi usiku wa manane wakati
bintiye kabaki peke yake nyumbani.
Katika spec, huhitaji kutengeneza mhusika mkuu mpya (main
character) kwa ajili ya episode. Haijalishi ni namna gani atakuwa funny,
kwa kuanzisha mhusika mkuu mpya, unabadilisha mwenendo wa episode. Hawa ni
wahusika ambao watakwenda ‘beyond episode’ unayoandika.
Ukishaandika
rasimu yako ya kwanza (first draft), unahitaji kupata maoni katika mfumo wa “maelezo”
(notes). Ikiwezekana kutoka kwa watu ambao wanajua kutoa maelezo. ‘Maelezo’
hapa inamaanisha mkusanyiko wa mapendekezo muhimu ambayo yatasaidia kuboresha
ubora wa jumla wa ‘spec script’ yako.
Kumbuka,
kuna tofauti kubwa kati ya maelezo na maoni. Maoni ni mambo kama, “Nimeipenda”,
“Inavutia sana”, “Inatisha” - na mambo mengine kama hayo. Kusema ukweli,
maoni ni kazi bure. Unahitaji maelezo zaidi yanayojibainisha ambayo yatakusaidia
kurekebisha palipoharibika.
Jaribu
kuwapa script yako marafiki ambao ni waandishi au wapo katika sekta ya filamu –
au angalau wenye uelewa wa kina kuhusu ukosoaji unaojenga (constructive
criticism) ambao wewe unauhitaji. Ipitisha
script yako angalau kwa watu 3-4. Hii itakupa mwanga wa kutosha kuhusiana
na maoni, lakini pia utaanza kuona mambo mbalimbali yanayofanana katika ‘maelezo’
ambayo umepewa. Ukipata maelezo yanayofanana kutoka kwa watu watatu au
wanne tofauti, hayo ndiyo yanayopaswa kushughulikiwa zaidi.
Kisha chukua muda wa kufanyia kazi maoni yanayostahili kuhusu
mahitaji ya spec script yako. Mara upatapo maelezo yote mkononi, anza
kuandika upya (rewrite) spec script yako. Shughulikia maelezo unayokubaliana
nayo na yapuuze usiyokubaliana nayo. Kumbuka hii ni script yako, huhitaji
kukubaliana na maelezo yote ulilopewa hata kama unadhani huyahitaji.
Kuandika
upya inaweza kuchukua muda pia. Jipe muda unaohitajika. Mara nyingi Utajikuta
unafanya kwa “ukamilifu”. Unavyoandika zaidi ili kuboresha script yako, ndivyo
inavyokuwa bora zaidi. Kuandika ‘spec script’ inaweza kuwa mchakato wa muda
mrefu na mgumu. Lakini kama utaupa muda na maandalizi, nafasi ya kuandika ‘spec
script’ ambayo itafanikiwa – itakufanya sasa kuajiriwa rasmi kwa kazi hiyo!
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment