Wasanii wa Kundi la Sanaa la ABY, Malapa Buguruni |
Jacob Steven maaruf kwa jina la JB |
Ni wazi kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo
yaliyopatikana kwenye tasnia ya filamu nchini bila kutaja Nyota Academia, Kaole
Sanaa Group, Kidedea, Kidedea Original, Mambo Hayo na makundi mengine ya sanaa
za maigizo.
Kimsingi makundi haya ndiyo yaliwaibua wasanii
wakubwa nchini kama marehemu Steven Kanumba, Vicent Kigosi (Ray), Jacob Stephen
(JB), Yvonne Cherry (Monalisa), Blandina Chagula (Johari), Jengua na wengine
wengi ambao wanaendelea kuipeperusha vyema bendera ya filamu za Bongo ndani na
nje ya Tanzania.
Makundi ya sanaa za maigizo bado yapo, tena
siku hizi yamekuwa mengi zaidi. Takriban makundi matatu hadi matano kwa kila
kata hasa jijini Dar es Salaam huku mengine yakiwa hayana hata usajili kutoka
Basata.
Hata hivyo, licha ya makundi haya kuwa
mengi na kuashiria kwamba Tanzania tuna vipaji vingi lakini bado naona utofauti
mkubwa wa ubora kati ya makundi ya sasa na yale zamani.
Haya ya siku hizi yameacha kutoa wasanii
kama Kemi wa Kaole, Tabia wa Kidedea (kwa sasa ni marehemu), Richie Richie wa
Nyota Academia na wengine wa mfano huo.
Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa siyo
sekta ya kuzalisha waigizaji bora bali ni sehemu ya kupotezea muda kwa wale
wasiokuwa na kazi. Mengi yamesheheni watu wanaopenda kujionyesha lukuki kuliko
kuwa na shauku ya kutimiza ndoto zao za kimaisha kupitia sanaa ya maigizo.
Hali hiyo imesababisha wachache wenye nia
ya dhati ama kuvunjika au kuvunjwa moyo na wengi waliojiunga na makundi haya
wakidhani kwamba baada ya wiki mbili wataonekana kwenye runinga na kuwa maarufu
kama wasanii waliotangulia.
Makundi mengi ya siku hizi yamesheheni
walimu wasio na sifa wasioifahamu kwa kina sanaa pana ya maigizo. Wengi ni
wenzangu na mimi ambao wamejipachika taji la ualimu mara tu baada ya kuigiza
kwenye filamu mbili tatu ambazo hazijauza hata kopi mia moja.
Nao tayari wamejiona wamekwiva kuwafunza
wengine na matokeo yake ni kujazana ujinga kwa kusifiana wenyewe kwa wenyewe kila
wanapokutana kwenye mazoezi. Wanasahau kwamba sanaa ya uigizaji ni kazi kama
ilivyo uhasibu na ukandarasi. Sanaa hii imewahi kubadilisha maisha ya baadhi ya
watu duniani, kutoka walalahoi kuwa mabilionea hivyo ni tasnia inayotakiwa
kuheshimiwa tena siyo kidogo.
Makundi mengi ya siku hizi yamesheni michango kila
kukicha tena mingi ni ile iliyokosa kichwa wala mkia. Pia hiyo inasababishwa na
makundi haya kugubikwa viongozi wenye njaa, wasio na kazi wala kibarua hivyo
kuamua kuwageuza wasanii kuwa kitega uchumi.
Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa kichaka cha wapenda
ngono zembe. Ngono ya kuchanganyana wenyewe kwa wenyewe. Pia, mara nyingi
uchafu huo hufanywa na watu wenye vyeo ndani ya makundi haya. Usishangae
mwalimu, mwenyekiti au hata katibu wa kundi akawa na uhusiano na wasichana
zaidi ya watatu katika kundi hilo hilo moja.
Mchezo huu mchafu umekuwa moja ya magonjwa
sugu yanayosababisha kufa kwa makundi haya kwa sababu pindi wasichana husika
wanapogundua kuwa wanachanganywa huzua tafrani na kutoelewana na husababisha
kundi kuyumba na hata kuvunjika kabisa.
Makundi mengi ya siku hizi yametawaliwa na
wasanii wasiokuwa na uvumilivu, wengi hutaka mafanikio ya haraka. Hawataki
shida wala tabu ya kutangatanga ili kutafuata nafasi zaidi za kuonyesha uwezo
ama kipawa walichojaaliwa na Mungu.
Wamekaa wakisubiri fursa ziwafuate kwenye
makundi yao. Pengine walitakiwa kupata nafasi ya kukaa na watu ambao
wamefanikiwa kutoka na wawaeleze jinsi mlima wa kukubalika ulivyo mgumu
kuupanda. Mtu asiye mvumilivu ni lazima ataishia kati tu. Msanii ni lazima
ajitoe mwenyewe, kuhangaika huku na kule ili kutafuta chochoro ya kuibukia
kileleni kwani siku nzote hakuna ‘shortcut’ ya mafanikio.
Makundi mengi ya siku hizi siyo ya muda
mrefu, mengi huanzishwa na kudumu kwa miezi michache kabla ya wanakikundi
kusambaratishwa na sababu hizo nilizotangulia kuzisema.
Hata hivyo, bado nina matumaini na makundi
ya sanaa za maigizo, naamini kama wanavikundi wataamua kufanya kazi kweli, basi
wale wauza sura wataogopa hata kusogeza pua zao karibu na makundi haya. Wasanii
wa kweli pekee ndiyo watakaosalia na kazi itafanyika.
Wale walimu wasio na sifa nao watatafuta shule
za sanaa na kusoma ili watakaporudi kwenye makundi yetu wawe walimu wa uhakika
na watuivishe vilivyo. Viongozi wanaojifanya viwembe kwa kuwachanganya madada
zetu nao watakoma na hata ile michango yao ya ovyoovyo itapungua kama siyo kufa
kabisa na tasnia yetu itasonga.
Source: http://mobile.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment