KILA mtu aliyezaliwa na
mwanamke anacho kitu cha pekee alichojaaliwa kuwa nacho. Kitu hiki si umbile
lake, elimu yake, umaarufu wake, usomi wake, cheo chake katika jamii, au
utajiri wake wa vitu na fedha; la hasha, bali ni kipaji chake.
Kipaji ni uwezo wa kiasili
ulio ndani ya mtu katika maumbile, nafsi na roho yake. Kipaji kinatoka ndani
yake. Ni tunu au zawadi toka kwa Mungu ambayo hakuna anayeweza kutunyang’anya
au kutuibia mpaka tutakapokufa.
Fedha na magari vyaweza
kuibiwa, nyumba inaweza kuanguka, kubomoka, kubomolewa au hata kuungua, lakini
vipaji hubakia kuwa nasi daima.
Kipaji ni karama. Ni zawadi anayokirimiwa mtu kutoka kwa
Mungu. Kipaji hiki hukua katika ufanisi na matumizi ikiwa kitakuzwa na
kuendelezwa na kimenuiwa kutumika kwa niaba ya vingine, si kwa ajili ya
ubinafsi bali kwa faida ya wengine na si yake wenyewe.