Aug 12, 2018

Tupaze sauti dunia ijue kuhusu michoro ya Tingatinga


SANAA ya ufundi ambayo inajumuisha uchoraji, upakaji rangi picha, ufinyanzi, uchongaji na utengenezaji wa mapambo mbalimbali ya asili ni utamaduni ambao, kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, ilianza nchini Tanzania.

Sanaa ya uchoraji ilianzia nchini Tanzania takribani miaka 5,000 iliyopita na uthibitisho halisi ni michoro iliyopo katika mapango ya Kondoa Irangi.

Kwa miongo kadhaa, Tanzania imejulikana kwa umahiri wa uchoraji wa picha licha ya kuwa Watanzania wenyewe wametajwa kujiona kuwa siyo walengwa husika wa sanaa hii.
Sanaa ya uchoraji ni lugha ambayo ina ulingo mpana na kila msanii ana lugha yake na wapo wasanii ambao wanafanana katika mfumo wa sanaa wanayofanya na wengine hawafanani kabisa.


Ni sawa na msanii wa muziki anakuwa na mashabiki ambao wanapenda aina fulani ya muziki, kwa mfano anayependa muziki wa reggae anaweza asiwe mpenzi wa muziki wa taarab, vivyo hivyo hata kwenye michoro wapo mashabiki ambao wanapenda rangi, muonekano wa picha au mada inayowakilishwa kwenye picha.

Tanzania tunavyo vitu vingi vizuri ambavyo huwezi kuvikuta sehemu nyingine: Mlima Kilimanjaro, mbuga ya Serengeti, Ngorongoro Crater, madini ya tanzanite, chipsi zege, mchele wa Kyera n.k. lakini tumeshindwa kuvitangaza, jambo linalokatisha tamaa.
Changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kulinda ubunifu wa wabunifu/ wasanii ili waweze kufaidi matunda ya jasho lao. Ulinzi wa ubunifu huu huitwa Miliki Bunifu (Intellectual Property).

Mara nyingi wizi wa kazi za ubunifu hauchukuliwi kama wizi kwa kuwa ubunifu si mali zinazoshikika (zinazohamishika na zisizohamishika) bali zisizoshikika ambazo hazitajwi kabisa kwenye sheria mama, ndiyo maana pamoja na sheria kuweko, serikali huzilinda kama fadhila tu. 

Kwa mfano, michoro ya Tingatinga ni miongoni mwa sanaa maarufu sana duniani, inayopendwa na iliyofanikiwa kupenya soko la kimataifa lakini wengi hawajui kama asili yake ni Tanzania.

Kwa Tanzania Tingatinga imekuwa maarufu tangu miaka ya sabini na kadri muda unavyozidi, ubunifu wa picha hizi pia unakua kila kukicha.

Kwa wengine, Tingatinga ni michoro inayotukumbusha jinsi tulivyouona ulimwengu tulipokuwa watoto. Tuliuona kuwa wenye kufurahisha na wenye rangi za kuvutia.
Michoro ya Tingatinga huonesha wanyama na tamaduni za Afrika, hasa zile za Tanzania, ambapo ndiyo chimbuko la sanaa hiyo. Sanaa hii ilipewa jina la mwanzilishi wake, Edward Said Tingatinga.

Machapisho mbalimbali yanaonesha kuwa Edward aliyezaliwa mwaka 1932 na kufa 1972, alipokuwa akikua alivutiwa sana na eneo la porini na wanyama mwitu waliokuwa karibu na kijiji chao kusini mwa Tanzania.

Alipokuwa na umri wa miaka 25 hivi, aliondoka nyumbani kwenda kutafuta kazi na maisha bora.

Baadaye, alihamia jijini Dar es Salaam, na akaajiriwa kuwa mtunza-bustani. Wakati wa jioni, kipawa chake kilijidhihirisha kupitia kuimba na kucheza dansi; hata alikuja kujulikana sana kama mtumbuizaji.

Maisha ya Edward yalibadilika ghafula mwaka wa 1968. Alipata kazi ya kuwasaidia wauguzi na madaktari katika hospitali ya umma ya Muhimbili mjini Dar es Salaam.

Akiwa huko, alianza kuchora kumbukumbu na mambo yaliyomvutia utotoni kwa kutumia aina ya uchoraji aliobuni mwenyewe. Na hapo ndipo sanaa ya Tingatinga ilianzia.

Hakukuwa na maduka yenye vifaa vya kuchorea kama vile brashi maalumu, rangi za kawaida na zile za asili, na vifaa vingine ambavyo Edward angeweza kutumia. Kwa hiyo, alitumia vifaa ambavyo kila mtu angeweza kununua katika duka linalouza vifaa vya ujenzi.

Kwa mfano alitumia rangi inayong’aa ya kupaka baiskeli, na ubao wa aina fulani ambao upande wake mmoja ulikuwa laini na uling’aa, na ambao ulifaa kabisa kuchorea picha zinazometameta.

Kuanzia na mchoro wake wa kwanza kabisa, sanaa ya Tingatinga imekuwa ikitumia rangi angavu na maumbo sahili. Hata hivyo, kadiri ambavyo miaka imepita, mtindo huo umeboreshwa na sasa kila picha ina madoido na maumbo kadhaa. Wasanii fulani huchora watu, wanyama, na vitu vingine vingi.

Michoro ya kisasa ya Tingatinga hujaribu pia kuonesha watu wa Afrika na tamaduni zao. Mchoro unaweza kuonesha pilikapilika kwenye soko lenye shughuli nyingi, wagonjwa kwenye zahanati, au maisha ya kawaida kijijini.

Tangu ilipoanzishwa, sanaa ya Tingatinga imewapa watu wa Afrika wenye vipawa vya kuchora nafasi ya kueleza wanachofikiri, na wakati huohuo wakijiletea mapato ya ziada.

Pamoja na utajiri mkubwa wa kihistoria katika upande wa utengenezaji na uuzaji wa picha za Tingatinga, bado kama nchi na waasisi wa sanaa hii hatujafaidika kabisa badala yake tumeshuhudia wajanja wachache wameipoka na kutengeneza mabilioni ya dola za Marekani.

Julai 2008 wachoraji wa Tingatinga nchini walitembelewa na moja ya kampuni kubwa za filamu ya Uingereza - Tiger Aspect Productions. Ujumbe ulikuwa kwamba filamu za watoto zinazotokana na sanaa ya Tingatinga zingeanza kuhuishwa na hii ingeifanya sanaa ya Tingatinga kuongeza umaarufu wa Sanaa nchini Tanzania.

Umoja wa Wachoraji wa Sanaa ya Tingatinga walisaini makubaliano na Tiger Aspect Productions kutoa wachoraji wenye ujuzi wa sanaa hii kwa studio mpya yenye makao yake jijini Nairobi.

Wasanii wa Tingatinga waliifurahia fursa hii mpya na matarajio yalikuwa makubwa kuwa wateja wengi wangekuja Tanzania kununua picha za Tingatinga.

Hapo ndipo tulipopigwa bao la kisigino kwani badala ya fursa hiyo kuja nchini ikaenda nchini Kenya, ambapo Kampuni ya Homeboyz walitumia nafasi hiyo kujipatia dola za Marekani bilioni 2 kwa michoro ya Tingatinga ili itengenezwe filamu za watoto maarufu kama ‘Tingatinga Tales’.

Ukisoma machapisho mbalimbali utashtuka kuona kuwa Tingatinga Tales zinatambuliwa kutoka Kenya, hivyo kuwafanya Wakenya kupata mirabaha/ gawio kupitia Tingatinga Tales.

Ni wakati sasa tupaze sauti zetu na kudai haki yetu, ili hiyo mirabaha, gawio au vyovyote iwavyo ianze kulipwa kwa nchi yetu, kwani ni haki yetu inayotokana na wabunifu wetu ambao kwa kweli wanastahili kufutwa jasho kwa kazi yao njema iliyotukuka.

No comments: