TANZANIA ni moja ya sehemu bora kabisa duniani
ambazo msanii atafurahia kutengeneza filamu yake au kupigia picha za video kwa
muziki wake, historia, utamaduni na wanyamapori.
Kuna hali ya hewa nzuri na watu wakarimu ambao
wako tayari kumkaribisha mgeni katika mtazamo wa Kitanzania.
Imekuwa inashangaza kuona wasanii wetu wanakwenda
kufanya video zao Afrika Kusini na Kenya, wakati Tanzania inashika nafasi ya pili
duniani, nyuma ya Brazil, kwa kuwa na vivutio vingi vya
utalii huku nchi ya Afrika ya Kusini ikishika nafasi ya 14.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti
uliofanywa na Shirika la Habari la CNN la Marekani. Hata hivyo, kulingana na
utafiti huo, Tanzania katika mapato na miundombinu yanayotokana na sekta ya
utalii inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 duniani!
Tujiulize, ni kwa namna gani sanaa inaweza kuitangaza
nchi? Hebu tuchukulie mfano wa Nigeria… tuanzie kwenye filamu zao, zimeweza
kuwatangaza kwa kiasi gani? Tutapata jibu la haraka kwamba taifa hilo
limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala cha chini.
Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la
Afrika na dunia, haiwezi kutufanya tuumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo
limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa ya maigizo, na zaidi kuvuta
watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.
Baada ya hapo, fikiria ni kwa kiasi gani kundi la
muziki la P-Square limefanikiwa kuifanya Nigeria kuwa taifa linalotajwa mara
nyingi na watu mbalimbali duniani kila yanapoibuka mazungumzo au majadiliano ya
kukua kwa muziki barani Afrika? Je, tunaweza kuona matunda ya wanamuziki
kufanikiwa?
Tangu mwaka 1983, Nigeria ilishaanza kung’ara
kimataifa kupitia sanaa. Kuchomoza kwa mwanamuziki Sunny Ade, kisha kampuni
kubwa ya muziki duniani ya Island Records kubeba jukumu la kutangaza muziki wa
staa huyo, kuanzia albamu yake “Synchro-System” hadi ziara zake, kulifanya watu
wa mataifa mbalimbali kuanza kuifuatilia Nigeria.
Ongezea mafanikio ya wanamuziki wa kizazi kipya:
2face Idibia, D’Banj, Davido, Wizkid, Iyanya na wengine wengi. Utapata jawabu
ni kwa kiasi gani, sanaa imeiweka Nigeria kwenye ramani ya dunia.
Mamilioni ya watu huingia Nigeria kila mwaka kwa
shughuli mbalimbali za utalii lakini zaidi kuona na kujifunza namna wasanii wa
nchi hiyo wanavyofanya sanaa za filamu na muziki.
Juni 2000, Benki ya Dunia kwa kutambua umuhimu wa
sanaa na nguvu yake kwa ukombozi wa kiuchumi kwa vijana wenye vipaji, ilifanya
kongamano la kujadili njia za kusaidia maendeleo ya muziki kwa nchi sita za
Bara la Afrika: Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Nigeria, Senegal na Mali.
Kwa nyongeza tu hapo ni kuwa nchi zote ambazo
zimetajwa, kutoka mwaka 2000 hadi 2010, kila moja imetengeneza wanamuziki
ambao, uwezo wao wa kifedha kwa kulinganisha na sarafu ya Tanzania, ni haki kuwaita
mabilionea.
Swali; Kama Benki ya Dunia inaweza kuwekeza kwenye
sanaa Afrika kwa kuamini inaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi katika uwanja mpana,
ni kwa nini Tanzania mpaka leo, hatujaifanya sanaa kuwa sekta rasmi ili itumike
katika mageuzi ya kiuchumi?
Tangu mwaka 2000 baada ya kongamano la Benki ya
Dunia, Ghana imefanikiwa kuingiza fedha nyingi katika Pato la Ndani la Taifa
kupitia sanaa, hasa baada ya wanamuziki wake kufanikiwa kupenyeza kazi zao
katika mataifa mbalimbali duniani. Afrika na nje ya Bara ya Afrika.
Ushuhuda mkubwa ambao Ghana inao kupitia maajabu
ya sanaa ni kutanuka kwa sekta ya Utalii baada ya wasanii wa nchi hiyo
kufanikiwa kutamba kimataifa.
Leo hii, Ghana inapokea mamilioni ya wageni wanaotembelea
vivutio mbalimbali, ikiwemo sanaa, lakini sababu kuu ni kwa kuvutiwa na kazi za
wasanii.
Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Ghana and the World Music Boom’, kilichoandikwa na John Collins,
mkufunzi katika Shule ya Sanaa za Maonesho katika Chuo Kikuu cha Ghana, yameelezewa
mafanikio ya Ghana kiutalii, baada ya wasanii wa Ghana kufanikiwa kutamba nje
ya mipaka ya nchi hiyo.
Mwaka 2003, Ghana ilianza kuwa na ingizo kubwa la
wageni, hivyo kuinufaisha sekta ya Utalii. Jumla ya watu 550,000 waliingia Ghana,
ikiwa ni mara mbili zaidi ya kabla sanaa haijawa na umaarufu wa kimataifa.
Taarifa imeongeza kuwa mwaka 2004, idadi ya
watalii ilipanda kwa 100,000 zaidi hadi kufikia 650,000. Yaani kadiri sanaa ya
Ghana ilivyokuwa inavuma kwenye soko la kimataifa, ndivyo na wageni
walivyomiminika nchini humo kushuhudia “yaliyomo”, hivyo kuwa na matokeo mazuri
katika ingizo la pato la kigeni.
Kwa mujibu wa Collins, hivi sasa Ghana inapokea
mamilioni ya wageni kila mwaka kutokana na mchango mkubwa wa sanaa. Na
inatambulika rasmi kwamba sanaa nchini Ghana inawezesha sekta ya Utalii kushika
nafasi ya tatu kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya dhahabu na mbao.
Kabla ya sanaa kuchukua nafasi pana, mpaka mwaka
2000 sekta ya Utalii ilikuwa na wastani wa kuingiza dola za Marekani milioni
350. Mwaka 2004 baada ya mwamko mkubwa wa sanaa, Utalii ulifikisha ingizo la
dola milioni 800.
Kwa sasa utalii kila mwaka unatengeneza wastani wa
zaidi ya dola bilioni 3 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 6.7.
No comments:
Post a Comment