Diamond Platnumz akitumbuiza |
“HATUPO katika kizazi cha taarifa na maarifa. Tupo
katika kizazi cha BURUDANI na STAREHE.” Tony Robbins.
Tony Robbins ni mwandishi wa
Marekani, mjasiriamali, mwalimu na anajulikana kwa matangazo yake kwenye
runinga, semina na vitabu, ikiwa ni pamoja na ‘Unlimited Power’ na ‘Awaken the
Giant Within’.
Burudani ni biashara inayokua kwa kasi sana barani
Afrika zaidi ya kawaida. Sekta ya burudani imejaa fursa nyingi sana kupita
kawaida. Yeyote atakayeamua kuichunguza sekta hii kwa makini atashangaa fursa
zilizojaa.
Kila siku mamilioni ya watu duniani wanahangaika
kutafuta sehemu za kustarehe, vitu vya kujistarehesha na kujiburudisha, michezo
na matamasha ya kufurahisha.
King Majuto katika sinema ya Daladala |
Sekta ya burudani inatengeneza zaidi ya dola billioni 50 za Marekani kila mwaka. Sekta hii
inaongoza katika kutengeneza ajira kuliko sekta zote barani Afrika.
Afrika ikiwa kama sehemu ya kivutio cha utalii,
vipaji vya filamu na muziki bado vibichi. Dunia nzima inahamia Afrika kwa
sababu Afrika inaendelea kukua na kukua katika sekta ya burudani.
Sekta za Filamu na muziki zimekua kwa kasi zaidi
ya kawaida. Zimejaa vipaji visivyo na kikomo. Hii fursa bado mbichi sana
Tanzania. Japo watu wanafanya muziki au kutengeneza filamu lakini sekta hii bado
haijaguswa vya kutosha.
Pamoja na matatizo yake lukuki lakini ukichunguza
waigizaji au waimbaji, kama akina Joti, Masanja Mkandamizaji, Diamond Platnumz,
Ali Kiba n.k. wanaingiza pesa nyingi kwa mwezi kuliko hata wakurugenzi wa
kampuni Afrika.
Wasanii katika burudani ni zaidi ya watu wa
kawaida. Wapo juu ya kilele. Msanii katika burudani anaweza kuingiza pesa
nyingi ndani ya dakika tano pesa ambayo mtu mwingine anaweza kuipata kama
akikusanya pesa hizo tokea anapojitambua mpaka uzeeni.
Wao wanaweza kutengeneza ndani ya dakika tano na
serikali inaweza kujipatia kodi kubwa hapa ikiangalia kwa jicho la kiuchumi.
Sekta hii imejaa pesa nje nje kuliko kawaida,
lakini ukikutana na waigizaji wengi maarufu utasikitika kwa kuwa bado
hawajagusa kabisa sekta hii.
Kuna uzembe fulani wa kufikiri hapa na wanajua
hivyo. Hakuna malengo hapa. Kuna ubabaishaji uliopindukia. Hii ndiyo sababu
tunawasikia wanatumika na wanasiasa.
Msanii wa filamu ni mtu mkubwa sana duniani, siyo
mtu wa mchezo mchezo lakini wasanii wetu Mungu awasaidie maana hawajaamka,
ndiyo maana hata soko la filamu ni kama limeparaganyika.
Wako wapi wafanyabiashara wajanja Afrika waweze
kuichangamkia fursa ya filamu Tanzania? Watanzania wanatamani kuona filamu
zilizobamba lakini hazipo sokoni.
Hakuna filamu nzuri sasa. Wasanii waseme wenyewe,
mauzo ya filamu za Kibongo yakoje kwa sasa? Yameshuka kuliko kawaida. Hii
haimaanishi kuwa Watanzania hawapendi filamu, ila ni kwamba filamu za maana ni
chache mno kuliko maahitaji ya soko.
Hii ndiyo sababu filamu na series za nje,
hasa za Kikorea, China na India zilizotafsiriwa zinabamba… hebu fikiria kama
badala ya umaarufu wa series hizo, tufanye ingekuwa ni filamu mpya ya JB ni
kiasi gani cha kodi serikali ingekusanya?
Lakini hao wanaotafsiri hizo filamu wanalipa kodi?
Mnajua wanaharibu kwa kiasi gani sekta ya filamu Tanzania? Lakini tujiulize,
kwanini hivi sasa filamu hizo zinatamba na kupata umaarufu? Ni kwa sababu
wasanii katika tasnia ya filamu nchini walibweteka.
Walibweteka na kusahau kuwa sanaa ndiyo inayoweza
kutengeneza pesa nyingi sana kuliko hata kazi za kuvaa tai posta.
Lakini hali hii si kwa Tanzania pekee, hata
Nigeria (Nollywood) ambao mchango wa sekta ya filamu kwa
Taifa ni Naira bilioni 853.9 (Dola bilioni 2.37 za Marekani)
wamegusa kiasi kidogo sana katika sekta hii ya filamu Afrika.
Katika nchi kama Nigeria yenye matatizo ya ukosefu
wa ajira, Nollywood peke yake imefanikiwa kuajiri zaidi ya watu milioni 1 (bila
maharamia) na kuifanya sekta hii ya filamu kuongoza baada ya sekta ya kilimo.
Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu
inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa
ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa. Matokeo ya kukubalika kwa sinema
pia huwafanya watayarishaji wa sinema, waigizaji na watendaji wengine kuwa na
heshima kwenye jamii na hata kisiasa.
Mwanzoni Nollywood ilianza kama aina fulani ya
wazimu wa kutengeneza ‘home video’ za bajeti ndogo.
Filamu zilitengenezwa na wafanyabiashara zaidi
kuliko wanataaluma, na baadaye soko la ushindani likaanza kudai ubora na ndipo
tulipoanza kuona filamu nzuri zikiibuka baadaye, kama ile ya Kunle Afolayan ya
‘The Figurine’.
Swali ni kwamba tupo serious au suala lilikuwa ni
kupata umaarufu tu ili uweze kuwasaidia kwenye mambo mengine yasiyo ya kisanii,
kama kukimbilia kwenye siasa? Nini kimetusibu jamani? Siasa?
Wapo wasomi wengi mitaani wamefungwa na vyeti vyao
wakati wana vipaji lukuki na wana uwezo wa kuanzisha projekti za filamu
Tanzania lakini wamebaki kukosoa tu na wengine kulala fofofo. Siku wakija
kuamka watakuta kila kitu kimekwisha haribika.
Nimekutana na vijana wa kawaida sana hawajaenda
hata shule, hawajui hata kuandika lakini waliweza kujiajiri kupitia filamu na
walikuwa wanaingiza pesa kimchezo mchezo kuliko hata mameneja na wengi wao
walimiliki kampuni tena nyingi zikiwa hata hazijasajiliwa.
Hebu fikiria, kama kungekuwa ana utaratibu wenye
kueleweka nchi hii ingeingiza pato kiaso gani kupitia filamu pekee?
Waafrika wengi wanapenda starehe, Waafrika wengi
tunapenda kuburudishwa na hii ni fursa kwa wasanii.
Fursa katika filamu na muziki ni zaidi ya kawaida
hapa Afrika na hasa Tanzania. Waulize wazee wa fursa, wamiliki wa CMG,
utashangaa pesa wanazoingiza.
Milango iliyofunguliwa na fursa hii ni mingi, cha
ajabu watu ni wagumu kuingia: fursa hii imefungua milango mingine zaidi ya
fursa nyingine.
No comments:
Post a Comment