Wanamuziki Profesa Jay (kushoto) na MwanaFA |
MUZIKI kama chombo ambacho hutumiwa kuelezea
historia ya jamii, hupasha ujumbe maalumu kwa wanajamii, hasa kutoka kizazi
kimoja hadi kingine na hutumiwa kuelezea historia, imani, itikadi na kaida za
jamii.
Kwa kawaida nyimbo ni zao la mazingira ya jamii.
Zinaweza kufananishwa na mtoto ambaye hufinyangwa na mambo mengi
katika historia ya jamii yake.
Hii inamaanisha kwamba muziki hauibuki katika
ombwe tupu na hauwezi vilevile kujiundia mazingira yake yenyewe. Mabadiliko na
maendeleo ya muziki yamekuwa yakifuatana na historia ya watu wenyewe.
Umuhimu wa muziki unadhihirika katika matumizi ya
nyimbo katika wakati maalumu kama njia mojawapo ya kuanzisha mabadiliko katika
tabia za jamii au mtu binafsi.
Wanamuziki Diamond Platnumz (kushoto), Aslay (katikati) na Ali Kiba |
Muziki hutumika kama njia mojawapo ya kujifundisha utamaduni na aghalabu hutumiwa katika kumwelezea mtu, mazingira yake na jinsi anavyoweza kuyatumia na kuyatunza vilivyo.
Kwa Tanzania muziki
umekuwa unabadilika sana, wasanii wengi wamekuwa wakibuni mitindo ya aina
mbalimbali ili kuzifanya kazi zao ziende mbali na kuvuta mashabiki wengi wa
muziki nchini na duniani kwa ujumla.
Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine,
wakazi wa eneo ambalo hatimaye limekuwa nchi ya Tanzania, walikuwa na utamaduni
wao. Utamaduni huu ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na
kabila. Moja ya vipengele ilikuwa muziki.
Kiasili, hatukuwa na ‘muziki’ katika makabila yetu
kabla ya ujio wa wageni, lakini tuliimba, tulicheza ngoma,
tulipiga vyombo mbalimbali, ila tulikuwa na utamaduni mwingine kuhusu kitu hiki
tunachokiita siku hizi muziki.
Watafiti wanatuambia tulikuwa na ngoma, ambayo
tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki. Ngoma ilikuwa ni chombo kile kilichotoa
muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno, ngoma ya
mashetani na kadhalika, na pia tulicheza ngoma.
Ujio wa wageni ukatuletea muziki wa dansi ulioanza
kama klabu za watu walioalikana kucheza aina mbalimbali za muziki wa kizungu (ballroom
dancing). Kisha taratibu ukaumbika ukifuata muziki wa soukous kutoka Congo
(rumba ya Kikongo) na tokea hapo ikaitwa ‘rumba ya Tanzania’.
Katika wakati huo pia muziki wa taarab, wa
Waafrika wa Pwani, haukuachwa nyuma. Ni uimbaji wa mashairi uliofuata muziki wa
bendi uliotokana na tamaduni nyingi, hasa muziki wa Waarabu na Wahindi.
Baadaye miaka ya 1990 ukaibuka muziki wa Hip hop, ambao baadaye ukapata jina la
Bongo Fleva uliotokana na hip hop kutoka Marekani, ikiwa na ongezeko la athira
ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat, dancehall, na mitindo ya asili ya
Kitanzania kama vile taarab na dansi.
Jina ‘Bongo Fleva’ ni tokeo la matini
yaliyoharibiwa kutoka ‘Bongo flavour’, ambapo neno ‘flavor’ linamaanisha ladha
na ‘Bongo’ huchukua nafasi ya jina la utani la Dar es Salaam,
ambako aina ya mtindo huu inatokea.
Lakini kwa sasa Bongo Fleva inatafsirika kama
muziki wa Tanzania kwa sababu hivi sasa neno Bongo limekuwa na maana ya
Tanzania.
Hadi hapa sina tatizo na neno ‘Bongo Fleva’,
binafsi linanikumbusha mtangazaji Mike Mhagama wa Radio One 99.6 FM mwaka 1996
alipokuwa akijaribu kutofautisha na muziki wa R&B na Hip Hop wa Marekani
kupitia kipindi chake maarufu cha redio, 'DJ Show'.
DJ Show kilikuwa kipindi cha kwanza cha redio
kukubali wanamuziki vijana wa Kitanzania wenye athira ya muziki wa Marekani.
East Africa Radio nao walikuwa na kipindi cha ‘The
Cruise’ ambapo kulikuwa na kipengele cha ‘Bongo Explosion’, wakati Clouds FM walikuwa na kipindi kilichoitwa ‘Fleva ya Bongo’, na Redio
Uhuru walikuwa na kipindi cha ‘Deiwaka’.
Vipindi hivyo vyote vilianzishwa kwa sababu muda
huo mwamko wa vijana kurekodi nyimbo zilizoonekana za ‘kisasa’ ulikuwa mkubwa.
Hivyo, nyimbo hizo (bila kuzingatia aina ya muziki
ambao msanii aliufanya) zikawa nyingi na zikapata wapenzi wengi sana, hii ndiyo
ilifanya kuwepo kwa vipindi hivyo vya muziki huo.
Kwa kutokea hapo unaweza ukaona kuwa kumbe ‘Bongo
Fleva’ inamaanisha mkusanyiko wa nyimbo za vijana wa Kitanzania, yaani ‘kizazi
kipya’.
Kwa mtiririko huo, bado nina shaka kama jina Bongo
Fleva linapaswa kuwakilisha aina hii ya muziki unaoimbwa na vijana wa Kitanzania.
Aina fulani ya muziki unatakiwa uwe na sifa za
kufanana kimahadhi, vionjo, mpangilio, mirindimo na vitu vingine vyote
vinavyoufafanua muziki husika, ndiyo maana hip hop hata iimbwe kona gani ya
dunia bado utajua tu hii ni hip hop, kitu hicho hamna kwenye Bongo Fleva yetu.
Japo aina hii imewatangaza wanamuziki wetu kama
Diamond, Ali Kiba na wengineo lakini ukweli tunahitaji kuweka sawa vitu kwenye muziki
kwa ajili ya utambuzi, hii itawasaidia sana wanamuziki wenyewe, kwani kwa sasa
ni kama wanafanya kitu wasichokifahamu hivyo ni vigumu wao kuwa bora sababu
hakuna ‘standard’ za kuwapimia, hii nayo inachangia sana wasanii wengi (wa hiyo
Bongo Fleva) kuibuka na kupotea.
Bongo Fleva ni kitu tata kidogo, ndiyo maana
baadhi yao, hasa wanaojitambua hawapendi uwaambie wanaimba Bongo Fleva. Hata
sasa kuna tofauti ya wazi kati ya wanaoimba RnB, Hip Hop n.k.
Swali la kujiuliza: Je, njia tunayoenda nayo
katika muziki wetu inatusaidia kujenga juu ya msingi sahihi wa waliotutangulia
au tunapotea na wimbi la utandawazi? Kwanini tunakosa alama ya mfano wa muziki
wetu?
Kwa kweli fani ya muziki nchini ipo katika hatari
kubwa ya kupoteza dira kwani wanamuziki wanaotamba sasa (wa Bongo Fleva) hawafuati
miiko katika uteuzi wa maneno katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui
kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na
waliotutangulia.
Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka
kwa fani hii. Pengine unaweza kujuliza, tunawezaje kuwa na utamaduni wa muziki
mmoja wakati Tanzania kila kabila lina muziki wa asili yake, wenye sauti
tofauti?
Kitu kikubwa ni kwamba ngoma ni kitu cha kipekee
utakachokikuta kwenye muziki wa asili wa karibia makabila yote. Hivyo, muziki
wa Kitanzania usioongozwa na ngoma bado ni vigumu kuuita wa Kitanzania.
Kwa maana hiyo, hatuna aina yetu ya muziki kama
taifa na tusidanganyane, aina ya muziki wa taifa haitungwi kama tunavyotaka
kulazimisha kupitia Bongo Fleva bali ni matokeo ya historia yenyewe!
No comments:
Post a Comment