![]() |
Wachekeshaji mahiri nchini ambao kwa sasa ni marehemu, King Majuto na Sharo Milionea |
WIKI iliyopita
tasnia ya vichekesho na wapenda burudani tulipata pigo kwa msiba uliogusa na
kuwashtua watu wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa sanaa ya
vichekesho, kutokana na kifo cha King Majuto.
King Majuto ambaye jina lake halisi aliitwa Amri
Athuman alikuwa msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki, na gwiji wa vichekesho ambaye umahiri wake ulikuwa wa
aina yake.
Majuto alifariki dunia wakati akipokea matibabu
kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, majira ya saa 2 usiku
wa Jumatano Agosti 8, 2018 akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Baada tu ya kifo chake watu maarufu ndani na nje
ya Tanzania walituma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya
kijamii, miongoni mwao akiwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.
![]() |
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na King Majuto |
Rais Magufuli alisema kuwa King Majuto atakumbukwa
kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na
uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na
kuunga mkono juhudi za Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kuhimiza
maendeleo.
Kwa kweli King Majuto alikuwa mfalme katika tasnia
ya maigizo ya uchekeshaji nchini Tanzania na Afrika Mashariki, aliweza
kujizolea umaarufu mkubwa kupitia namna ambavyo alikuwa akiigiza na kuwa
miongoni mwa watu wenye mvuto mkubwa miongoni mwa wasanii.
Vyombo vya habari vilipotangaza kuwa
King Majuto alikuwa akiomba msaada wa shilingi 500,000 ili
kupata matibabu nchini India vilimuibua Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Dk Mwakyembe aliunda kamati ya wanasheria kwa
lengo la kupitia upya mikataba ya wasanii ili waweze kulipwa fidia zao na aliweza
kukutana na wasanii wa fani mbalimbali nchini kuzungumzia masuala kadhaa
ikiwemo wizi wa kazi zao na maslahi yao.
Hata hivyo, kabla ya kifo chake, King majuto aliamua
kuwasamehe baadhi ya waandaaji na wasambazaji ambao inasemekana walikuwa
wamemdhulumu mamilioni ya fedha baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutishia kuwashitaki watu hao.
Hili ni somo la kwanza linalotuhusu wote:
kusamehe. Haijalishi umeumizwa kiasi gani lakini unatakiwa kusamehe na kuyaacha
maisha yasonge badala ya kukumbuka yaliyopita ambayo yanaweza kukuumiza na
kukufanya ushindwe kupiga hatua kwenda mbele.
Kwa sasa wasanii wengi wameendelea kubaki wakilaumu
tu kuwa wameibiwa sana, wameweka visasi na vinyongo kiasi cha kusahau kuwa
wanatakiwa wasahau na kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua katika matatizo
waliyo nayo.
Lakini pia wanapaswa watambue kuwa katika biashara
yoyote makubaliano ya kazi ni muhimu sana kwa pande zote kuwa na haki na wajibu
wa kila upande. Katika jambo hili, umakini wa hali ya juu huwa unahitajika sana
ili kuepusha upande mmoja kuumizwa.
Na hili ni somo la pili: mikataba kabla ya kazi. Katika
suala la mikataba ni vyema kushirikisha wanasheria ambao ndiyo wataalamu wa
mikataba ili kuepuka kudhulumiwa, lakini pia kutokana na elimu ndogo ya wasanii
wengi, ni muhimu kuwa na wasimamizi (mameneja) wanaoelewa masuala ya mikataba.
Ni vyema wasanii wakatambua kuwa hata kama kuna
wizi wowote uliofanyika, basi hawakuibiwa bali mikataba waliyoingia ndiyo iliyowaponza.
Katika kipindi hiki tunachomuombolzeaa King Majuto
ni vyema kutafuta namna ya kutatua changamoto ya kuibiwa, lakini kwanza wasanii
wakubali mapungufu yao na pindi wanapoona mikataba kwa lugha ya Kiingereza
ambayo inawapa tabu walio wengi, ni vyema wakaikataa mikataba hiyo au kuipeleka
kwa watu wenye utaalamu na lugha hiyo, hasa wanasheria, na wasipende kuendekeza
njaa.
Lakini pia vyama vya sanaa na mashirikisho yanapaswa
kuwa na wanasheria ambao watasimamia shughuli za wasanii wao, ikiwemo
kuwaongoza katika kuingia mikataba.
Kwa kufanya hivi, wasanii wataweza kujiamini
katika utendaji wa kazi zao, kwani hawatakuwa na wasiwasi wa kunyanyasika pindi
washirika wao katika mikataba watakapoonekana wanakengeusha mambo.
Suala la mikataba limekuwa likipuuzwa sana na
Watanzania wengi (si wasanii tu), hasa linapokuja suala la kusoma vipengele na
kuelewa vinamaanisha nini. Wengi hukimbilia kuangalia sehemu inayotaja pesa tu
na wakiona pesa nyingi basi husaini bila hata kujali maeneo mengine muhimu.
Mikataba ya aina hii imesababisha vilio,
malalamiko na kesi za ajabu ambazo kimsingi zingeweza kuepukika endapo
kungekuwa na umakini kabla ya kuingia mkataba husika.
Bahati mbaya wasanii hawajifunzi kabisa kutokana
na makosa ya wengine, kwani inapotokea mwenzao kaingia mkataba wa aina hii
utashangaa hata watu wake wa karibu nao hurudia makosa kama hayo, kiasi kwamba
suala hili limekuwa kama ni desturi kwao.
Inakuwa vigumu kuelewa kama wanafanya shughuli zao
kwa mazoea na si kitaalamu, kwa maana ya kuifanya kazi yao kama ajira yao rasmi
ambayo inawaingizia kipato kwa kujikimu na kuendesha maisha yao ya kila siku.
Kukubali mikataba isiyo na maslahi kwao imekuwa ni sawa na kujimaliza wenyewe.
Ukiwaangalia wasanii wachache wenye maendeleo utagundua
kuwa hawa ni wale wenye kupenda kuingia mikataba ambayo ama wameipitia kwa
umakini au wamepata ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalam wa sheria, na
huingia mkataba hiyo kwa kila kazi wanazofanya na kupewa nakala za mikataba
hiyo.
Jambo la ajabu ni pale wasanii wengi wanapodai
kuwa na mikataba lakini wao wenyewe huwa hawana nakala za mikataba hiyo, kwani kuna
aina ya ujanja ujanja ambao hufanyika ambapo wasanii wengi huambiwa waache
mkataba ili ukasainiwe na mwanasheria na baada ya hapo wengi huwa hawauoni tena
mkataba wao.
Wakati huu wa majonzi ya kuondokewa na gwiji wa
vichekesho wasanii wautumie kutafakari kuhusu mustakabali wa tasnia ya sanaa,
hasa wajifunze kuingia mikataba kwa kila kazi wanazofanya. Ni vizuri zaidi mikataba
hiyo ikapitia mikononi mwa watu wanaoweza kuitafsiri.
No comments:
Post a Comment