Wasanii Nandy na Bill Nass katika clip ya video chafu iliyoenea mtandaoni |
Hamisa Mobeto |
INASHANGAZA sana! Katika kipindi ambacho Sheria za
mitandaoni zimetungwa ili kudhibiti matumizi ya mitandao hiyo, ndipo mdudu
mbaya sana wa video chafu kaingia katika tasnia nzima ya burudani.
Kabla ya huu mtindo mpya wa video zinazodhalilisha
utu tumekuwa tukishuhudia jinsi wasanii wa kike wanavyokuwa nusu watupu kitu
kinachosemwa eti ndiyo maendeleo (kupiga hatua), na pengine inabainishwa kuwa
hiyo ndiyo dalili ya kuwepo kwa mafanikio katika tasnia hii.
Wachambuzi wengi wa burudani wamekuwa wakiandika
makala/uchambuzi kuwaponda wasanii wenye tabia za kupiga picha chafu, lakini
wakasahau kuwa hata vyombo vya habari (wakiwemo wao wenyewe) haviwezi kukwepa
kuwa ni sehemu ya kashfa hizi.
Vyombo vya habari (hasa magazeti pendwa) ndivyo
vimekuwa mstari wa mbele kusambaza, japo vyombo hivyo hivyo kwa njia ya ajabu
sana vimekuwa pia mstari wa mbele kulaani.
Haiwezekani nguvu ya kupita tu ikatusababishia
mabadiliko tunayoyashuhudia sasa kwa kisingizio cha utandawazi au maendeleo.
Kabla ya awamu hii ya Rais John Magufuli nilikuwa
nashuhudia tukiwekea picha za wasanii walio nusu utupu kwenye kurasa za mbele
za magazeti yetu, mtindo ulioanza polepole ukiwa umepambwa na maelezo kuwa hiyo
ilikuwa njia ya kurekibisha tabia, au mara nyingine ulifanywa kwa kisingizio
cha kuonesha jinsi wasanii wetu walivyochanganyikiwa kwa kuiga tamaduni za
Magharibi.
Ilishangaza sana kuona magazeti yanashupalia
kutafuta picha mbalimbali zilizowaonesha wasanii wa kike wakiwa watupu, na
wasanii wengi walijipeleka wenyewe kwenye vyombo vya habari, na kupiga picha
chafu ili kujitengenezea skendo mbaya kwa dhumuni la 'kutoka kisanii'.
Ndiyo maana ilikuwa haishangazi kuona wasanii
walioandikwa vibaya kutolalamika au kuchukua hatua zozote za kisheria. Si hivyo
tu, hata pale wasanii walipohisi umaarufu wao unachuja waliwatafuta waandishi
na kutengeneza skendo kwa kile walichodai ‘kuosha nyota!’
Sasa imeonekana magazeti hayana dili tena, mambo
yote ni mtandao, kwa kuwa tunakwenda na wakati! Au siyo? Hivyo kwa sasa video ndizo
zimekuwa zikitafutwa kwa udi na uvumba na hata wengine kuahidiwa fedha nyingi
kama watafanikiwa kuvujisha video za wenzao.
Hali hii ya kuvujisha video chafu za wasanii wetu
kwenye mitandao na kupatiwa promo kubwa zinawafanya mpaka watoto wadogo kupata
taarifa hizo bila hata kuhangaika.
Kwa sasa imekuwa ni fasheni kwa wasanii wengi wa
nchi hii, maarufu na hata wasiokuwa maarufu, kujitafutia kiki kwa njia ya
skendo ya picha na video chafu kwa kisingizio cha kutafuta ‘promo’.
Mwanzoni mdudu wa skendo na picha chafu alikuwa
ameweka kambi kwenye tasnia ya filamu (Bongo Movie) lakini kwa sasa ameenea
kwenye sekta nzima ya burudani, hii inatokana na dhana mbaya ya ‘biashara ni
matangazo’.
Huu msemo wa ‘biashara ni matangazo’ umekuwa
ukichukuliwa vibaya na ni hatari sana si tu kwa uhai wa maadili katika sanaa,
lakini pia kwa uhai wa maadili katika vyombo vya habari.
Dhana hii imekuwa chachu ya kuchochea sanaa chafu
na inakinzana na tamaduni zetu kwa kisingizio cha utandawazi. Hata hivyo
ieleweke kuwa dhana ya biashara ni matangazo inakubalika katika biashara
zisizohusiana na sanaa, burudani au utamaduni kwa kuwa inapotumika kuhusisha
kazi za sanaa husababisha uchafu huu tunaouona.
Wengi wa wanaojiita mastaa, iwe wa filamu au muziki
waliopata umaarufu kupitia skendo za magazetini au wanaokubali picha zao za
utupu zitumike kwenye mitandao hawaijui thamani ya ustaa wao.
Hata skendo zao za ngono mfululizo tunazoziona
kwenye vyombo vya habari ni ujinga mtupu!
Inashangaza kuona mtu akiimba wimbo mmoja tu au kutokea
kwenye filamu moja au mbili, tena kwa kushirikishwa kwenye sehemu ndogo sana,
ataanza kujiita staa na kujitafutia skendo kwenye magazeti na mitandao ya
kijamii ili asomwe. Ndiyo maana sishangai kuona zinaibuka skendo za aibu kibao!
Sitaki kumumunya maneno, vyombo vya habari
(magazeti, redio na televisheni) na mamlaka zinazosimamia maadili katika vyombo
vya utangazaji kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hawawezi kukwepa
lawama hizi.
Hivi inakuwaje vyombo vya habari kuruhusu video za
wasanii maarufu duniani kurushwa bila hata kuangalia maadili yaliyomo humo
yanaendana vipi na hadhi ya nchi yetu huku tukiwafungia wasanii wa ndani?
Tunawaandaaje watoto wetu kwa kuruhusu kurusha
sanaa chafu za aina hii kwenye vyombo vyetu vinavyoangaliwa na kila rika?
Hali hii kwa sasa inakuwa ngumu hata kwa watoto
kukwepa kupata picha, video na taarifa hizo hata kama tukiamua kuwafungia
ndani, TV itawaletea au mazungumzo mazito ya vipindi vinavyoendelea katika
radio zetu mida ya kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 7 mchana. Bila hata kuwepo na
chembe ya staha hali hii imekuwa kubwa kwa kisingizio kikubwa cha uhuru wa
kutoa habari.
Imefika wakati, tena nadhani tumechelewa kulisema
hili; ni lazima sasa tufungue mdomo na kusema kuwa inatosha. Mamlaka
zinazohusika na udhibiti zisisubiri shinikizo bali wawe macho saa ishirini na
nne kufanya kazi zao kwa weledi.
Watambue kuwa hata nchi ambazo wasanii wetu waiga,
huwa zina staha zake kutokana na mila za huko. Picha hizi za utupu zisiwe
zinapatikana kiholela hivi, kama ni vipindi vya TV basi zichambuliwe na
zihamishiwe vipindi vya usiku wakati watoto wamelala, magazeti yenye picha za
aina hii yatafutiwe njia za kuratibu, ikiwezekana picha hizo zisiwekwe kabisa
ukurasa wa mbele ambapo hata watoto wanaona mara moja.
Pia tuache unafiki wa kuhubiri tusichotenda na
kutenda tusichohubiri, hasa kwa vyombo vya habari ambavyo kila siku
‘vinashadadia’ skendo za wasanii na kutuonesha picha za utupu kwa kisingizio
cha kurekebisha tabia.
Ni mambo ya ajabu: unapigaje picha ya binti akiwa
mtupu usiku wa manane akiwa klabu kisha unaweka katika ukurasa wa mbele wa
gazeti lako asubuhi na kudai eti unamrekebisha mtu tabia? Hapa sioni kama kuna
kurekebishana, bali kiukweli tunasambaza tu yale yaliyokuwa siri usiku na kuyaweka
hadharani hata kwa watoto.
No comments:
Post a Comment