Apr 27, 2018

Muungano wetu na utamaduni wetu


JANA Aprili 26, Tanzania iliadhimisha miaka 54 ya Muungano tangu nchi zilizoitwa Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuzaa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania. Nchi hizi mbili yaani Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja) ziliungana Aprili 26, 1964.

Jahazi linalowabeba Watanzania limeweka historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi.

Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu: Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Tanzania ni nchi, watu wake mmoja mmoja huitwa Mtanzania na kwa ujumla wao wanaitwa Watanzania, hivyo kuunda taifa la Tanzania.


Nchi ya Tanzania kwa mapana na marefu yake imejumuisha watu kutoka makabila tofauti tofauti yasiyopungua 120 yakiwemo makabila makubwa na mengine madogo madogo, ambayo yote hutunza mila na desturi zao kwa kiasi tofautitofauti.

Makabila haya yanatofautiana kwa mambo mengi yanayojikita katika utamaduni na historia ya kabila husika.

Waasisi wa Taifa la Tanzania wakiongozwa na Mwalimu Nyerere na Abeid Aman Karume kwa namna ya pekee sana waliunganisha Watanzania huku wakisisitiza kuweka utaifa kwanza, ilhali kila mmoja akibaki na kabila lake.

Waasisi hawa walifanya haya ili kuibua haja ya kujenga utambulisho na kielelezo cha uhai wa taifa la Tanzania duniani, yaani utamaduni.

Utamaduni ndiyo mfumo wa maisha ya watu jinsi wanavyoishi na maendeleo yao kijamii, kiuchumi, kisiasa n.k. Tanzania ni moja kati ya nchi zinazosifika duniani kwa kulinda maadili yao.

Muungano wa Tanzania ulifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na uhusiano ambao ulishabihiana kama siyo kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar).
Ingawa zipo pia sababu za kijiografia, kisayansi na kihistoria zilizochangia huu muungano wetu, lakini katka makala yangu nitajikita zaidi katika sababu ya kitamaduni.

Kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano mkubwa wa kiutamaduni baina ya Wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilishamiri baina yao hata kabla ya uhuru wa nchi hizi.

Ndiyo maana harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe zilihusisha pande zote katika kushirikiana na zilichangia zaidi kutuunganisha.

Inaaminika (na ndiyo ilivyo) kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza, ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.

Hali kadhalika, Watanganyika wana mchango wao mkubwa sana kwenye mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, ndiyo maana wasioyatakia mema mapinduzi hayo walizusha kwamba Watanganyika walipelekwa Zanzibar kupindua kwa sababu za kikabila/ kitabaka.

Kiutamaduni, licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120, tuna mfanano mkubwa katika utamaduni wetu ikiwemo lugha adhimu ya Kiswahili, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi (ya heshima ambayo kila mtu anapaswa kuvaa na si mavazi yanayovunja maadili ya taifa), ujenzi wa nyumba na tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika).

Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo kikuu cha ndani cha jamii yetu.

Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.

Heshima iliyopo miongoni mwa jamii hii pia imesaidia watu kuwa na maendeleo kwa sababu ya heshima hiyo.

Lakini, wakati tukitimiza miaka 54 ya muungano wetu, jamii ya Kitanzania inaonekana kuanza kupoteza mila na tamaduni zake kila kukicha.

Tanzania ya leo, siyo tu inapuuzia utamaduni wake, bali haitendi mengi yaliyoasisiwa na waanzilishi wa taifa letu, hivyo kuelekea kupoteza historia nzuri ya Tanzania.

Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake.

Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.

Haya yanafanyika huku vyombo vya kuyasimamia vikiwepo na havisemi kitu. Hivi huu Utamaduni ambao kila siku tunauhubiri una picha gani? Hivi viongozi wanaosimamia haya maadili wanajua kweli mila na desturi za jamii zetu?

Kitu kibaya, utakuta Mkurugenzi wa Utamaduni anaomba apigiwe Kwaito katika sherehe ya Kitaifa! Najua tumeshapotea sana baada ya miaka 54 ya muungano wetu, tusisubiri miaka mingine 54 ili kuyarekebisha haya.

Watanzania wote kwa ujumla wetu tuzinduke, maana dunia sasa ipo kwenye vita ya utamaduni na kutawalana kiakili kwa kisingizio cha utandawazi.

Hali ya mtu kujitenga na tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi tuziishizo.

Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu, upendo na kadhalika.

Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inawakumba sana vijana ambao bila kujua huwa wanajikuta katika utamaduni hasi unaowasukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na kukosekana kwa tamaduni.

Hii inajionesha hasa katika sanaa zetu na hasa filamu na muziki wa kizazi kipya, sanaa hizi nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetufanya kukosa kabisa vipaumbele katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.

Sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, jambo hili linaonesha umuhimu wa utamaduni si kitu kilichoibuka tu.

Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.

Sanaa zetu zimesahaulika kabisa, na tumepokea zile ya nje tena kwa fujo, hali hii imesababisha Watanzania kuwa wafuatiliaji na waigaji wa tamaduni za nje badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili sanaa zetu ziende na matakwa ya dunia kwa kuziboresha.

Tunapaswa sasa kwa ujumla wetu tujitambue kuwa sisi ni Watanzania na tunapaswa kuilinda Tanzania yetu na vizazi vyetu kwa kuepuka mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya jamii zetu.

No comments: