Wasanii wa kizazi kipya wanaounda kundi la Tanzania All Stars wakiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara |
UHAKIKA wa sanaa – iwe sanaa yoyote ile – ni
kipaji kutoka kwa Mungu, ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji.
Ijapokuwa kudhihiri kwa sanaa kunatokana na jinsi
sanaa yenyewe itakavyobainishwa, lakini huo si uhakika wote wa sanaa. Kabla ya kubainishwa, kuna hisia na utambuzi na
udiriki wa sanaa yenyewe na kwamba mambo yote yanachimbukia hapo.
Baada ya kuonekana, kutambuliwa na kubainishwa
uzuri, unyofu na uhakika wa sanaa, hapo ndipo zinapoweza kuzuka maelfu na nukta
ndogondogo na nyembamba sana ambazo baadhi ya wakati hawawezi kuziona nukta
hizo isipokuwa wasanii wenyewe.
Mtu asiye msanii anaweza kushindwa kuona hata nukta moja kati ya hizo na sababu yake ni kuwa msanii ana kurunzi na kipaji cha kipekee cha kuweza kupenya ndani kabisa na kuona nukta hizo nyembamba, ndogondogo na uhakika halisi.
Hiyo ndiyo huitwa sanaa ya kweli na ya uhakika
kutokana na kuwa imechimbuka kutoka katika udiriki, ubainifu na utambuzi wa
kweli.
Kabla ya mtu yeyote mwingine, thamani za sanaa na
nafasi yake ya kweli katika jamii inabidi wasanii wenyewe waitambue na kuipa
heshima yake.
Wasanii wanapaswa kujua thamani ya shehena yenye
thamani kubwa iliyomo ndani ya dhati zao. Namna ya kuheshimu na kujua thamani ya kipaji
hicho nayo ni kule kuupa usanii hadhi yake na kuuweka katika nafasi
unayostahiki.
Sanaa ni miongoni mwa nukta za fahari na zenye
thamani kubwa katika moyo wa mwanaadamu.
Sanaa ina lugha pana ambayo hakuna lugha yoyote
nyingine yenye upana kama huo. Si lugha ya sayansi, wala lugha ya kawaida, wala
lugha ya mawaidha yenye upana kama wa lugha ya sanaa.
Inabidi sanaa ipewe umuhimu na kila leo inabidi
ipanuliwe na inabidi pafanyike juhudi za kuhakikisha muundo wa kujivunia wa
sanaa ndiyo unaotumiwa.
Bila ya kuwepo sanaa, matamshi ya kawaida hayawezi
kupata nafasi yake katika akili ya mtu yeyote yule, hasa wakati sanaa inapokuwa
na mvuto na athari za kudumu.
Sanaa ni ala na nyenzo nzuri sana ya kufikisha na
kupanua fikra sahihi. Sanaa ni ala, ni zana ni chombo; naam chombo muhimu mno.
Si sahihi kuipuuza sanaa na kudharau wajibu wa
kuiendeleza, kuikuza na kuipanua sanaa, na si sahihi kudhani kwamba sanaa ni
dhambi au kufikiri ni makosa kuwa msanii na vitu kama hivyo.
Sanaa ni uhakika wenye fahari kubwa na kwa kawaida mtu anayepewa
kipaji hicho na Mungu huwa ni kama ambavyo watu wengine walivyopewa utajiri,
hivyo, anapaswa kujua uzito wa jukumu alilopewa, yaani ajue thamani ya neema
alizopewa na Mungu na atekeleze jukumu lake kwa mujibu wa neema hizo.
Majukumu hayo si lazima yote yawe ni ya wajibu wa kijamii, kidini
au kisheria, hapana, kwani kuna majukumu mengi ambayo mtu anatekeleza kwa
kusukumwa tu na nafsi yake.
Wakati mwanaadamu ana macho, hiyo ni neema ambayo baadhi ya watu
hawanayo.
Lakini pamoja na kwamba macho hayo yanampa mambo mazuri na yana ladha
hizi na zile kwa mwanaadamu, lakini pia mwanaadamu ana majukumu ambayo anapaswa
kuyatekeleza kutokana na kuwa na neema hiyo ya macho.
Hata hivyo, wakati mwingine sanaa inatumiwa vibaya kisiasa. Siasa
katika dunia ya leo inafanya ushakii wa kutumia vibaya sanaa. Kama tutasema
wanasiasa hawafanyi hivyo tutaonekana hatujui yanayoendelea.
Si kuwa wanasiasa wa leo tu ndio wanaotumia vibaya sanaa, bali
wanasiasa wa huko nyuma pia walikuwa wakifanya vivyo hivyo.
Kwa mfano, sekta ya filamu duniani inadhibitiwa na mabeberu,
sinema ni moja ya sanaa za kisasa zilizopiga hatua kubwa kabisa.
Taasisi kubwa kabisa na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza
sinema duniani leo hii ni ile ya Kimarekani ya Hollywood.
Mtu anapojiuliza, Hollywood inawatumikia akina nani, majibu yake
huwa rahisi kuyapata. Ni rahisi kujua Hollywood inatumikia fikra gani na iko
mrengo gani.
Taasisi hiyo kubwa ya sinema na utengenezaji filamu ambayo ina
makumi ya mashirika na makampuni makubwa makubwa ya kutengeneza filamu,
imeajiri wacheza filamu, wasanii, wasimamiaji wa sinema, waandishi na watungaji
mbalimbali na kuwekeza fedha nyingi sana katika upande huo kwa shabaha ya
kutumikia lengo maalumu.
Lengo hilo ni la kufanikisha mambo ya kisiasa za kibeberu za
Magharibi.
Hata hapa nchini, wasanii wamekuwa wakitumika
kisiasa huku hali zao wenyewe katika upande wa maisha yao zikiwa si nzuri sana,
ndiyo maana haishangazi kuona wakijiingiza kwenye biashara haramu kama dawa za
kulevya.
Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya sanaa huwa mara
nyingi wanapokuwa wameshikamana na vitu maalumu wanashindwa hata kurudisha
fedha walizowekeza.
Kwa kweli inabidi kuwasaidia watu hao na kama hawakusaidiwa huamua
kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia fedha za kuweza kuendelezea
kazi zao.
Lililo muhimu kwao wakati huo ni kupata watazamaji wengi zaidi na jambo
hilo si kwamba ni zuri wakati wote.
Kukimbilia kwenye mambo ya kifuska, kueneza fikra za maingiliano
haramu ya kijinsia na mambo kama hayo katika utengenezaji filamu ni jambo
ambalo kwa kiasi fulani linafanyika kwa lengo la kufanikisha fikra hiyo ya
kuvutia watazamaji wengi zaidi.
Lakini msanii hapaswi kumpa kijana kitu ambacho kitamsukuma kwenye
ufuska na ufisadi. Kufanya hivyo kunakwenda kinyume kabisa na fikra ya kumfanya
mtu awe huru kuamua na kuchagua anachotaka.
Masuala ya kuchochea fikra za watu hayampi mtu uhuru wala fursa ya
kufikiri na kuchukua maamuzi anayopenda. Bali humsukuma mtu moja kwa moja
upande maalumu bila ya kuwa na nguvu zozote za kuamua.
Inabidi kazi za kisanii zifanyike kwa sura ambayo msanii ataweza
kuwaonesha watu kazi zake za kisanii bila ya kuchochea hisia wala kufanya jambo
ambalo mtazamaji atalazimika kuvutika upande wake bila ya kuwa na uhuru wa
kuamua.
Kama kazi ya kisanii itamvutia mtu bila ya kutumia vitu kama
hivyo, hapo ndipo mtu atakapoweza kujua kuwa kazi hiyo ya kisanii imefikia
kwenye kiwango bora.
No comments:
Post a Comment