Apr 27, 2018

Sanaa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi


Sanaa za Tanzania
KATIKA ulimwengu wa kimaada unaodhibitiwa na fikra za kupenda dunia, thamani za utamaduni (sanaa ikiwemo ndani yake) huwa hazipewi nafasi na siku zote utajiri wote wa sanaa unapimwa kwa fedha.

Suala muhimu katika ulimwengu huo ni fedha, kwa hivyo kila kitu kinapimwa thamani yake kwa kuangalia kitaingiza kiasi gani cha fedha.

Utaona inatazamwa elimu fulani itaingiza fedha kiasi gani, inaangaliwa kazi fulani ina uwezo wa kuingiza kiasi gani cha fedha na vitu kama hivi. Lakini hali haiko hivyo katika upande wa utamaduni.

Hapana, kwani elimu ni njia ya kuwa na maisha bora, na sanaa ni chombo cha kuwa na ustawi katika maisha.



Mchoraji Lutengano Mwakisopile akichora katika eneo la 
bustani ya kaburi moja, Posta jijini Dar es Salaam

Yaani msanii hata kama watu hawatakuwa wanajua kazi zake za kisanii na hata kama hakutakuwa na mtu yeyote atakayekuwa anatumia usanii wake, lakini bado ana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Inawezekana kwamba katika jamii fulani kutokana na umasikini au ukosefu wa uzoefu watu wasiweze kuonesha uwezo na vipaji vyao vya kisanii au kuwekeza inavyotakiwa katika suala hilo, lakini kuweko wasanii tu katika jamii hiyo ni jambo linalotakiwa kuthaminiwa sana.

Hali hiyo inashuhudiwa katika jamii nyingi duniani. Lakini suala hilo la kukosekana uwekezaji na vitu kama hivyo, halipaswi kufanywa kuwa sababu ya kuzuia kuchemka vipaji vya kielimu na kisanii katika jamii.

Katika baadhi ya nchi, zinatumia sanaa kwa maendeleo, hasa za  maonesho, ili kumuwezesha mwanajamii kujiletea maendeleo yake mwenyewe.

Mbinu ya sanaa kwa maendeleo imejikita zaidi katika kuamini kuwa ikiwa jamii fulani ina matatizo ya kimaendeleo, ni wanajamii wenyewe ndio wana uwezo wa kuyajadili na kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo. 

Ingawa dhana hii siyo ngeni sana masikioni mwa wanajamii na wanaharakati mbalimbali wa maendeleo, lakini haitumiki sana kama kielelezo kuonesha mchango wa sanaa katika kuleta maendeleo ya Watanzania.

Kwa nchi zilizoendelea wanaamini kuwa sanaa ni chombo kinachoweza kuionesha jamii jinsi ilivyo kwani sanaa kwa maendeleo ni zao la jamii yenyewe.

Mara nyingi hutumia fani mbalimbali za sanaa zilizopo katika jamii husika kama vile ngoma, hadithi, maigizo, nyimbo, mashairi, viziga na nyinginezo katika kuamsha ari na kuwawezesha wanajamii kupata fursa ya kujadili na kuhoji mambo mbalimbali, hasa yanayohusu usimamizi wa maliasili ambayo yamekuwa kikwazo cha maendeleo.

Sanaa shirikishi inalenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kujiletea maendeleo.

Pia kama sanaa ikitumika vizuri, inaweza kuwahamasisha wanajamii kuinuka na kuweza kuwawajibisha viongozi wazembe pale wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao.
Hali kadhalika, msanii anapaswa kujua kuwa ana jukumu mbele ya uhakika maalumu. Uhakika huo ni upi?

Suala la msanii kujua yuko katika daraja gani katika upande wa tafakuri ili kwa njia hiyo aweze kuuona na kuutambua ima uhakika wote au sehemu ya uhakika huo, huo ni mjadala mwingine.

Fikra na utambuzi wa kiakili unapokuwa mkubwa ndivyo utakavyomwezesha kutumia vizuri zaidi ule utambuzi wa ndani kabisa wa sanaa na hatimaye kuchangia maendeleo ya nchi yake.

William Shakespeare (gwiji wa fasihi, mashairi na tamthiliya na mwandishi maarufu wa Kiingereza wa karne ya kumi na saba) hakuwa msanii tu, bali katika tungo zake kunashuhudiwa pia mafunzo na maarifa mengi.

Maarifa hayo nayo hayawezi kupatikana kwa kuwa msanii tu, bali misingi inayotakiwa ya kifalsafa na kifikra nayo inahitajika.

Inabidi kuwe na kigezo, kuwe na nukta ya kukimbilia, kuwe na sehemu ya kushikilia yenye fikra kuu na aali ya kuweza kuutia nguvu utambuzi huo wa kisanii ndipo baadaye ubainishaji wa sanaa uweze kupata msukumo na nguvu.

Jambo hilo inabidi lishuhudiwe katika sekta zote za sanaa. Kuanzia sanaa ya usanifu majengo hadi uchoraji na ubunifu na hadi kwenye kazi za sinema, tamthilia, ushairi, muziki na sekta nyingine za sanaa, kote huko kunashuhudiwa maana hiyo.

Baadhi ya wakati mnaweza kuona jengo limejengwa kwa usanii wa hali ya juu, lakini baadhi ya wakati pia mnaweza kuona jengo lisilo na usanii wa aina yoyote ile mkahisi hakuna fikra wala tafakuri yoyote iliyotumika ndani yake.

Wajenzi wa majengo hayo mawili kama watatakiwa kujenga jengo moja, bila ya shaka kila mmoja atakuja na fikra yake. Hivyo kama ujenzi wa mji fulani watapewa watu wawili wenye fikra hizo tofauti, matokeo yake yatakuwa nusu ya mji huo inatofautiana kikamilifu na nusu yake ya pili.

Mwisho, sanaa katika nchi yoyote mara nyingi huambatana na utamaduni wan chi husika.
Bahati mbaya katika nchi za ulimwengu wa tatu, wengi wetu tunadhani ili kuwa wa kisasa na kupata maendeleo lazima tuwe kama nchi za Magharibi na Marekani.

Tunasahau kuwa usasa au kwenda na wakati kama wanavyoita  si kuwa kama nchi za Magharibi. Usasa si kuacha na kuua tamaduni zetu kama Waafrika na Watanzania na kuakisi zile za nchi zilizoendelea ili kujipatia maendeleo.

Sanaa pasipo utamaduni ni moja ya sababu kubwa inayoifanya nchi yoyote kushindwa kupiga hatua ya maendeleo. Tamaduni ndizo zinazofanya nchi kuendelea kusonga mbele kimaendeleo na kuipa utambulisho kama taifa.

Inasikitisha sana! Tunadhani kupata maendeleo ni kuwa kama nchi za Magharibi na Marekani kwa kutupa kila kitu chetu na kuiga vya kwao!

Taifa lisilo na tamaduni imara haliwezi kusonga mbele na ndiyo maana mabepari kwa kutambua hilo wameanzisha vita vya kiutamaduni na wanaua tamaduni zetu kwa kasi wakisema ni mambo yaliyopitwa na wakati.

No comments: