Mwl. Kassim El-Siagi akizungumza na wananchi
waliohudhuria tamasha hilo muda mfupi kabla
tamasha halijaanza
Nikiwa katika picha na wadau wa filamu jijini Tanga,
katikati ni Amri Bawji (mwenye baragashia) na kulia ni
Nassib Ndambwe, mmoja wa waandishi wa script nchini
WIKI iliyopita nilitembelea jiji la Tanga wakati wa tamasha la filamu za Kiswahili zilizotengenezwa mkoani Tanga. Tamasha hilo liliandaliwa na kampuni ya El-Siagi Movies na kudhaminiwa na StarMedia kampuni ya ving'amuzi vya StarTimes, na Nyumbani Hotels & Resorts kupitia vinywaji vyake vya Bavaria. Jiji la Tanga ndilo wanaloishi watu ninaopenda kuwaita “magwiji wa filamu nchini”, kama ambavyo nimewahi kuandika katika makala zangu kadhaa zilizopita.
Kwa nini nawaita watu hawa magwiji wa filamu? Kwa sababu ndiyo watu pekee waliothubutu kuandaa filamu za kibiashara katika miaka ya 1990 japo mazingira yalikuwa magumu sana; wakati huo hakukuwa na mahala pa kuuzia filamu, hata uoneshaji sinema kwenye majumba ya sinema ulikuwa ukisuasua kutokana na kuingia kwa vituo vya televisheni, na sinema zilizotawala nchini zilikuwa za Kihindi.
Ni filamu ya “Shamba Kubwa” (1995) iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim El-Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za kibiashara nchini. Kwa walio wengi pengine watanishangaa kwa kuwa hawajahi kuiona filamu hii kwa kuwa wakati ule ilioneshwa kwenye majumba ya sinema; Majestic Cinema – Tanga, Emipre Cinema – Dar es Saalaam, Metropole Cinema – Arusha, na kadhalika.
‘Shamba Kubwa’ ndiyo filamu iliyowaibua wasanii ambao baadaye wamekuwa mahiri katika ulimwengu wa filamu, kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi, ni filamu hii iliyoteka wengi kwa wakati ule japo teknolojia ilikuwa bado ndogo sana ukilinganisha na hivi sasa.
Filamu hii na nyingine zilizofuata kama ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Mwl. Kassim El-Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji, zote zikitengenezwa na magwiji kutoka Tanga zilitengenezwa katika mfumo wa VHS (analogy), na hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango kidogo, lakini zilivutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa hadithi.
Tanga pia ndiyo mkoa wa kwanza kuanzisha chama ili kukabiliana na changamoto za tasnia ya filamu. Walianzisha Chama cha Watengeneza Filamu wa Tanga (Tanga Film-Makers Association “TAFMA”), wakati huo hata ile filamu ya Girlfriend inayojulikana kwa wengi ilikuwa haijatungwa.