TANGU filamu ya Black Panther itoke, kwa kweli imenifikirisha sana kwa jinsi
ilivyojaribu kuiweka Afrika katika nafasi chanya, ikiionesha Wakanda (Afrika) kuwa nchi bora sana.
Kwa jinsi Wakanda
ilivyoonekana, maana yake ni kuwa kama Afrika isingetawaliwa na wakoloni na kuachwa
kukua yenyewe, ingekuwa mbali sana.
Ukiangalia filamu nyingi za watu weusi, mazingira
ya Afrika yanaonekana kuwa ni mabaya sana na machafu, lakini tofauti katika
filamu hii, nchi ya kufikirika ya Wakanda ina teknolojia za hali ya juu kuliko
hata nchi kubwa za ulaya na Marekani.
Pia inaonesha kukatwa
mawasiliano kati ya Wamarekani weusi na Waafrika wa bara la Afrika.
Ikiwa imetokana na
hadithi ya michoro, Marvel Comic Black Panther, shujaa katika filamu ni
T'Challa (Chadwick Boseman), ambaye anarudi nyumbani kwao baada ya kifo cha
baba yake, Mfalme wa Wakanda.
Anapochukua madaraka
ya kuwa mfalme, T'Challa anakabiliwa na mgogoro unaoelezea uongozi wake na
hatima ya taifa la Afrika.
Akizungukwa na
wanawake katika maisha yake, ikiwa ni pamoja na mama yake (Angela Basset),
mpenzi wake (Lupita Nyong'o), dada (Letitia Wright) na mkuu (Danai Gurira),
T'Challa anapigania kati ya kuwa Mfalme na kurekebisha makosa ya zamani.
Kinachofurahisha mno, filamu hii ina maudhui ya
kiafrika, kwani hata matatizo ya kiutawala ambayo alikuwa anapambana nayo
Tchalla yanaonesha kabisa kuwa ni ya kiutamaduni wa Afrika.
Kwa mfano ili uchaguliwe kuwa mfalme inabidi
upambane na mpiganaji katika kila kabila katika nchi ya Wakanda na ukishinda
ndipo unachaguliwa kuwa mfalme wa nchi hio, utamaduni wa namna hii ulikuwa
unafanyika huko zamani katika nchi za Afrika na kuuweka katika filamu hii
kunaonesha ni jinsi gani filamu ilipania kuakisi utamaduni wa kiafrika.
Katika suala la mavazi (costumes) yaliyotumika, filamu hii imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
sana, ukiangalia mavazi anayovaa mfalme wa Wakanda, pia mavazi wanayovaa watu
waliopo kwenye baraza la serikali ya nchi hiyo ni ya kiafrika.
Kwa ujumla mavazi yana nafasi kubwa sana katika filamu
kuonesha utamaduni fulani au kupeleka aina fulani ya ujumbe kwa hadhira
iliyokusudiwa.
Hivyo, katika filamu hii licha ya kuwa Wakanda ni
nchi iliyoendelea sana kiteknolojia lakini bado inakumbatia asili yake ya kiafrika
katika mavazi na utamaduni wake kiujumla.
Ingawa Black
Panther siyo kwamba ni filamu bora kuliko zote za Marvel la, ila ni filamu yenye upekee sana na huwezi kuifananisha
na filamu kama Thor Ragnarock au Guardians Of The Galaxy 2, ingawa zote
ni nzuri.
Filamu hii ina umuhimu mkubwa kwa jamii ya watu
weusi kwa sababu: ndiyo filamu ya kwanza ya kueleweka ya Superhero mweusi.
Negros wa Marekani hawakuamini macho yao kuona
mhusika mweusi anapewa heshima na thamani kubwa hadi kufikia kutengenezewa filamu
iliyosubiriwa kwa hamu ulimwenguni kote.
Hasa ikizingatiwa kuwa Negros wametoka mbali sana,
toka enzi za mwanamama Rosa Parks kunyimwa kiti katika basi, kisa ni mtu mweusi
hadi zama hizi mwanadada Lupita Nyong’o anapewa uhusika mkubwa katika filamu ya
kampuni kubwa ya wazungu.
Zimekuwepo filamu nyingi za watu weusi kama Superheroes
zilizofanyika huko nyuma, lakini Black Panther inaonekana ndiyo ya kueleweka
zaidi.
Filamu hii itaongeza umoja na mshikimano kati ya
wazungu na jamii ya watu weusi, pia itapunguza ubaguzi kidogo kwa sababu imempa
nafasi mtu mweusi kuwa nyota wa mchezo tofauti na filamu nyingine ambazo watu
weusi wanakuwa kama wasaidizi katika filamu za ki-Superheroes, mfano Falcon ni
msaidizi wa Captain America na War Machine ni msaidizi wa Iron man.
Filamu ya Black Panther inafungua milango kuachiwa
kwa filamu nyingine zinazohusu Superheroes weusi katika ulimwengu wa Marvel.
Ukitoa series ya Empire iliyofanikiwa kuwainua
sana watu weusi katika ulimwengu wa sinema licha ya kukosolewa kukosa maadili
ya kiafrika kutokana na ushoga ulioonekana, filamu ya Black Panther itainua
sana jamii ya watu weusi katika ulimwengu wa sinema, kwa kuwa Marvel wamepania
kuona filamu hii ikifanya vizuri na inasemekana ndiyo filamu yao muhimu sana
kuwahi kufanya tangu waanze kuachia filamu mwaka 2001.
Tayari filamu hii
imevunja rekodi kwenye wiki yake ya kwanza ya uzinduzi ikitajwa
kuingiza kiasi cha dola za Marekani milioni 192 nchini Marekani, ambazo ni
zaidi ya shilingi bilioni 432 za Tanzania.
Kiasi hicho kimevunja rekodi zilizowahi kuwekwa na
filamu kibao kwenye ‘box office’, ikiwemo ile iliyowahi kuwekwa Aprili mwaka
jana na The Fate of the Furious.
Filamu hii pia imeingiza zaidi ya dola milioni 361
kutoka sehemu zingine duniani. Pia imekuwa filamu ya pili kutoka kwenye kampuni
ya Marvel kuwa na ufunguzi mkubwa zaidi ikiongozwa na filamu ya The Avengers ya
mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment