INGAWA Tanzania kuna zaidi ya makabila 120 na
lugha 128 zinazotumika, Watanzania tumeweza kubaki kama tulivyo, Watanzania. Popote pale Mtanzania atakapokwenda atajiita Mtanzania,
akiulizwa zaidi ya hapo, anaweza akataja kabila yake. Ila, Watanzania hupenda
zaidi kuwa Watanzania. Ndiyo utamaduni wetu.
Kinachoonekana sasa ni Watanzania kutaka kugawanyika
kwa misingi ya kidini, hasa kati ya Wakristo na Waislamu, japo wameishi pamoja
vizuri tangu uhuru.
Pamoja na hayo, Sera ya Ujamaa na lugha ya
Kiswahili zimechangia sana kutufanya kuwa wamoja. Rangi, ladha, urafiki na
uchangamfu ndiyo viungo muhimu vya utamaduni wa Tanzania.
Japo yapo mambo mengi yanaweza kutofautiana kutoka
kabila moja hadi jingine, lakini lugha ya Kiswahili, muziki wa asili (ngoma),
sanaa, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi, ujenzi wa nyumba na
tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika), ni mambo
yanayoshabihiana sana.
Hata hivyo, lengo la makala yangu ni kuibua mjadala
zaidi kwa hoja mbalimbali ambazo zimekuwa zikiibuka juu ya suala la maadili
katika kazi za sanaa na namna au changamoto zinazotukabili sote juu ya namna ya
kukuza na hata kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na
maadili yetu ya KiTanzania.
Swali la kujiuliza: Je, njia tunayoenda nayo
katika kazi zetu za sanaa inatusaidia kujenga juu ya msingi sahihi wa
waliotutangulia au tunapotea na wimbi la utandawazi?
Ukweli tatizo la maadili katika sanaa na udhibiti
wa kazi chafu limekuwa gumzo, ingawa kwenye upande wa filamu mamlaka yenye
dhamana imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti tatizo hili.
Kwenye muziki, bado wengi wanajiuliza kwa nini
tunakosa alama ya mfano muziki wetu? Ni nini chanzo cha wanamuziki wetu kuimba
nyimbo zisizo na maadili?
Utafiti na wachambuzi wengi wa masuala ya sanaa huelezea
kuwa fani ya muziki nchini ipo katika hatari kubwa ya kuporomoka kwani
wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika uteuzi wa
maneno katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila,
desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.
Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka
kwa fani hii. Je, kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au
kudhibiti tatizo hili?
Unaweza kujuliza, tunawezaje kuwa na utamaduni wa
muziki mmoja wakati Tanzania kila kabila lina muziki wa asili yake, wenye sauti
tofauti?
Kitu kikubwa ni kwamba ngoma ni kitu cha kipekee
utakachokikuta kwenye muziki wa asili wa karibia makabila yote. Hivyo, muziki
wa kiTanzania kwa ujumla unaongozwa na ngoma.
Kwa miaka dahari tumekuwa na utamaduni fulani, iwe
kwenye furaha au huzuni, nyimbo, kucheza na muziki kwa ujumla imekuwa njia ya Watanzania
kujieleza na kujiburudisha kwa namna moja au nyingine.
Changamoto inayotukabili katika muziki wetu ni
namna ya kuweza kudhibiti muziki wenye mapokeo hasi na usioendana na maadili yetu.
Hali hii imesababisha hivi karibuni Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuzifungia nyimbo kadhaa zisizokuwa na maadili baada
ya kupokea orodha kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Nyimbo hizo zimefungiwa kutokana na kuwa na
maudhui ambayo ni kinyume na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005, ingawa
hatua ya kuzifungia nyimbo hizi imezua maswali mengi sana kuliko majibu.
Ni kweli tumekuwa na idadi lukuki ya waimbaji
bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi, ambao hufanya
kazi zao kuisha kwa muda mfupi.
Si hivyo, tutazidi kuwa wasindikizaji wa kupokea
mitindo ya muziki toka nje na baadaye kulalama kudai ni chetu huku tukiendelea
kutengeneza kazi kwa kunakili, kama hatutakuwa makini katika kuchagua kilicho
bora kwetu.
Sina tatizo na mamlaka zilizofungia nyimbo zisizokuwa
na maadili, lakini tunahitaji kuangalia zaidi ya hapo, kwa kutafuta njia sahihi
zaidi ya kuwasaidia wasanii badala ya kusubiri wakosee ili tukimbilie
kuwafungia.
Kwa nini zisitungwe kanuni (kama si sheria) zitakazofanya
kazi zote zitakazotoka kabla hazijakwenda sokoni zipate ithibati au kwa lugha
nyepesi kibali ili ziweze kusikika na kuonekana.
Pengine kwa kiasi fulani kama si sana tutaweza
kulinda maadili ya sanaa na kudhibiti kazi chafu, pia kukuza viwango vya kazi
zetu za sanaa hapa nchini. Aidha hatua zaidi ziwepo kwamba atakayekaidi maelekezo
haya adhabu kali ichukuliwe dhidi ya msanii yeyote nchini bila kujali umaarufu
wake.
Na hali hii isiangalie muziki na unenguaji tu, pia
fani nyinginezo za sanaa. Baraza la Sanaa la Taifa lisiangalie muziki tu
wakasahau ngoma za asili. Yako wapi mashindano ya taifa ya muziki wa asili
nchini? Ziko wapi tuzo za muziki wa asili Tanzania? Baraza la Sanaa lina mpango
gani kuhusu muziki wa asili?
Nilidhani ili kuendeleza muziki utakaofuata
maadili ingekuwa vyema kuwekeza katika muziki wa asili ili wasanii wa muziki wa
kizazi kipya waache tabia ya kukana nyimbo zao za asili na kuiga muziki wa nchi
nyingine ambao hutokana na nyimbo za asili za nchi zao.
Kuiga huko ndiyo kunaelezwa kusababisha kupoteza
ladha na uhalisia wa muziki wa Tanzania, na hatimaye mamlaka kuzifungia nyimbo
na kuwafungia wasanii ambao tulipaswa kuwalea kimaadili.
Pia Baraza la Sanaa la Taifa liwekeze nguvu katika
fani za uchoraji na uchongaji ambazo kwa kiasi kikubwa bado zinalinda maadili
yake ya mapokeo ya utandawazi na bado tunajivunia Watanzania katika michoro ya Tingatinga
na michoro mingine ya kina mzee Lilanga na mingi inayoelekeza maisha halisi ya
Mtanzania na Mwafrika kwa ujumla.
Wakati sanaa ya kucheza au kuigiza ikiwa inakua
nchini, sanaa ya uchoraji na uchongaji vinyago imeenea. Uchoraji wa Tingatinga
na vinyago vya Wamakonde vinapendwa sana na watalii na wenyeji pia.
Uchongaji ni fani isiyoteteleka kabisa, ona
vinyago vya Wamakonde (lipiku, mashetani) moja ya vinyago maarufu na bora
kabisa duniani, ni fani ambayo haijaingiliwa na sanaa chafu. Hata hivyo, ubunifu zaidi unahitajika katika fani
hizi za kazi za mikono ili ziweze kushindana kitaifa na kimataifa.
No comments:
Post a Comment