Prof Stephen Hawking enzi za uhai wake |
|
NILIWAHI kusoma riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo iliyoandikwa na Profesa Euphrase Kezilahabi,
inayoonesha maisha yaliyopo duniani ni sawasawa na fujo, kwani kila mtu
anayekuja duniani huleta fujo zake na baadaye kutoweka.
Fujo hizo zimekuwa zikitofautiana, wapo waliofanya
fujo kwa jina la amani, waliofanya fujo kwa kutumia nguvu na wengine wamefanya
fujo za kimaandishi, fujo ambazo hazitafutika hadi dunia inafutika…
Nimejikuta nikiikumbuka
riwaya hii baada kutafakari kuhusu maisha ya Prof Stephen
Hawking, mwanafizikia maarufu duniani aliyefariki dunia jana Jumatano Machi 14, 2018 akiwa na miaka 76.
Prof Stephen Hawking ni mmojawapo wa watu waliojaliwa uwezo mkubwa wa akili,
amejulikana sana si kwa sababu ya usanii au umaarufu, bali kwa sababu ya uwezo
mkubwa kiakili na mchango wake katika sayansi.
Prof Hawking alifahamika sana kwa
kazi yake ya kisayansi kuhusu uwepo wa eneo katika anga za juu ambapo nguvu za
mvutano huwa za juu sana kiasi kwamba miali nururishi au hata mwanga hauwezi
kuponyoka.
Kwa Kiingereza, eneo hilo hufahamika kama 'Black
Hole' nadharia aliyoieleza mwaka 1974 ikionesha kwamba 'black hole' hutoa
"Miali ya Hawking".
Alitumia hilo kujaribu kufafanua kuhusu asili ya
vitu vyote duniani na angani na aliandika vitabu kadhaa maarufu vya sayansi
kikiwemo A Brief History of Time (Historia Fupi kuhusu Wakati) mwaka 1988
kilichouza nakala zaidi ya milioni 10.
Prof Hawking alizaliwa Januari 8, 1942
huko Oxford, Uingereza. Alipata nafasi Chuo Kikuu cha Oxford kusomea sayansi ya
mambo asilia mwaka 1959, kabla ya kusomea shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu
cha Cambridge.
Mwaka 1963, Prof Hawking alipatikana
na ugonjwa ulioathiri mfumo wake wa neva na mawasiliano mwilini akiwa na miaka 21. Madaktari walimwambia hangeishi zaidi ya
miaka miwili.
Ugonjwa huo ulimfanya kulemaa na kulazimika
kutumia kiti cha magurudumu.
Nyakati za mwisho za maisha yake, alikuwa hawezi
kuzungumza ila kwa kutumia kifaa cha kufasiri mawazo yake na kuyageuza kuwa
sauti.
Kutokana na umuhimu wake, maisha yake yameigizwa
kwenye filamu ya The Theory of
Everything ya mwaka 2014, ambapo Eddie Redmayne aliigiza nafasi ya
mwanasayansi huyo.
Filamu hii
imetengenezwa kwa hadithi ya maisha yake kushangaza.
Filamu hii ya The Theory of Everything
(Nadharia ya Kila kitu)
iliyoandikwa na Anthony
McCarten na kuongozwa na James
Marsh, imejaribu kuyachora maisha
ya mwanafizikia huyu mwenye kipaji cha hali ya juu na mwanafizikia wa wakati
wetu.
Filamu hii imepata
maoni mazuri, imesifiwa kwa muziki, upigaji picha, na uigizaji wa Felicity
Jones na hasa Eddie Redmayne, kiasi cha kutajwa kwenye tuzo mbalimbali na matamasha
ya filamu, pamoja na kushinda Tuzo za Oscar kama Muigizaji Bora wa Kiume.
Filamu hii pia iliteuliwa
kwenye Tuzo za Oscar kwenye vipengele vya Sinema Bora, Muigizaji Bora wa Kike (Felicity
Jones), Skripti Bora iliyotokana na kitabu, na Muziki Bora (Jóhannsson).
Filamu hii pia iliteuliwa
kwenye maeneo kumi katika Tuzo za British Academy Film (BAFTA); na ilishinda Tuzo
ya Filamu Bora ya Uingereza, Mwigizaji Bora wa Kiume (Eddie Redmayne), na Skripti
Bora iliyotokana na kitabu (Anthony McCarten).
Iliteuliwa pia kuwania
tuzo nne za Golden Globe, ikashinda Tuzo ya Mwigizaji Bora (Eddie Redmayne), na
na Skripti Bora iliyotokana na kitabu (Anthony McCarten).
Pia iliteuliwa kuwania
tuzo tatu katika Tuzo za Chama cha Waigizaji wa Televisheni; ikashinda tuzo
moja ya Mwigizaji Bora wa Kiume (Eddie Redmayne).
Filamu hii imeonesha maisha ya Stephen Hawking alivyojikuta akimpenda Jane Wilde, aliyekuwa mwanafunzi
wa sanaa wakati wakisoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge miaka ya 1960.
Jane Wilde alipenda
sana kumwita Stephen Hawking mrithi wa Albert Einstein, na baadaye mume na baba wa
watoto wao watatu.
Kwa muhtasari, filamu
hii imeigizwa vizuri mno, picha zake zimepigwa vizuri na ukichanganya na muziki
wa Jóhannsson, inakufanya kujikuta ukiwa sehemu ya hadithi.
No comments:
Post a Comment