Kampuni hii inafahamika kwa filamu za The Karate
Kid, Ghostbusters, Spider-Man, Men in Black, Underworld, Robert Langdon, The
Smurfs, Sniper
na nyingine nyingi. Niliwasiliana
na Sony Pictures nikiwaomba watafute njia ya kudhibiti filamu za Hollywood
zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika Mashariki.
Walichonijibu Sony Pictures ni kwamba, hawajali kuona filamu zao zikisambaa, maana walikwishapata faida maradufu kupitia box office, na kusambaa kwake kunasaidia kuwatangaza zaidi!
Hapo
ndiyo shaka yangu ilipoanzia, maana pia nilikuwa na sababu ya msingi kutaka
kunusuru soko la filamu zetu kwa kuwa filamu za nje hazilipi kodi huku wasanii
wetu wasio na mitaji wala dhamana katika benki wakibanwa kulipa kodi bila
uhakika wa soko lao.
Ukiangalia
kwenye stesheni zetu za televisheni kumejaa tamthilia kutoka China, Ufilipino, Mexico,
India
na Korea, ambazo zinaruka karibu kila kituo na tunashuhudia hata matangazo
yakinakshiwa na miziki kutoka nje.
Hivi sasa vipindi kutoka nje, filamu, picha za
katuni na maonesho ya mambo mbalimbali vimetawala nchini na watu wametekwa
kuangalia vipindi hivyo.
Na katika mkumbo huo, wasambazaji wakubwa wa
filamu nchini wameachana na sinema zetu na badala yake wanasambaza filamu
kutoka Bollywood zenye tafsiri za Kiswahili.
Kuna
wakati niliongea na watu wa kituo cha utamaduni cha Ufaransa (Alliance
Française) wakasema
kuwa filamu ndiyo chombo kikuu kilichoisaidia Ufaransa kutangaza utamaduni wao
duniani.
Pia kwa miaka mingi Ufaransa imefanikiwa sana
kuitumia sekta ya televisheni na filamu kutangaza utamaduni wao duniani.
Ufaransa imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa bajeti za
kutengenezea filamu na vipindi vya televisheni kwa nchi zinazoongea Kifaransa.
Kama hiyo haitoshi, wamepanua wigo na sasa wanatoa pesa hata kwa nchi zingine
kama Tanzania.
Ndiyo maana, yeyote atakayeandika script yake ya
filamu au kipindi cha televisheni na kuitafsiri kwa Kifaransa, atapewa udhamini
wa maelfu ya Euro na ubalozi wa Ufaransa ili atengeneze.
Unaweza ukashangaa, kwa nini wanatoa udhamini kwa
watengeneza filamu katika nchi zetu? Nadhani unaanza kupata picha kuwa sasa
dunia imeingia kwenye vita
ya utamaduni, ya kutawalana kiakili.
Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha
katika mazingira yake. Hiyo inajumlisha ujuzi, imani, sanaa, maadili, sheria, desturi
n.k. ambavyo mtu anajipatia kama mwanajamii.
Kama sifa maalumu ya binadamu, inayomtofautisha na
wanyama, utamaduni ni suala la msingi, ukihusisha yale yote yanayopokezwa katika
jamii fulani, kama vile lugha.
Tunasahau kuwa sekta ya televisheni na sinema ni
chombo muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi
husika.
Ndiyo maana nchi za China, Korea au India
zinaingia gharama kubwa za kutafsiri filamu na tamthilia zao kwa Kiswahili
kisha kuzitoa zioneshwe bure katika vituo vyetu vya televisheni.
Kwa mfano, China kupitia Idhaa ya kiswahili ya
CRI, ilifanya kazi ya kutafsiri tamthilia ya ‘Doudou na Mama Wakwe zake’ na
kutia sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthilia hii kwa zaidi ya
miezi 10, kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na Afrika ya mashariki.
Watazamaji wanavutiwa na vipindi vya nje kwa
sababu vipindi vyetu havivutii na havina ubora unaokubalika kimataifa, vituo
vya televisheni nchini vimechukulia hili kama fursa ya kuonesha vipindi
vilivyotafsiriwa kutoka China, Korea na India kwa kuwa wanavipata bure (au
kulipia pesa kiduchu).
Hivi
hatujiulizi: kwa nini nchi za China na Korea wanaingia gharama kubwa za
kutafsiri tamthilia zao kwa Kiswahili na kuzitoa zioneshwe bure kwenye
televisheni zetu?
Kwa
nini Sony Pictures au nchi ya Marekani hawataki kudhibiti filamu za Hollywood
zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika?
Au
hatujiulizi kwa nini India nao wameruhusu filamu zao zitafsiriwe Kiswahili na kuuzwa
kwenye nchi zetu? Ni kwa sababu hii ni vita ya utamaduni, ya kutawalana kiakili.
Hivi tunaandaa taifa (kizazi) la aina gani? Kwa
mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani wa utamaduni? Tuamke, huu
ni mkakati maalumu wa kujenga jamii itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza
tamaduni za nje, na hivyo kutawaliwa kiakili.
Nadhani
tunajenga jamii ya watu waliochanganyikiwa. Hatulioni sasa ila ni uhakika lina
madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu.
Tunaona
vichupi vya vijana wetu kwenye video za miziki zinazooneshwa kwenye vituo vyetu
vya televisheni, utazuiaje hizo wakati vituo hivyo vinarusha video za nje zenye
vichupi?
Ukiangalia
kwa makini, hata mfumo wa utangazaji katika baadhi ya vituo vya Redio na
Televisheni umeigwa kutoka Magharibi, kitu kinachotoa taswira ya kuua suala la ubunifu
na kubaki watupu tusio na kitu chochote.
Bahati
mbaya sana katika dunia hii ya vita ya utamaduni, ukitaka kupata fedha nyingi
kwa urahisi basi fanya jambo linalodhalilisha utamaduni wako au taifa lako au
fanya jambo linalotukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi.
Kwa
sasa, katika tasnia ya muziki na filamu, Watanzania tumebakiwa na kitu kimoja
tu tunachoweza kujivunia kwamba ni chetu: lugha ya Kiswahili.
Lakini
bahati mbaya ni kwamba lugha hii hata hivyo wasanii wetu hawaijui vyema, ndiyo
maana si ajabu kukuta wakichanganya R na L, DHA na ZA n.k.
No comments:
Post a Comment