Filamu ya Gifted Hands |
Lakini wote hawa wanahitaji kuzitimiza ndoto zao; ila
katika safari ya kutimiza ndoto hizi kuna vikwazo na mambo mbalimbali ambayo
huwazuia watu wasiziishi ndoto zao na kuishia kulaumu na kulalamika, hasa
uzeeni.
Wewe je, una ndoto? Je, ndoto yako ni ya namna gani? Je, umewahi kujiuliza kwamba ufanye nini uweze kuitimiza ndoto yako?
Kimsingi, kila mmoja ana ndoto fulani katika maisha yake ambayo anataka itimie, lakini inawezekana kabisa hajui ni kwa jinsi gani hiyo ndoto inaweza ikatimia, au hajui nini cha kufanya wakati huu.
Inawezekana ukawa una ndoto zaidi ya moja na hujui cha kufanya. Lakini ni lazima ujue kwamba ili ndoto itimie kwa namna yoyote ile inahitaji jambo moja la msingi nalo ni ‘muda’.
Muda ni msingi mkubwa sana wa kutimiliza ndoto zako, ni sawa na kusema huwezi kutimiza ndoto yoyote ile pasipo kuwa na muda.
Muda unahitajika sana, kwa maana ukikosa muda huwezi kutimiza ndoto; mfano, chukulia mwenye ndoto fulani amekosa muda ghafla akafa, Je, ndoto yake itatimiaje naye hakuwa na muda tena wa kuishi?
Lakini jambo jingine kubwa ni kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa, ambao walifanikiwa kuziishi ndoto zao.
Ipo haja kubwa ya kujifunza kupitia watu waliofanikiwa ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kupitia mafanikio yao kuna mambo mengi ya msingi tunakuwa tunajifunza na kuachana na makosa ambayo wao waliyafanya pasipo kujua.
Mafanikio ya watu mbalimbali waliofanikiwa hayakuja hivi hivi tu, bali walipitia vikwazo hivi na vile hadi kufanikiwa, ndiyo maana inasemwa kuwa ‘dunia uwanja wa fujo’. Hii maana yake ni kuwa, maisha yaliyopo duniani ni sawasawa na fujo, kwani kila mtu anayekuja duniani huleta fujo zake na baadaye kutoweka.
Mmoja wa watu waliovuka milima na mabonde katika maisha na hatimaye kufanikiwa ni pamoja na Benjamin Solomon Carson Sr., daktari na mtaalamu wa Nyurolojia nchini Marekani.
Ben Carson |
Benjamin Solomon Carson Sr., ambaye anafahamika
zaidi kama Ben Carson, pia ni mwandishi wa vitabu, akiwa ameandika vitabu vya Take
The Risk; The Big Picture; Think Big na Gifted Hands: The Ben Carson Story.
Kitabu cha Gifted Hands (Mikono Yenye Vipawa),
kinaelezea hadithi ya kweli inayohusu maisha ya mtaalamu huyu wa Nyurolojia.
Si nia yangu kukielezea kitabu hiki, bali filamu
ya Gifted Hands inayotokana na hadithi ya kitabu hiki, inayoelezea historia ya Carson
kuanzia alivyokuwa mtoto katika eneo la Detroit hadi wakati akiwa mkurugenzi wa
idara ya watoto ya Nyurolojia katika Hospitali ya Johns Hopkins akiwa na umri
wa miaka 33.
Gifted Hands ni filamu ya mwaka wa 2009
iliyoandaliwa na Thomas Carter na kuigizwa na Cuba Gooding Jr na Kimberly
Elise. Inazingatia hadithi ya maisha ya daktari huyo maarufu
wa upasuaji, Ben Carson, kati ya miaka ya 1961 na 1987.
Filamu yenyewe imeandaliwa na Johnson na Johnson Spotlight
Presentation na ilioneshwa kwenye stesheni ya TNT Jumamosi ya Februari 7, 2009.
Jina la filamu hii lilikuwa limetumika hapo awali
1992 kwa filamu fupi kuhusu Ben Carson iliyotolewa na Zondervan, ingawa filamu
hizi ni tofauti.
Ben Carson (Cuba Gooding) anaanza maisha akiwa
katika hali ya taabu nyingi: yeye akiwa mtoto wa asili ya Kiafrika huko
Marekani, hana baba na masomo yamemshinda shuleni.
Inaanza akiwa akila vyakula kama vibanzi akitazama
runinga na anahitaji miwani. Mama yake aliyeacha shule akiwa daraja la tatu,
anaanza kufanya maamuzi kwa ajili yake kwa kuwa anaona mwenendo wa Ben ni
mbovu.
Watoto wake wawili, Ben na Curtis, walipohitaji
kujua hesabu ya kuzidisha aliwafanya waape kuwa watasoma yeye akiwa ameenda kwenye
uchunguzi katika taasisi ya waliorukwa na akili.
Mama yao anapoona kizuizi cha ufanisi wa watoto
wake ni runinga anawaagiza wasome vitabu viwili kila wiki kutoka maktaba na
kuandika ripoti kuvihusu. Anawapeleka pia kwenye shule bora zaidi.
Wakati huo huo, Ben anaanza kunawiri kimaisha na kiakili.
Kwa kipindi hiki Ben anapata miwani aliyohitaji, na anajifunza hesabu ya
kuzidisha. Ben anaanza kutafiti ulimwengu wa vitabu, na
anaendelea kukua ndani yake. Anaanza pia kuwa na hasira nyingi, hasira hii ingemharibia
utoto wake kama isingekuwa muujiza uliomfanyikia.
Baada ya kukaribia kumwua mtu kwa ghadhabu zake,
anagundua kuwa amekuwa mateka wa hasira hizo na anahitaji kufanya marekebisho
haraka. Anakwenda chumbani mwake na kumlilia Mungu na
kuomba kwamba anaweza kumkomboa kutoka kwenye tatizo la hasira.
Katika mtihani anaongoza shuleni katika darasa
lake la nane na anaendelea kufaulu hadi kuwa nambari tatu akiwa shule ya sekondari. Kwa jitihada na njaa ya ufanisi, anapata udhamini
unaomwezesha kwenda chuo kikuu. Anapita mtihani wa somo la udaktari na hiyo
inamwezesha kuenda Chuo kinachofundisha madaktari na wauguzi.
Carson anapata maisha magumu akiishi na madaktari
na wanafunzi wenzake akifanya kazi katika Hospitali ya Johns Hopkins. Akiwa
huku ndiko anakofanya upasuaji kama bila kusimamiwa na msimamizi akihatarisha
kazi yake ya udaktari ili kuokoa maisha ya mgonjwa.
Kwa mafanikio hayo, Ben Carson anaigizwa (na Cuba
Gooding) kama daktari wa upasuaji mwenye kipaji katika filamu hii ya Gifted
Hands (yaani Mikono Yenye Vipawa).
Ilivyopokewa
Ilipotoka, wakosoaji wa filamu wakaipa filamu hii
jumla ya kitaalamu ya alama 63/100 katika tovuti ya Metacritic.com. Huku
ikisemwa kuwa, filamu hii ni bora kwa nchi iliyopewa changamoto na rais wake
mpya kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment