Mar 7, 2018

Filamu ya The Silent Child: Somo kubwa kwa tunaodhani ‘hawawezi’




MARA nyingi nimewashauri wasanii wa Tanzania kutengeneza filamu fupi, kwani soko lake limejengwa katika misingi imara, haliangalii majina ya watu bali misingi na weledi.

Soko kubwa la filamu hizi lipo kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa, kwani matamasha ya filamu ni sehemu nzuri zaidi ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa.

Naam… sanaa ya filamu ni kitu cha ajabu sana. Si kila mtu anaweza kuipenda kazi yako. Ila unachotakiwa ni kusimamia ndoto yako pasipo kukata tamaa. Hasa ukiwa na script nzuri na mipango sahihi.

Kama utatumia muda vizuri kuisuka script yako kwa kufuata misingi, utengenezaji wa filamu fupi unaweza kuwa rahisi na kwenda vizuri zaidi.

Wiki hii kulikuwa na Tuzo ya Oscar katika kitengo cha Filamu Fupi kuhusu Matukio Halisi, na filamu ya The Silent Child.


Filamu hii ilikuwa inashindana na filamu za Watu Wote iliyowashirikisha Wakenya ikihusu shambulio ambapo watu 2 waliuawa ndani ya basi eneo la Mandera mwaka 2015, Dekalb Elementary; The Eleven O'Clock na My Nephew Emmett.

The Silent Child ni filamu fupi ya Uingereza iliyoandikwa na kuigizwa na Rachel Shenton na kuongozwa na Chris Overton, ambaye ni mchumba wa Rachel. Filamu hii imetolewa mwaka 2017 na kampuni ya Slick Films.

Ni hadithi ya Libby, msichana kiziwi mwenye miaka minne ambaye ana tatizo la kusikia, ndiye mdogo zaidi katika familia yake. Anaishi na mama Sue (Rachel Fielding), baba Paul (Philip York) na ndugu zake wakubwa.

Filamu hii imeigizwa na Maisie Sly (Libby), binti wa miaka sita, ambaye pia ana tatizo la kusikia.

Libby anaishi maisha ya upweke hadi pale mfanyakazi wa ustawi wa jamii, Joanne (Rachel Shenton) anapoanza kutembelea nyumbani kwao na kumfundisha lugha ya ishara, mara ulimwengu mpya wa furaha unamfungukia.

Ingawa somo kubwa la filamu hii ni uziwi, Shelton na Overton wanatutaka tuone nini kinachoweza kutokea kwa kijana anayeonekana kama 'asiyeweza' na wale walio karibu naye kwa sababu hawezi kuwasiliana nao sawasawa.

Overton anatumia lugha ya ishara vizuri, kuonesha jinsi inavyotoa uhuru halisi wa kujieleza kwa Libby. Katika mojawapo ya nyakati bora zaidi kwenye filamu, tunamuona Libby katika chumba na viziwi wengine anapogundua ghafla kuwa anajua anaweza kuelewa nini wanasema.

Filamu hii imetokana na uzoefu wa Shenton mwenyewe kama mtoto wa mzazi kiziwi. Lugha ya Ishara ya Uingereza ndiyo iliyotumiwa katika filamu hii.

Wakati akitoa hotuba yake baada ya filamu hii kushinda Tuzo ya Oscar, Rachel Shenton alitoa hotuba yake ya kupokea tuzo kwa lugha ya ishara ambapo alisema:

"Nilitoa ahadi hii kwa mwigizaji wetu nyota ambaye ana miaka sita kwamba ningetoa hotuba hii kwa lugha ya ishara. Mikono yangu inatetemeka, kwa hivyo naomba radhi…

"Filamu yetu inahusu mtoto asiyeweza kusikia ambaye anazaliwa katika ulimwengu wa kimya. Si filamu iliyoongezwa chumvi, haya ni mambo ambayo yanawatendekea mamilioni ya watoto kote duniani ambao huishi katika kimya na kukumbana na matatizo katika kuwasiliana na hasa katika kupata elimu."

Shenton ni mmoja tu miongoni mwa waigizaji wachache wa kike kuwahi kutoa hotuba kwa lugha ya ishara. Jane Fonda alitoa sehemu ya hotuba yake ya ushindi kwa lugha ya ishara kwa filamu yake ya Coming Home mwaka 1979.

Louise Fletcher pia alitoa hotuba kwa lugha ya ishara kwa sababu ya wazazi wake wasioweza kusikia aliposhinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike kwa filamu yake ya One Flew Over The Cuckoo's Nest miaka mitatu awali.

Marlee Matlin, ambaye ana matatizo ya kusikia, pia alitoa hotuba kwa lugha ya ishara baada ya kushinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike kwa filamu yake ya Children Of A Lesser God mwaka 1987.

No comments: