Kikundi cha Sanaa cha TaSUBa wakifanya vitu jukwaani |
DAH! Ama kweli siku hazigandi na maisha hayarudi
nyuma! Maisha yakipita yamepita, japo historia ndiyo inayoweza kuturudisha
nyuma tupendavyo. Enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na baadaye Ali Hassan Mwinyi kulikuwa na vikundi vingi vya sanaa, hasa
vya sarakasi, maigizo, ngoma, mazingaombwe na kadhalika.
Vikundi hivi vilitoa burudani ya aina yake katika
jamii husika, na watu walikuwa wakienda kwenye kumbi mbalimbali, hasa jijini Dar
es Salaam na miji mikubwa mwisho wa wiki kupata burudani ya aina yake.
Nakumbuka kulikuwa na vikundi vya sanaa vya DDC
Kibisa, Muungano Culture Troup, Makutano Dancing Troup, Ujamaa Ngoma Troup, Mandela
Theatre, Bima Modern Taarab, Super Fanaka, Reli Kiboko Yao, JWTZ, Tancut Almasi,
UDA, Urafiki n.k.
Pamoja na kutumbuiza kwenye kumbi mbalimbali, vipo
vilivyokonga nyoyo kwa burudani na vichekesho vya papo kwa papo jukwaani na
maigizo yaliyorushwa kwenye kituo pekee cha redio cha wakati huo, Radio
Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Nakumbuka tukiwa wadogo tulizoea kusikiliza
vipindi vya Mahoka au Pwagu na Pwaguzi vikirushwa na RTD, bila kusahau vipindi
vya Twende na Wakati, Mzee Jangala n.k.
Kwa kweli hawa jamaa walikuwa vinara wa burudani
kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu bila
kuwaona.
Pamoja na kutoa burudani murua vikundi hivi
vilijenga uzalendo kwa vijana wa wakati ule. Hakika uzalendo kwa wakati huo
ulikuwa juu, ila kwa sasa tunashuhudia anguko kubwa linalosababisha janga kubwa
kwa Taifa.
Kwa kipindi kirefu tumekosa vionjo vya sanaa
kutoka kwa vikundi kama hivyo... vikundi vingi kwa sasa ni vya kwenye runinga
na si ukumbini ama stejini.
Watu wengi siku hizi wamekuwa wanaanzisha vikundi
vya sanaa pasipo kuwa na malengo, wanakaa kutegemea runinga zirushe kazi zao,
jambo linalowafanya wasanii kuhama vikundi mara kwa mara kila wanapoona hakuna
uhakika wa kuonekana kwenye runinga.
Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa linasajili
vikundi vya sanaa kila kukicha lakini vikundi vingi vinakufa kwa muda mfupi
pasipo kutimiza malengo waliyojiwekea kutokana na kukosa maono.
Kutokana na kukosa maono, imewapenyeza wenzetu Wachina
na wa Mataifa ya Magharibi kwa kasi kubwa na sasa wamejizatiti katika kutangaza
utamaduni wao. Kwa mfano, Wachina wana vikundi vingi vya sanaa na
ndivyo vinawachangamsha wao.
Laiti tungejua umuhimu wa vikundi
hivi, tungerudisha misingi ya utamaduni na sanaa (hili nitaliongelea vizuri
siku nyingine), kwani wanasayansi wamekadiria kwamba kufurahi humuongezea mtu
afya bora na maisha marefu.
Yapo manufaa mengi ya kufurahi ikiwa
ni pamoja na kuongezeka mara tatu kwa kiasi cha hewa kinachovutwa ndani ya
mapafu na vile vile kuboreshwa kwa mzunguko wa damu, umeng'enyaji na uyeyushwaji
wa chakula, utendaji wa ubongo na kuondolewa kwa vitu vyenye kudhuru.
Hata baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni
miaka ya 1990, tulikuwa na vikundi vya sanaa vya kina Mzee Small, Mzee Majuto
na kina Onyango na wenzake vilivyotuburudisha sana.
Mara wakaibuka Max na Zembwela na 'Mizengwe' yao
na kutoa burudani kulingana na wakati. Kisha ikawa zamu ya Ze Comedy (EATV) ya kina Masanja, Joti, Mpoki na wenzao, kuuteka
umma wa Watanzania kwa burudani ya aina yao.
Nchini Kenya bado wana utamaduni wa vikundi vya
sanaa kuburudisha katika kumbi mbalimbali kila mwisho wa wiki.
Mchekeshaji maarufu wa Kenya, Daniel Ndambuki "Churchill" |
Kwa mfano mchekeshaji Daniel Ndambuki, maarufu
kama Churchill, huandaa vipindi vya runinga kama Churchill Show ambavyo kabla
ya kurushwa kwenye runinga, ucheshi wa papo kwa papo jukwaani hufanyika kwenye
ukumbi wa Carnivore jijini Nairobi.
Churchill Show imekusanya wachekeshaji wakongwe na
wachanga, kwa ucheshi wa papo kwa papo jukwaani (stand-up comedy).
Aina hii ya ucheshi Wakenya wamefanikiwa sana, tofauti na Tanzania.
Daniel Ndambuki kabla hajaanzisha Churchill Show alikuwa
katika kundi la Ridiculous lililojulikana zaidi kama “Red Corna”, ambalo kundi
la Ze Comedy waliiga ucheshi wa papo kwa papo lakini wakashindwa kabla
hawajarukia kuigiza taarifa ya habari ambayo pia waliiga kutoka Red Corna ya
Kenya.
Niliwahi kushuhudia jinsi Ze Comedy walivyokuwa
wanahangaika kuchekesha papo kwa papo pale kwenye ukumbi wa Starlight!
Aina hii ya ucheshi wa papo kwa papo inahitaji
uelewa mkubwa sana wa jambo unalotaka kuliigiza ili lichekeshe, kwani
kichekesho kinategemeana sana na tukio la papo kwa papo au lililotokea!
Hii ni kwa sababu sisi Waafrika kwa sehemu kubwa
hutumia ishara, mifano katika hadithi na matukio ya kuchekesha. Ucheshi kwa
kawaida huwa na mwisho wenye kufurahisha, ingawa wakati mwingine unaweza
kuegemea mambo yanayosisimua au mabaya.
Tanzania tunao wasanii wazuri lakini wamekosa
mwongozo mzuri wa kuwafanikishia kazi zao.
Wasanii wetu wanatakiwa kuongeza wigo wa ubunifu
na kujifunza zaidi kama wanataka kuendelea kutusisimua, aidha wanapaswa
kufuatilia sanaa za wenzetu ikiwa ni pamoja na kununua kazi hizo,
wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu,
wazame ndani ya akili za watazamaji wao kujua mahitaji yao na wasome alama za
nyakati.
Kila jamii ina utamaduni wa kipekee sana wa
kuchekesha. Bahati mbaya Watanzania tumeathiriwa na mifano ya nje.
Vijana wa Tanzania wameshindwa kuelewa kwamba
tunatazama vipindi vya nje kwa ajili ya kuangalia wenzetu wanafanyaje kazi zao
lakini si kuiga, kwani si mwalimu mzuri kwetu.
Ndiyo maana natamani sana enzi za vikundi vya sanaa
vya DDC Kibisa, Muungano, Makutano, Ujamaa, Mandela, Bima, Super Fanaka, na
kadhalika zirudi.
No comments:
Post a Comment