JUZI nilipata nafasi ya kujadili jambo na
Mpigapicha mkuu wa gazeti la HabariLeo, Fadhili Akida, ambaye alionesha nia ya
kutaka kutengeneza filamu fupi, ingawa hakujua soko lake likoje.
Tulijikuta tukiwa katika mazungumzo hayo baada ya
mchambuzi maarufu wa filamu nchini, ambaye pia ni mhariri wa uzalishaji wa
gazeti la HabariLeo, Beda Msimbe, kuibua hoja kuhusu filamu fupi.
Wakati nikiongea na Fadhili, nilijaribu kumweleza
uzoefu wangu kuhusu tasnia ya filamu na kile ninachojua kuhusu sekta hii na
soko la filamu fupi. Ni mara nyingi nimekuwa nikiwashauri wasanii wetu
kuligeukia soko la filamu fupi, kwani soko hili limejengwa katika misingi
imara, kwani haliangalii majina ya watu bali misingi na weledi.
Soko kubwa la filamu hizi lipo kwenye matamasha ya
filamu ya kimataifa, ambako ukipeleka filamu yako inaweza kupata watazamaji
tofauti ambao si marafiki au jama watakaoiona filamu hiyo.
Matamasha ya filamu ni sehemu nzuri zaidi kwa
ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa. Pia ikitokea ukabahatika kuwa mmoja wa washindi wa
tuzo katika tamasha la filamu, jua itakuwa rahisi kwako kuaminiwa, na hivyo kupata
udhamini wa kutengeneza kitu kikubwa zaidi.
Pia utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa,
na hapo ndiyo utakapojua kuwa upo katika mstari sahihi.
Soko la filamu fupi si la ubabaishaji kama hili tulilolizoea,
kwani ukitengeneza kazi nzuri ujue itapata soko tu. Kuna matamasha zaidi ya elfu tano katika sehemu
mbalimbali duniani, na idadi huongezeka kila mwaka. Matamasha haya yana
taratibu zake, yapo ambayo huhitaji kutoa ada ya kiingilio na mengine hutoza
malipo ya ada ya kuingia, chochote kuanzia dola 10/ na 50/.
Ni vyema kwa wasanii wa Tanzania kufikiria soko
hili hasa ikizingatiwa kuwa, thamani ya filamu zetu imeshuka sana, hii
inatokana na wasambazaji wa filamu waliolihodhi soko hili kutozingatia weledi
wala misingi na hivyo kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizo na ubora.
Soko la filamu nchini (Bongo Movies) limejikita
katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism), kitu ambacho ni
hatari, na hata muundo wa soko hili umeshusha hadhi ya utamaduni.
Umuhimu wa sinema fupi unaonekana sasa hasa
kutokana na ile dhana ya filamu kusemwa kuwa hazifanyi vizuri sokoni kinyume na
ukweli ulivyo, kwani tatizo ni kutokuwepo uwazi katika biashara kati ya
mtayarishaji wa filamu na msambazaji.
Soko la filamu nchini ni kama yalivyo masoko
mengine, hutegemea sana taarifa iliyo sahihi. Ili masoko yaweze kuwa katika
ushindani mzuri, wadau wote sokoni wanapaswa kuwa wamepata taarifa sahihi
kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba kutokana na matendo yao.
Ikiwa baadhi watakuwa na taarifa sahihi zaidi
kuliko wengine, hizo tofauti zitasababisha kuwepo na matokeo mabaya.
Kuna matatizo mengi katika soko la filamu nchini,
ugumu na makosa yanayofanya utengenezaji wa filamu kuwa wa gharama kubwa zaidi
na kutumia muda mwingi kuliko inavyotakiwa, huku mtengenezaji akiwa hajui
atakachopata.
Pia kadiri mtandao wa intaneti unavyoendelea kwa
kasi duniani, filamu fupi za dakika kadhaa ambazo huoneshwa kwenye mtandao
zimeanza kushamiri sana duniani. Kuna wakati utakuta filamu fupi baada ya kuwekwa
kwenye mtandao wa intaneti, inaangaliwa na watu zaidi ya mara milioni moja. Na
kila inapoangalia huingiza pesa.
Kwa vijana wengine wanaopenda kutengeneza filamu
fupi imewapa fursa ya kutimiza ndoto yao, kwa kuwa gharama ya filamu za dakika
chache ni ndogo ikilinganishwa na ile ya filamu za kawaida, ufundi wa
utengenezaji wake ni rahisi, na kwamba filamu za aina hiyo zinazooneshwa kwenye
mtandao wa intaneti, zinawafikia watu wengi zaidi.
Hivi sasa baadhi ya vijana wanataaluma nchini pia
wameanza kutengeneza filamu fupi, hali ambayo pia inatia moyo sana. Tafiti
zinaonesha kuwa, katika miaka mitano ijayo thamani ya soko la filamu fupi
nchini itapanda mara dufu.
Nimalizie makala yangu kwa kuiangazia filamu fupi
inayoitwa ‘Watu Wote’, iliyotengenezwa nchini Kenya, inayohusu shambulizi la
kigaidi la Alshabaab nchini Kenya, ambapo watu 2 waliuawa ndani ya basi eneo la
Mandera mwaka 2014.
Hii filamu imeteuliwa kushindania tuzo maarufu za
Oscar mwaka huu. Awali filamu hii ilikuwa imeshinda Tuzo za Oscar kitengo cha
wanafunzi mwaka jana na kuwa filamu ya kwanza kutoka Kenya kushinda tuzo hiyo.
Filamu hiyo ya Watu Wote imeorodheshwa kushindania
kitengo cha Filamu Bora Fupi: Matukio Halisi katika Tuzo za Oscar. Kwa kweli ni
hatua kubwa sana kwa waandaaji wa filamu hii.
Filamu hii inashindana na filamu nyingine nne
ambazo ni Dekalb Elementary; The Eleven
O'Clock; My Nephew Emmett na The Silent Child.
Hata kama haitashinda tuzo, lakini kitendo cha
kutajwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro cha kuwani tuzo tayari kimewatangaza
wasanii na waandaaji wa filamu, na hivyo kujijengea jina na mtandao mkubwa
kimataifa.
Filamu hii ina kisa cha kawaida, ikieleza hadithi
ya Kenya, kuhusu Wakenya na imeshirikisha waigizaji wa Kenya. Filamu inasimulia shambulio hilo la mwaka 2014
kaskazini mwa Kenya, ambapo maudhui ya uadui wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu
yanaangaziwa.
Ni mara ya kwanza ambapo filamu ya Kenya imeteuliwa
kuwania Tuzo ya Oscars, jambo linaloisaidia nchi ya Kenya kupanda ngazi.
Kufuatia mafanikio ya filamu hii fupi, Kenya sasa inaongoza katika kueleza
ulimwengu hadithi za Afrika.
Katika hadithi kuhusu shambulizi hilo, Waislamu
walikataa kujitenga na Wakristo walipoamriwa kufanya hivyo na magaidi wa
Alshabaab kutoka Somalia.
Japo ni hadithi ya kawaida lakini kinachoipa
hadithi hii upekee ni kitendo cha kuonesha undugu wa Wakenya na njia mwafaka ya
kukabiliana na ugaidi kote Ulimwenguni.
Filamu
ya Watu Wote imetengenezwa ikilenga kuwakumbuka mashujaa wa shambulizi hilo la
kigaidi.
No comments:
Post a Comment