Mlima Kilimanjaro |
KATIKA nchi hii kuna maeneo bora ya upigaji picha,
kuanzia Tanzania Bara hadi Zanzibar, kuanzia kwenye mlima mrefu hadi kwenye
maziwa yenye kina kirefu kabisa katika Bara la Afrika.Tanzania ni nchi ya maajabu na vivutio: mlima
mrefu Afrika (Mlima Kilimanjaro), mbuga bora yenye wanyama wa kuvutia duniani
ya Serengeti, yenye stori ya wanyama wanaohama kila mwaka na kurejea.
Bila kuzunguka, hebu tutafakari ni kwa namna gani
filamu na muziki vimeweza kuitangaza Nigeria? Tuanzie filamu, tasnia yao ya filamu (Nollywood)
imeweza kuwatangaza kwa kiasi gani? Tutapata jibu la haraka kwamba taifa hilo
limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala cha chini.
Steven Kanumba, enzi za uhai wake |
Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la
Afrika na dunia kwa kiasi fulani, haiwezi kutufanya tuumize kichwa sana kujua
kwamba taifa hilo, limeweza kupata matangazo mengi kupitia maigizo, na zaidi
kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.
Baada ya hapo hebu tujaribu kuwaza, ni kwa kiasi
gani kundi la muziki la P-Square limefanikiwa kuifanya Nigeria kuwa taifa
linalotajwa mara nyingi na watu mbalimbali duniani kila yanapoibuka mazungumzo
au majadiliano ya kukua kwa muziki barani Afrika? Je, tunaweza kuona matunda ya
wanamuziki kufanikiwa?
Tangu mwaka 1983, Nigeria ilishaanza kung’ara
kimataifa kupitia sanaa. Kuchomoza kwa mwanamuziki Sunny Ade, kisha kampuni
kubwa ya muziki duniani ya Island Records kubeba jukumu la kutangaza muziki wa
staa huyo, kuanzia albamu yake “Synchro-System” hadi ziara zake, kulifanya watu
wa mataifa mbalimbali kuanza kuifuatilia Nigeria.
Ongezea mafanikio ya wanamuziki wa kizazi kipya:
2face Idibia, D’Banj, Davido, Iyanya na wengine wengi. Jumlisha na ukweli
kwamba zama hizo hakukuwa na mtandao mkubwa wa mawasiliano kama ilivyo sasa.
Kisha pata jawabu ni kwa kiasi gani, sanaa
imeiweka Nigeria kwenye ramani ya dunia. Ukweli kwamba Nollywood imefikia
mafanikio makubwa na kushika namba tatu kwa utengenezaji na uuzaji wa filamu
duniani kwa sasa baada ya Hollywood, Marekani na Bollywood, India. Kwa kweli
Sanaa ni mtaji mkubwa nchini Nigeria.
Bila shaka mpaka hapo, tutakuwa tumeshajiridhisha
pasipo shaka kuwa sanaa imechangia ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini humo kwa
kiasi kikubwa sana.
Mamilioni ya watu huingia Nigeria kila mwaka kwa
ajili shughuli mbalimbali za utalii lakini zaidi kuona na kujifunza namna
wasanii wa nchi hiyo wanavyofanya sanaa za filamu na muziki.
Kwa kuangalia mfano wa Nigeria, ni wakati sasa kwa
mamlaka husika nchini kuamua kwa dhati kabisa kuwawezesha wasanii wa Tanzania
kwa maslahi ya Taifa.
Uwekwe mkakati mahsusi wa kuwatambua
watayarishaji/ wasanii na kudhamini kazi zao, watengeneze fedha na wasaidiwe
kwenda kujitangaza nje ya nchi. Baada ya hapo kutakuwa na matokeo yanayoonekana.
Mfano mdogo tu, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu alimchukua msanii wa filamu nchini, Aunty Ezekiel,
walikwenda Marekani kufanya kile ambacho walikisema kuwa ni kuutangaza Utalii
wa Tanzania. Ni mfano mzuri endapo unafanywa kwa nia ya dhati
kutangaza vivutio vyetu, japo sitaki kuzungumzia suala la kuwepo matumizi
mabaya ya fedha za umma.
Ni kwa sababu Tanzania yetu haina utaratibu wa
kufuatilia wageni wanaokuja nchini.
Kwa mfano, wakati Kanumba (marehemu Steven
Kanumba) alipokuwa anatingisha katika soko la filamu, watu mbalimbali walikuwa
wanakuja nchini kutoka mataifa tofauti kufuata filamu za Kanumba na za wasanii
wengine, nao walikuwa wanakwenda kuuza.
Kanumba alipofariki dunia, idadi ya watu waliokuja
nchini kufuata filamu zake iliongezeka maradufu. Watu walikuwa wengi sana. Hata
sasa watu huwa wanakuja lakini si kwa idadi kubwa kama kipindi kile. Wengi wanaokuja sasa mahitaji yao huwa ni filamu
za kina JB, Ray, Gabo, Jully Tax na wengine japo siyo sana.
Pia kuchomoza kwa wanamuziki kama Nasibu Abdul
(Diamond Platnumz) na ushindani wake na Ali Kiba, kumekuwa na matokeo ya ujio
wa wageni wengi, kuja nchini kununua kazi zao (ingawa kimagumashi kwani
serikali haipati kitu) na kwenda kuziuza kwao.
Diamond Platnumz |
Ali Kiba |
Ripoti ya Mtafiti mmoja inathibitisha kuwa wauzaji
CD za muziki na filamu, wanabainisha kuwa kuna kundi la watu kutoka Comoro,
Sudan, Ethiopia, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, DRC, Congo Brazzaville na
kwingineko mpaka Afrika Magharibi kuja nchini.
Miongoni mwao wapo mpaka ma-DJ ambao mbali na kazi
za Diamond na Ali Kiba, hufuatilia za wanamuziki wengine wa hapa nchini ili
kwenda kuboresha ladha ya kazi zao.
Kwa mujibu wa mtafiti huyo, mafanikio ya kina Diamond
nje ya Tanzania, yamesababisha ujio wa wageni wengi na kufanya biashara ya
muziki iende vizuri kila wanapokuja. Wapo wafanyabiashara wanaokuja kununua CD
kwa wingi, tena kwa jumla, nao husema wanakwenda kuzirudufu ili wakauze kwenye
nchi zao na kupata faida.
Kwa kawaida huanza kuulizia nyimbo za Diamond na Ali
Kiba, baadaye hutaka kujua wanamuziki wengine ambao wanafanya vizuri.
Kuna ma-DJ, ambao hutaka mseto wa nyimbo za
wasanii wa Tanzania ili wakawarushe katika madisko yao, na inasemekana wanakuja
Tanzania kwa sababu wanajua ndiyo nyumbani kwa kina Diamond, Ali Kiba na
wengine na hivyo hata muziki wa wasanii hawa unakuwa rahisi kuupata.
Hali hii inaonesha kuwa kama Sekta za Filamu na
Muziki zitakuwa rasmi [kwa maana ya rasmi na si kuwekewa stempu za TRA pekee]
na kuwekewa utaratibu, inaweza kusababisha utambuzi sahihi wa idadi ya wageni
wanaowasili nchini kitalii kwa matilaba ya sanaa na kadhalika.
No comments:
Post a Comment