Dec 31, 2017

Mwaka 2017 umekwisha, dira ya wasanii ni ipi?

Wasanii mbalimbali wakifuatilia mjadala kwenye ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)

Msanii akipiga tarumbeta

HEBU fikiria, unaamka asubuhi na mapema, unajiandaa na kubeba begi lako kisha unaelekea kituo cha basi, unalikuta gari na kupanda, lakini hujui unaelekea wapi!

Au mpo katika kituo cha mabasi, mara basi linakuja, kila mmoja analikimbilia na kupanda, tena mnafikia hatua ya kugombea siti, na safari inapoanza ndipo mnagundua kuwa gari haliendi kule mnakokwenda. Mnataharuki na kuanza kumpigia kelele dereva kumtaka asimamishe gari!

Dereva anawashangaa na analiegesha gari pembeni, kisha anawauliza kwani ninyi mnaelekea wapi? Hapo ndipo mnapojigundua kuwa kila mmoja anaelekea sehemu tofauti kabisa na linakokwenda gari!

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakembye

Kumbe hata dereva ana safari yake na alidhani kila abiria aliyepanda ndani ya basi alikuwa anakwenda kule anakoelekea yeye!

Sasa gari limeegeshwa kando ya barabara, abiria wanalumbana na kupiga kelele, kila mmoja anataka gari lielekee kule anakokwenda, hakuna tena kusikilizana bali ni kelele mtindo mmoja!

Badala ya kukaa chini na kuangalia utaratibu mzuri wa kuangalia mtafikaje mnakokwenda mnabaki kulumbana na kumtaka dereva apishe kwenye usukani ili mtu mwingine aendeshe gari!

Hii ndiyo hali halisi iliyopo kwenye sekta ya sanaa, miaka inazidi kusonga mbele lakini sekta ya sanaa inazidi kupotea kwa kukosa mwongozo.

Hali inakatisha tamaa, wasanii na viongozi wao wamefikia ukomo wa kufikiri, wanaonekana kulumbana tu pasipo kutafuta namna ya kutoka hapo walipo, nadhani kwa kuridhika na hali ilivyo au wamekata tamaa, ingawa bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi.

Hadi leo sekta ya sanaa haina dira (vision) bali kinachoonekana hapa ni kuwa kila mmoja anafikiria tu atatoka vipi.

Sanaa kama nguzo muhimu ya kuutangaza Utamaduni wa nchi, inapoteza mwelekeo kwa kuwa wasanii wamekosa dira ya pamoja kwa mustakabali wa maendeleo ya sanaa, kwani sanaa hukua na pia huweza kufa.

Dira ni maono au mwelekeo ambao mtu, kikundi, taasisi au taifa hujiwekea kama mwongozo ili kufikia kwenye maendeleo tarajiwa.

Kwa kukosa dira au kutokana na mifano niliyoieleza hapo juu, ni wazi kuwa sanaa zetu haziwezi kukua bali zinakufa na sasa zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Tusipochukua juhudi za ziada tutazika uasili wa sanaa zetu tulizopokezwa na wazee wetu kutoka kizazi hadi kizazi.

Mapokeo ya kazi ya sanaa katika jamii yoyote ile hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika.

Kama ilivyoelezwa katika Kitabu cha Utamaduni chombo cha maendeleo, nanukuu: “sanaa ndicho chombo ambacho jamii zisizokuwa na jadi ya kusoma na kuandika inatumia katika kuhifadhi na kuwasilisha kumbukumbu za mambo muhimu katika maisha yao” (uk.3).

Tujiulize: je, sanaa zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo na kuashiria Historia inayolingana na mila na desturi nzuri za kizazi husika?

Au kizazi hiki kinaweka kumbukumbu potofu ya sanaa zetu na uasili wake kwa vizazi vijavyo? Mfano nyimbo za matusi; Filamu na nyimbo za mapenzi peke yake au zisizo na asili yetu bali zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje?!

Haya ni mambo muhimu ambayo inabidi wasanii wote wajiulize katika kazi zao za kila siku. Je, ni kweli sanaa zetu zinaubeba utamaduni wetu na kuutangaza nje ya mipaka yetu?

Mada hii inajikita katika fani zote za sanaa kuanzia muziki, filamu, sanaa za maonesho na kazi za mikono, japo kwa muhtasari na ujumla wake inaogelea katika kazi mbalimbali za sanaa zilizotolewa katika kipindi hiki tulicho nacho na kilichopita.

Makala na mazungumzo yaliyotangulia yamekuwa yakihoji maswali mengi juu ya njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa kama kweli tunajenga juu ya msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi?

Tatizo la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu limekuwa gumzo na wengi wanajiuliza kwa nini tuna kosa alama ya mfano muziki wetu?

Nini chanzo cha wasanii wetu kuigiza na kuiga filamu chafu (zisizo na maadili)? Kwa nini hatuna dira (maono) wala sera (mwongozo)? Au ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo?

Kwa mfano, fani ya muziki ipo katika hatari kubwa ya kuporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika uteuzi wa maneno katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Kadri muda unavyozidi kwenda ndivyo tunavyozidi kuwapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone, Trumpet, Drums, Tumba n.k.

Matokeo yake tunakuwa na idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi, ndiyo maana kazi zao nyingi huisha kwa muda mfupi, huku tekinolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kukuta kila ala ipo studio kwenye computer.

Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka kwa fani hii. Je kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?

Pia safari ya sekta ya filamu kwa kweli imekuwa ni ndefu mno na hatujui lini tutafika kwenye maendeleo ya filamu, au mapambano yetu ya kuhakikisha kuwa na sisi tunapata kutambuliwa kimataifa na kukubalika bado yanaendelea ingawa kwa kiwango hafifu.

Sekta ya filamu Tanzania imesafiri njia ndefu sana hasa tunapoangalia katika suala la muda, lakini linapokuja suala la ukuaji ili kujilinganisha na maendeleo ya haraka katika sekta za filamu za nchi zilizoendelea duniani, inaonekana wazi kuwa tunayodai ni mafanikio tuliyoyapata ni sawa na fizikia ya muda wa safari… Hakuna uhalisia kabisa!


Hebu tujiulize; tumekwenda umbali upi? Ukweli tunaonekana kusimama pale pale tukiwa kama jiwe lisilotembea (unmovable stone).

No comments: