Peter Tosh |
Filamu ya Off Side |
Sikuwa shabiki wa
muziki wa reggae, ila nilipolazimika kusikiliza reggae nilipenda nyimbo za Lucky
Dube na Peter Tosh. Wanamuziki wote wawili kwa sasa ni marehemu.
Ukiusikiliza kwa
makini ujumbe ndani ya wimbo wa Equal Rights, utagundua kuwa ni chemsha bongo
ya aina fulani. Maneno ya Peter Tosh katika wimbo huu yanaakisi hali halisi ilivyo
katika shughuli za sanaa Tanzania, hasa muziki na filamu.
Ukiongea na wasanii
wengi wa Tanzania watakwambia kuhusu ndoto walizonazo, kama vile kuingia kwenye
soko la kimataifa na kadhalika, lakini hutawaona wakihangaika kutafuta taarifa
au maarifa, kufanya utafiti au mazoezi yanayostahili juu ya kazi zao ambazo wanataka
zikatingishe ulimwengu.
Pamoja
na kuwepo fursa nyingi pia tatizo kubwa linalowasumbua wasanii wengi ni dhana
dhalili (inferiority complex), kwani hawajiamini eti kwa kuwa hawawezi kuongea
Kiingereza kwa ufasaha kama wenzao toka Kenya, Uganda na kwingineko.
Wapo
waliowahi kukiri kuwa lugha ya Kiingereza ni kikwazo kwao kuigiza na waigizaji
wa kutoka nje ya nchi.
Japo katika muziki
tunajivuna kuwa na wasanii mahiri wanaoutangaza vyema muziki wa bongo fleva nje
ya mipaka yetu, kama Ali Kiba, Diamond Platnumz na wengine, lakini kumekuwepo
malalamiko ya kuibiana nyimbo na kukosa ubunifu kwa wengi.
Bado wanamuziki wengi
wamekumbwa na skendo za kuiba nyimbo za wenzao na kuzirekodi tena au
kuzitangaza kuwa ni kazi zao kwa kubadili majina.
Muziki wa Bongo Fleva
umejaa nyimbo nyingi zilizonakiliwa kutoka kwa wanamuziki mbalimbali wa nje, na
si hivyo tu bali wamekuwa wakiiga mpaka mavazi na uchezaji na hata namna ya
utengenezaji wa video unafanya kazi nzima iwe ni kivuli tu cha kazi kutoka nje.
Mara nyingi hata
baadhi ya watengeneza muziki, maarufu kama maproduza, wako tayari kukubali kuwarekodi
wasanii ambao walitakiwa kupewa ushauri wa kuacha kuimba.
Mara nyingine
waimbaji ni wazuri lakini muziki unakuwa hauna uhusiano wowote na uimbaji wao kutokana
na mapungufu ya produza, hivyo basi kuwa na maana kwa wale tu ambao wanafahamu
lugha inayoimbwa.
Ukijumlisha na
tatizo sugu la rushwa na upendeleo katika vyombo vya habari, nyimbo ambazo hazikustahili
kurushwa hewani hurushwa mara kwa mara, hivyo kuwafanya wanamuziki chipukizi
kuiga makosa.
Jambo hili la
mapungufu linafanyika si kwa muziki wa bongo fleva tu bali hata kwenye muziki
wa dansi, kwa mfano, ukiingia katika kumbi za muziki wa dansi, ni kuiga kutupu
kuanzia uvaaji wa wanamuziki, wachezaji wao, aina ya uimbaji, uchezaji, na
mbaya zaidi kwa kuwa karibu wote wanaiga sehemu moja bendi nyingi zinafanana
utadhani zimefanya mazoezi pamoja.
Ukija kwenye filamu
pia ni matatizo matupu. Filamu zetu (Bongo Movies) nyingi zinaaminika kukopi
hadithi na visa vya filamu nyingine za nje.
Pamoja na kuweko
kwa wasanii wazuri wa filamu, tatizo lililoota mizizi la kuwahusisha katika
uigizaji warembo maarufu ili kuuza filamu limechangia kuishusha hadhi kazi ya
uigizaji.
Pia uigaji wa kila
kitu kutoka Nigeria umeathiri kwa kiwango kikubwa katika kuendeleza soko la
filamu za Tanzania. Huwa najiuliza: hivi kwani ni lazima hata wanakijiji
katika filamu zetu wapake rangi kama wanakijiji katika filamu za Kinaijeria?
Je, waganga wa jadi
katika filamu zetu lazima wavae mavazi mekundu na kujichora kwa vile Wanaijeria
wanafanya hivyo? Hata majina ya filamu lazima yawe ya Kiingereza kwa kuwa Wanaijeria
wanafanya hivyo?
Yaani hatukuishia
kukopi stori tu, tumekopi hadi majina ya filamu zilizowahi kutoka, na mbaya
zaidi tukaiga hadi cover za filamu hizo jambo ambalo limetutia aibu kubwa
miongoni mwa mataifa mengine. Ingawa tumekuwa waigaji lakini hiki kimekuwa
kichekesho mno.
Aibu kubwa hutukuta
sisi tunaosafiri nje ya nchi au kuangalia sinema kwenye chaneli za nje, hasa
kwa vile tunajua kuwa mamilioni ya watu wanaangalia kutoka sehemu mbalimbali
duniani.
Halafu kuna yale
maandishi ya Kiingereza ambayo hudaiwa kuwa ndiyo tafsiri ya mazungumzo ya
Kiswahili katika filamu zetu, mara nyingi tumetia aibu kwa tafsiri mbovu, maana
mara nyingine hayaleti maana iliyokusudiwa kabisa, jambo linalozifanya kazi
zetu kujitoa zenyewe katika mashindano ya soko la dunia.
Yote haya
yametokana na wasanii kuwa na ubinafsi na kupenda kufanya kazi kibinafsi badala
ya kushirikiana. Ili tupenye soko la dunia tunapaswa kuuvunja ukuta wa fikra (ubinafsi,
uvivu na dhana
dhalili).
Wajerumani
walijikuta kwenye mtanziko mkubwa wa kuhitilafiana mitazamo, wa Magharibi
wakawa na mitazamo inayokinzana na wa Mashariki... wakashindwa kabisa kupatana,
na mwisho wakajenga ukuta wa kuwatenganisha.
Ukuta ule haupo
tena, ulibomolewa baada ya miaka mingi kupita lakini ni baada ya kujitambua
kwamba ukuta wa mawe ulikuwa ni matokeo ya ukuta wa kifikra na kimtazamo.
Walivunja ukuta wa fikra kwanza kabla ya kuvunja ukuta unaoonekana..
Waisrael wanajenga
ukuta kuzunguka Ukanda wa Gaza kujikinga na Wapalestina. Hii ni dhana
iliyojengeka mioyoni mwao lakini kuna siku ukuta huo utavunjwa.
Trump anataka
kujenga ukuta mpakani na Mexico, ni dhana iliyo mawazoni mwake na anataka
kuifanya iwe halisi. Atajenga sasa lakini kuna siku itafika ukuta huo utabomolewa.
Tuvunje ukuta wa
fikra sasa maana ukuta ni kitu kinachotokana na dhana. Dhana huzaliwa, hukua,
hubadilika na hata kufa pia. Hivyo nawashauri wasanii kuuvunja ukuta wa fikra
badala ya kuanza kumtafuta mchawi.
No comments:
Post a Comment