Mwanamuziki Msaga Sumu |
Mwanamuziki Sholo Mwamba |
MUZIKI wa
Tanzania unabadilika sana, wasanii wengi wamekuwa wakibuni mitindo ya aina
mbalimbali ili kuzifanya kazi zao ziende mbali na kuvuta mashabiki wa muziki
nchini na duniani kwa ujumla.
Miaka ya nyuma muziki wa dansi ndiyo ulikuwa ulishika
hatamu, muziki huu ulioanza kama klabu ambapo watu walialikana kucheza aina
mbalimbali za muziki wa kizungu mtindo maarufu uliojulikana kama ballroom
dancing. Kisha taratibu ukaumbika ukifuata muziki wa
soukous kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (rumba ya Kikongo) na tokea
hapo ikawa inaitwa ‘rumba ya Tanzania’.
Katika wakati huo pia muziki wa taarab, wa
Waafrika wa Pwani, haukuachwa nyuma. Ni muziki uliotokana na tamaduni nyingi,
hasa muziki wa Waarabu na Wahindi, na ni uimbaji wa mashairi uliofuata muziki
wa bendi.
Baadaye miaka ya 1990 ukaibuka muziki wa Hip hop,
ambao baadaye ukapata jina la Bongo Fleva, uliotokana na hip hop kutoka
Marekani, ikiwa na ongezeko la athira ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat,
dancehall, na mitindo ya asili ya Kitanzania kama vile taarab na dansi.
Wakati bongofleva ikitamba baadhi ya wasanii
wakaja na aina mpya ya muziki wa mduara, uliochanganywa kutoka muziki wa
taarab, dansi na mitindo ya asili.
Kiasili, mduara ni muendelezo kutoka kwa muziki wa
kikundi cha zamani cha Sunburst, ambacho miaka ya 1970 kilikuwa maarufu, hasa kwa
nyimbo za kitoto kama ‘Ukuti’. Kikundi hiki kiliwahi kutamba na wimbo wao wa Banchikicha.
Lakini kwa kuwa muziki hubadilika na kuja na
vionjo tofauti, hivi sasa nchini tuna muziki wa singeli unaotokana na
mchanganyiko wa ladha mbalimbali kama Taarab, Mduara, Bongo Fleva, Mchiriku na Vanga
(mdundiko) la Kizaramo ambalo ndilo limezaa muziki huu.
Muziki wa singeli uliibuka kutoka uswahilini na
kutapakaa nchi nzima na ulianza kutishia mustakabali wa muziki wa bongo fleva,
hasa hip hop.
Muziki huu ulianzia katika shughuli za harusi au
maulidi - hasa mkesha maarufu kama "vigodoro", ukakua na kuenea kwa
kasi kubwa, hasa jijini Dar es Salaam, ukajizolea mashabiki lukuki na
kufanikiwa kuzalisha vipaji kadhaa.
Pamoja na umaarufu wake, bado ni vigumu sana kwa
mtu wa makamo kuuelewa muziki wa singeli, tena pale atakaposhuhudia wakiwa
wanatumbuiza katika majukwaa lazima aseme hawa vijana wanashtua kidogo vilevi
ndiyo wapate mzuka wa kuimba.
Ukiachilia mbali mashabiki wa muziki huo, hata
asilimia kubwa ya wasanii wa muziki huu wakiwa wanatumbuiza wanakuwa na hulka
ya ajabu pindi wawapo jukwaani, hata kama unaupenda lakini hamu huisha pale tu
mambo yanapokuwa yanaenda kinyume na muziki wenyewe.
Tangu kuibuka kwa muziki huu nimekuwa najiuliza
kama unaweza kuwa mapinduzi mapya badala ya kuwa kaburi la muziki. Kama aina ya
muziki mwingine uliowahi kutamba hapa nchini kama mchiriku, mduara n.k. na
kupotea, nina shaka hata singeli inaonesha kupitia hatua za mwisho za kufa na
kuiacha bongo fleva kama ilivyokutwa!
Jambo la kwanza la kuzingatia katika muziki huu kuendelea
kubaki kwenye chati kama Bongo Fleva na Afropop zilikofikia ni aina ya mashairi
yanayoandikwa katika nyimbo zenyewe, na hii itasababisha kuwafikia hata watoto
na watu wa rika mbalimbali nchini.
Siyo lazima kuandika kwa lugha za kigeni ili wananchi
pamoja na watu wa mataifa waelewe, la hasha! Kuandika kwa maadili na mistari
itakayogusa jamii ndiyo nguzo kubwa ya kuweza kuufikisha mbali sana muziki huu
kwa kuzingatia tu kwamba kilichoandikwa hata mtoto anaweza kukitamka.
Nyimbo za Mapenzi siyo mbaya ila kuna walio chini
ya umri wa miaka 18, vipi kuhusu wao? Nini wanajifunza kutokana na aina hizi za
nyimbo? Je, vipi kama wakiwa wanaimba na kufuatisha mistari hiyo mbele ya
wazazi na ndugu zao wa karibu?
Suala jingine ambalo ni la msingi ni muonekano wa
Wasanii wenyewe, kwani wamekuwa wakivaa mavazi yanayotia hasira mbele ya jamii
inayowazunguka, hivyo, kuleta tafsiri mbaya kwa watazamaji na mashabiki
mbalimbali nchini.
Kiufupi, wananchi amekwishaupokea muziki huu japo
siyo kwa mikono miwili ila kwa jitihada mbalimbali ambazo watafanya wasanii
hawa lazima wafikie lengo na huenda ukawa muziki mkubwa sana tofauti na
unavyofikiriwa.
Suala la matumizi ya vilevi pia ni la kuangaliwa
kwa makini, kwani wasanii wa Singeli wengi wao wamekuwa wakikiri kutumia vilevi
tofauti kama vile bangi, ugoro pombe kali n.k., ili kuweza kuleta ‘amsha amsha’
katika majukwa wanayopanda.
Hili ni moja kati ya vitu vitakavyoushusha muziki
huu kiwango kwa asilimia kubwa na huenda ukachukiwa kuliko hata aina zingine za
muziki hapa nchini.
Wasipoangalia wasanii wa Singeli wataishia kusema
WanaBongo Fleva wameloga ingawa ni wao wenyewe wanajiloga kwa kutokuupa heshima
muziki wao.
Ikumbukwe pia hata miaka hiyo Bongo Fleva
ilivyokuwa ikianza muziki ulionekana kuwa ni uhuni na ni kitu kinachofanywa na
wavuta bangi mpaka kusababisha wazazi kuwakataza watoto wao wasijihusishe
kabisa na muziki huo.
Cha msingi sasa ni kujiwekea malengo katika muziki
wao na kuhakikisha hawafanyi mambo yasiyoipendeza jamii kama wakati ule wa
muziki wa Mchiriku na Mnanda ambao ulikuwa ni muziki wa fujo, pombe na aina
zote za ‘ushenzi’ zilikuwa zikifanyika huko.
Muziki ni ajira, malengo, ubora na heshima hivyo
lazima tu wayasimamie haya ili kuweza kutoboa, vinginevyo tutarajie kifo cha
muziki huu mapema.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment