LEO tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 18 tangu Baba wa Taifa na muasisi
wa taifa hili, Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza na kuzikwa Butiama,
kijiji alichozaliwa.
Mwalimu Nyerere alikuwa
kati ya viongozi wachache wa Afrika walioacha mwangwi katika utamaduni wa nchi
zao.
Nyerere alikuwa mwalimu. Ni
sahihi kusema silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere
kama kiongozi wa Tanganyika na baadaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa
na daima alikuwa akiwafundisha watu.
Yapo mengi kuhusu Mwalimu
Nyerere lakini ninachosema hapa ni ule mchango wa Mwalimu katika sekta ya
utamaduni.
Baada ya Tanganyika kuwa
huru Desemba 9 mwaka 1961, Mwalimu Nyerere aliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa
na Vijana mwaka 1962.
Wakati akiunda wizara hiyo,
alitamka wazi kwamba utamaduni ni kiini na roho ya Taifa akisema nchi inayokosa
utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho hivyo kukosa sifa ya
kuitwa Taifa.
Katika kipindi chote tangu
mwaka 1962, shughuli za sanaa na utamaduni zilipewa nafasi katika mfumo wa
kiserikali.
Wakati wa Mwalimu Nyerere
uhusiano wa sekta ya utamaduni na maendeleo ulitambuliwa hasa miaka ya 70.
Kwa mfano iliyokuwa Wizara
ya Utamaduni wa Taifa na Vijana (1979) iliwateua wataalamu waandike kitabu Utamaduni Chombo cha Maendeleo.
Katika dibaji ya kitabu hicho, aliyekuwa waziri wa wizara husika alitoa maelezo yaliyojaribu kuonesha uhusiano kati ya utamaduni, uhuru na maendeleo nchini. Nanukuu:
“Kuna sababu nyingi za kuutambua utamaduni kuwa ni chombo cha maendeleo.
Moja ni kuwa vipengele na fani mbalimbali za utamaduni ndizo zilizo katika
kiini cha umoja wa jamii. Utamaduni ni sehemu ya siasa ya Taifa letu lenye
msingi na shabaha ya umoja wa kweli. Uhuru wetu uliletwa na umoja. Maendeleo
hayapatikani bila ya uhuru na umoja. Hivyo utamaduni kama nguzo ya umoja, ni
chombo cha maendeleo (Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, 1979, uk. vii)”.
Katika jitihada za kukuza
utamaduni, Mwalimu Nyerere alianzisha Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita)
mwaka 1967, hiyo ikiwa ni miaka sita tu baada ya uhuru, ili kukuza Kiswahili
kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu,
mafunzo na biashara nchini.
Miaka minane baadaye,
Serikali ya Nyerere ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Baraza la
Muziki la Taifa (BAMUTA), ambayo yaliunganishwa mwaka 1984 kuwa Baraza la Sanaa
la Taifa la sasa (Basata).
Madhumuni ya Basata na
mabaraza yaliyolitangulia yalikuwa kufufua, kuendeleza na kukuza sanaa za asili
(utamaduni) mbalimbali za Watanzania.
Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kilianzisha masomo ya sanaa tangu mwaka 1966. Mwaka 1973, mafunzo ya
sanaa kwa walimu wa shule za msingi yalianzishwa katika Chuo cha Ualimu
Chang’ombe, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa katika Chuo cha Ualimu
Butimba, jijini Mwanza.
Chuo cha Sanaa Bagamoyo
ambacho sasa kinaitwa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa) kilianzishwa mwaka
1981 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wasanii ili kukuza na kuenzi utamaduni wa
Mtanzania.
Mwaka 1985 Serikali
ilianzisha matamasha na mashindano ya fani za utamaduni kuanzia ngazi ya
wilaya, mkoa, kanda hadi taifa.
Katika duru nyingi za
kimataifa, nchi yetu chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilisifiwa kwa jitihada za
kukuza utamaduni.
Lakini sasa tumejikuta
tukiangukia kule kule alikosema Mwalimu Nyerere wakati ule kuwa ni ‘kusanyiko
la watu wasio na roho’; tunapotea taratibu tukibaki kuwa taifa lisilo na
utamaduni wake, lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu, wasio na fahari ya
utaifa wao, wasio na umoja, uzalendo, mshikamano au heshima mbele ya mataifa.
Kwa kawaida utamaduni huipa
jamii utambulisho kama Taifa. Sura na haiba ya jamii ya nchi hueleweka na
kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake. Utamaduni hurithishwa kutoka
kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani.
Mwalimu Nyerere
alihakikisha utamaduni wetu haupotei bali unaendelezwa na alijua kuwa nyenzo ya
kuuendeleza ni kuanzisha vituo maalumu vya jumuiya vilivyojengwa katika kila
wilaya, 'Community Centres'.
Vituo vya jumuiya viliwekwa
chini ya maofisa utamaduni kuvisimamia na kuwa mahala ambapo serikali
ilipatenga maalumu kwa ajili ya shughuli za sanaa na kutafiti masuala
yaliyohusu utamaduni: Lugha, Mila na Desturi katika ngazi ya Wilaya.
Vituo vya jumuiya au vituo
vya kijamii yalikuwa maeneo ya umma ambapo wanajumuiya walikuwa wanakusanyika
kwa shughuli za vikundi, usaidizi wa kijamii, habari za umma, na madhumuni
mengine.
Leo hii vituo hivyo havipo
tena baada ya kugeuzwa kuwa ofisi za Manispaa au kukodishwa kwa watu binafsi
ili kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali vijana walio Manispaa
wanapewa sehemu nyingine maalumu kufanya shughuli zao za sanaa.
Kukosekana kwa vituo hivyo
vya kijamii na maofisa utamaduni kuwa chini ya Tamisemi badala ya idara ya
tamaduni yamechangia kuudidimiza utamaduni na sanaa nchini.
Utamaduni ukilelewa vizuri
ni chombo chenye nafasi nyingi za ajira, huongeza pato la eneo husika kwa
kuhamasisha maendeleo, huleta uzalendo, ubunifu wa mambo ya utamaduni,
huhamasisha utalii katika utamaduni, ni sehemu ya utalii ambayo kwa bahati
mbaya haijatumika kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.
Nina matumaini makubwa kuwa
Rais John Magufuli ataendeleza alipoishia Mwalimu Nyerere kwani tangu ameingia
madarakani mwaka 2015 namwona Mwalimu Nyerere mpya kupitia kazi mbalimbali
anazofanya na bila shaka hatosita kuingia pia eneo hilo la utamaduni kwa mapana
yake.
No comments:
Post a Comment