MAPOKEO
ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo,
mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio
ya jamii husika.
Kama
sanaa zenu haziakisi maisha yenu, basi mjue kuwa vizazi vyenu vitarithi mambo
yasiyokuwa yenu. Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia
hufa.
Unaweza
kujiuliza; Je, filamu zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa
na vizazi vijavyo? Au kizazi chetu kinaweka kumbukumbu potofu ya filamu na
sanaa zetu na utamaduni kwa vizazi vijavyo?
Niliwahi kuandika kuhusu uoneshaji wa video na
sinema kiholela unavyoathiri vijana na watoto kisaikolojia na kimaadili, na
kwamba umechangia kwa kiwango kikubwa kuporomoka kwa maadili ya kijamii na
kuongezeka kwa uhalifu miongoni mwa vijana.
Hii imetokana na kukosekana udhibiti wa mabanda ya
video yaliyochukua nafasi ya majumba rasmi ya sinema yaliyofungwa au kugeuzwa
kuwa ya kufanyia huduma nyingine za kijamii.
Mabanda haya yamekuwa yakionesha sinema chafu
maarufu kama ‘Pilau’, ‘Kachumbari’, ‘Kuchikuchi Hotae’, ‘Yale mambo yetu’,
‘Picha la ukweli’, ‘Ubwabwa’ na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si
rahisi kujua maana yake.
Siku hizi habari za kila aina kuhusu ngono zinapatikana kwa
urahisi kupitia televisheni, sinema, video za muziki, na intaneti. Na
imechukuliwa kama ni jambo la kawaida kutazama ponografia (picha za ngono).
Kutazama ponografia kunaweza kuwafanya watazamaji wafanye ngono
potovu. Imani kwamba wanawake hufurahia ubakaji, na kwamba wabakaji ni watu wa
kawaida imeenea sana miongoni mwa wanaume wenye mazoea ya kutazama ponografia.
Watafiti wanasema kwamba ukizoea kutazama ponografia unaweza
kuathiri uwezo wako wa kufurahia na kufanya ngono katika ndoa. Dk. Victor
Cline, mtaalamu wa kutibu watu wanaotawaliwa na mambo ya ngono, amewahi kueleza
kwamba watu wanaotazama ponografia hujikuta wakipata aina fulani ya ulevi
(addiction) unaowafanya kuendelea tu bila kuacha.
Mtu anayeanza kutazama ponografia kidogo-kidogo, asipoacha
mwishowe anaweza kuwa na mazoea ya kusoma habari na kutazama picha chafu zaidi
za ponografia. Dk. Cline anadai kwamba mazoea hayo yanaweza kuongoza kwenye
matendo mapotovu ya ngono.
Wanasayansi wanaochunguza tabia za wanadamu wanakubaliana na
jambo hilo. Dk. Cline anaripoti kwamba “upotovu wowote wa ngono unaweza
kuanza hivyo... na kwamba mtu hawezi kuacha hata akisumbuliwa sana na dhamiri,
maana inakuwa kama kilema.”
Hatimaye, huenda ikamfanya mtu anayetazama ponografia akajaribu
kufanya mambo yasiyo ya adili aliyoona, na mara nyingi matokeo huwa mabaya
zaidi.
Tatizo hilo linaweza kuanza hatua kwa hatua bila kutambuliwa.
Huongezeka na kuenea kama kansa. Kwa kawaida mazoea hayo hayakomi, wala hayawezi
kutatuliwa kwa urahisi kwa sababu yanakuwa yameathiri ubongo wa mtu husika.
Haishangazi kwamba mara nyingi wanaume waliozoea kutazama
ponografia hawakubali kwamba wana tatizo, na ni kawaida kwa wenzi wa ndoa
kukosana, nyakati nyingine kutalikiana, na hata mahusiano mengine ya karibu
huharibika kwa sababu hiyo.
Takwimu zinaonesha kwamba watazamaji wengi wa ponografia ni
wavulana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17. Kwa kweli, wengi wao
hujifunza masuala ya ngono hasa kupitia ponografia. Hilo lina matokeo mabaya
sana.
Mbaya zaidi sinema za ponografia hazioneshi kuhusu masuala ya mimba
za umri mdogo na magonjwa yanayoambukizwa kingono kama UKIMWI, jambo hilo huonesha
kwamba mambo yanayooneshwa katika ponografia hayana madhara.
Watafiti fulani husema kwamba kutazama ponografia kunaweza pia
kuathiri ukuaji wa kawaida wa ubongo wa mtoto. Uchunguzi wa athari za sauti na
picha za ponografia katika utendaji wa kawaida wa ubongo unaonesha kwamba
kutazama ponografia huathiri kabisa uwezo wa kawaida wa kufikiri.
Pia hudhuru ubongo
wa watoto unaoathiriwa kwa urahisi kwa sababu hufanya wasione mambo kihalisi na
hudhuru afya yao ya kiakili na ya kimwili, na huwazuia kupata furaha.
Ponografia huathiri mitazamo na tabia. Ujumbe wake unavutia hasa
kwa sababu si halisi na hivyo unaifanya ionekane kuwa yenye kusisimua zaidi
kuliko mambo halisi. Watu wanaotazama ponografia hutarajia mambo yasiyo halisi
ambayo huharibu mahusiano.
Ponografia inaweza kuwafanya wenzi wa ndoa wakose kuwa wanyofu
na wakose kuaminiana, sifa ambazo ni muhimu katika ndoa. Kwa sababu ponografia
hutazamwa hasa faraghani, mara nyingi humfanya mtu atumie hila na uongo. Wenzi
wa ndoa huhisi kwamba wamesalitiwa. Hawaelewi kwa nini mwenzi wao havutiwi nao
tena.
Mapambano ya kuacha mazoea ya kutazama ponografia hayapaswi
kuchukuliwa kijuujuu tu; yanaweza kuwa mapambano magumu. Dk. Victor Cline
ambaye ametibu mamia ya watu wenye mazoea ya kutazama ponografia asema hivi:
“Ahadi hazitoshi. Haitoshi kuwa na makusudio mema. Mtu mwenye mazoea ya
kutazama ponografia hawezi kufaulu peke yake bila kusaidiwa.”
Dk. Cline asema kwamba hatua ya kwanza ya tiba ni kumhusisha
mwenzi wake ikiwa amefunga ndoa. Anadai kwamba “Tiba hufaulu haraka ikiwa wote
wawili wanahusishwa. Wote wawili wameumia. Wote wanahitaji msaada.”
Ikiwa mtu ni kapela (hajaoa au kuolewa), mara nyingi rafiki
mwenye kuaminika au mshiriki wa familia anaweza kumuimarisha. Haidhuru ni nani
anayehusika katika tiba hiyo, Dk. Cline hueleza sheria moja thabiti: Sema
waziwazi kuhusu tatizo hilo na unapotumbukia tena katika mazoea hayo. “Siri ‘huua’,”
yeye anasema. “Huleta aibu na dhamiri mbaya.”
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment