NAUKUBALI sana
mkoa wa Tanga, una historia nzuri katika burudani na unaaminika kuwa ndio
kitovu cha burudani katika nchi hii, kuanzia kabumbu, muziki, sinema na
kadhalika. Tanga ni jiji lililo
ufukoni mwa Bahari ya Hindi.
Jina la mji wa Tanga
linaaminiwa kutokana na neno “tanga” yaani kitambaa kikubwa kinachokingamishwa
kwenye mlingoti wa jahazi, ilipewa jina hilo kwa sababu kisiwa cha Toten ilipo
hori ya Tanga kina umbo linalofanana na kitambaa cha aina hii.
Tanga ni miongoni
mwa mikoa michache nchini yenye historia kubwa ya soka la Tanzania. Ni ngumu
kuzungumza historia ya soka la nchi hii bila kuutaja mkoa wa Tanga, ambako
waliwahi kupita wachezaji wakubwa na kucheza hadi timu ya taifa ya Tanzania
(Taifa Stars).
Pia wachezaji
kadhaa wa mkoa huo wamewahi kutamba katika klabu kongwe za Simba na Yanga za Dar es
Salaam baada ya kuwika katika klabu zao za Tanga za African Sports na Coastal
Union. Historia ya soka la Tanzania haijawaacha Tanga, japo wenyewe
wanaonekana kutojali hali waliyonayo sasa kwenye medani ya soka.
Katika muziki,
Tanga ina historia nzuri kimuziki na sifa zake zilianza kusikika kuanzia enzi
za utawala wa Wajerumani, ambapo
shule ya kwanza ya serikali ilijengwa hapo enzi hizo hizo za Wajerumani, kisha
mji uliendelea kukua sana kutokana na kilimo cha katani, na hivyo kukusanya
vijana toka kila kona ya nchi kwenda kutafuta kazi katika mashamba makubwa ya
katani wakati huo.
Tanga ukawa mji
ambao kutokana na uwingi wa vijana wakati huo, shughuli za burudani ya muziki
nazo zilifikia kiwango cha juu kuliko sehemu nyingi Tanzania.
Ukizungumzia
historia ya muziki wa dansi, huwezi kukwepa kuzungumzia Tanga, kwani historia
inaeleza kuwa kabla ya kuanza vikundi vya muziki wa dansi kulianzishwa klabu za
kucheza dansi. Klabu hizo zikitumia muziki wa santuri, wanachama wake walicheza
na hata kushindana kucheza muziki kwa mitindo mbalimbali ya kigeni ikiwemo waltz, tango, chacha, rhumba na kadhalika.
Klabu za kwanza
nchini zilianzia Tanga. Kulikuwa na klabu kama Young Noverty miaka michache baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia,
wakati huo nchi ya Tanganyika ikiwa changa kabisa. Mtindo huu wa vilabu vya
dansi ulienea na baadaye kuingia Dar es Salaam na miji mingine iliyokuwa
imeshaanza wakati huo.
Vilabu hivi ndivyo
baadaye vikaanzisha vikundi vya kwanza vya muziki wa dansi. Hata majina ya
vikundi hivyo vya kwanza yalihusiana na klabu za burudani za wakati huo.
Kulikuwa na vikundi kama Coast Social
Orchestra, na kadhalika. Hivyo mji wa Tanga ulikuwa katika ndoto za vijana
enzi hizo.
Kati ya klabu hizo
kulikuweko klabu iliyoitwa Young
Nyamwezi, kama jina lake lilivyo ilikuwa ni klabu ya vijana kutoka
Unyamwezini. Hatimaye mwaka 1955 klabu hii ilianzisha bendi yake iliyoitwa Young Nyamwezi Band, bendi hii ilikuja
kukua, na baada ya Uhuru ilibadili jina na kuitwa Jamhuri Jazz Band.
Hakika kwa vijana
waliokuwa wapenzi wa muziki miaka ya 1960 na 70 ilikuwa lazima uifahamu Jamhuri
Jazz Band, muziki wake ulijulikana Afrika Mashariki nzima. Bendi hii ilikuwa
ikibadili mitindo ya upigaji wake na kupiga katika mitindo ya ‘Toyota’ na
hatimaye ‘Dondola’.
Ukiongelea filamu,
Tanga ndiyo mkoa wanaotoka magwiji wa filamu za kizazi kipya waliothubutu
kuandaa filamu miaka ya tisini japo mazingira yalikuwa magumu. Japo wengi
wanadhani filamu ya ‘Girlfriend (2003)’
ndiyo ilifungua ukurasa wa Bongo Movies,
ni filamu ya 'Shamba Kubwa (1995)’
ya Mwl Kassim El-Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za
kibiashara Tanzania.
Kipindi kile
teknolojia ilikuwa bado ndogo na vituo vya televisheni ndo kwanza vilikuwa
vimeanza, kwani wakati huo kulikuwa na vituo vya CTN, DTV na ITV tu, ambavyo
hata hivyo vilirusha matangazo yake jijini Dar es Salaam.
Filamu ya ‘Shamba
Kubwa’ ndiyo iliyowaibua wasanii ambao wamekuja kutamba katika ulimwengu wa
filamu; kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi,
na iliteka wengi.
Baadaye zilifuatia
sinema za ‘Love Story Tanganyika na
Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo
Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia
Hadaa (2000)' ya Mwl Kassim El-Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji. Zote hizi zilitengenezwa na magwiji kutoka
Tanga.
Filamu hizi
zilitengenezwa katika mfumo wa VHS (analogia), na hata uhariri wake
ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango
kidogo, lakini ziliweza kuvutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa
hadithi zake.
Filamu zingine
zilizotengenezwa Tanga ni ‘Shahidi’
ya Amri Bawji, ‘Fimbo ya Baba’ na ‘Chukua Pipi’ ambazo zimetayarishwa na
Shirika la Uzima Kwa Sanaa (UZIKWASA) la Pangani Tanga. Zipo pia ‘Ua la Matumaini’ na ‘Habari Kubwa’ za Mwl Kassim El-Siagi.
Ukiuacha mji wa
Dar es Salaam, ni mji wa Tanga ndio ulikuwa na majumba mengi ya kutazama
sinema. Katika mji wa Tanga kulikuwa na majumba ya sinema ya Majestic, Novelty, Regal na Tanga Cinema.
Hapa sijagusia
kuhusu mkoa wa Tanga kujaaliwa warembo wenye kujua kumliwaza mwanaume
akaliwazika, ndio maana inasemwa ‘Tanga ndiko mapenzi yalikozaliwa!’ Sijui kama
nitakosea nikisema Tanga ni ‘Los Angeles’
ya Tanzania. Yupo atakayebisha?
No comments:
Post a Comment