Jul 18, 2017

My Wife's Murder: Sinema ya Bollywood itakayokuacha mdomo wazi muda wote

Filamu ya My Wife's Murder ya India
NI kazi ngumu kufuatilia mipango ya muuaji usiyemjua, lakini muongozaji wa filamu za Bollywood, Jijy Phillip, amejaribu kufikiri nje ya boksi katika kisa cha filamu ya My Wife's Murder (Mauaji ya Mke Wangu). Filamu hii ilitengenezwa upya kufuatia filamu ya kwanza iliyoitwa ‘Madhyanam Hathya’, iliyoongozwa na Ram Gopal Varma. Hadithi ya filamu hii inaonekana kuchukua kisa cha Horace William Manton, mtuhumiwa mkuu katika kesi ya mauaji ya Luton Sack.

Lengo la sinema yoyote ni kumsisimua na kumfanya mtazamaji muda wote macho yake yasitoke kwenye runinga hadi mwisho, na filamu hii imefanikiwa. Ukianza kuiangalia utajikuta umekamatika ndani ya dakika 15 tu za mwanzo. Inspekta (Mkaguzi) wa Polisi Tejpal Randhawa (Boman Irani) anapewa jukumu la kuchunguza kesi ya mwanamke aliyekufa na mwili wake kupatikana katika bwawa.


Boman Irani

Anafuatilia kuona ikiwa kesi hiyo ina uhusiano na ripoti ya mwanamke aliyepotea iliyotolewa na Ravi Patwardhan (Anil Kapoor), miliki kampuni ndogo ya kutengeneza filamu, na mkwewe.

Baadaye inagundulika mwanamke aliyekufa katika bwawa ni Sheela (Suchitra Krishnamoorthy), mke wa Ravi aliyeripotiwa kutoweka. Kwa mujibu wa Ravi, Sheela aliaga anakwenda kuwatembelea wazazi wake, lakini akaambiwa na mkwe wake kuwa hajafika licha ya kuondoka nyumbani saa 24 zilizopita.

Ravi na mkwewe wanakwenda katika kituo cha polisi cha karibu kutoa taarifa za kutoweka kwa Sheela. Katika uchunguzi wake, Insp. Tejpal anaangalia uwezekano labda wakati Sheela anaelekea kwa wazazi wake kuna mtu (au watu) wasiojulikana, walimuua na mwili wake kutupwa katika bwawa.

Suchitra Krishnamoorthy

Lakini anapochunguza zaidi haoni jambo lolote linaloonesha lengo ya mauaji hayo, maana hakuna pesa yoyote iliyoibiwa na mwili wa Sheela hauna alama yoyote ya kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia. Kwa kuzingatia ukweli huu, Insp. Tejpal anamtilia shaka Ravi.

Msaidizi wa Ravi, Reena (Nandana Sen), anajaribu kusaidia Rav, lakini ushiriki wake unafanya mambo kuwa mabaya zaidi kwa upande wake na mchumba wake. Hapo ndipo sinema inaponoga, inamchukua mtazamaji hadi kilele cha msisimko, hasa Insp. Tejpal anapoanza kumchunguza Ravi na hatimaye anagundua mengi yaliyo nyuma ya mauaji ya Sheela.

Nandana Sen

Insp. Tejpal anakileta kisa kizima katika wakati ambao mtazamaji atake asitake atapata kiwewe, maana siri nzima ipo katika maisha ya Ravi.
Uongo mmoja unaanzisha mwingine, na hivyo kuwaacha wote Ravi na hata watazamaji wakijiuliza kama muuaji atafanikiwa kuukwepa mkono wa sheria.


Alamsiki.

No comments: