Jul 18, 2017

Tasnia ya filamu Tanzania ni sawa na soka bila refa!

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiongoza maandamano ya Wasanii wa Filamu

HADI leo sijajua ni ‘impact’ gani iliachwa na maandamano ya mwezi Aprili mwaka huu ya wasanii wa filamu walioandamana kushinikiza kusitishwa kwa uuzwaji wa filamu kutoka nje ya nchi kwa madai zinaharibu soko la ndani!
Athari pekee niliyoishuhudia ni ufa uliojitokeza kati ya wasanii waliounga mkono maandamano na waliopinga, kiasi cha kuibua mihemko iliyosababisha kutishiana maisha na kutukanana matusi ya nguoni.

Kwa sasa Sekta ya filamu Tanzania ipo ‘Babeli’ ingawa ilifikia hatua ya kutingisha Afrika. Sidhani kama kuna mtu atabisha kuwa filamu za kibongo ‘hazikutesa’ Afrika Mashariki na nchi za Maziwa Makuu. Filamu hizi zilisaidia kwa kiwango fulani kuitangaza Tanzania na kuwatangaza wasanii wa nchi hii. Sinema hizi ziliuzwa kwa wingi mitaani, watu walizichangamkia; wanawake na vijana ndio wakiwa wateja wakubwa wa sinema hizi.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiongoza maandamano ya Wasanii wa Filamu
Msanii wa Vichekesho, Steve Mengere maarufu kama Steve Nyerere akiongea kuhusu maandamano ya Wasanii wa Filamu

Uchumi wa soko huria la filamu ulichangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sinema za Kiswahili. Ilikuwa ukipita mitaa ya jiji la Dar es Salaam au katika miji mikubwa unaona mabanda ya kuoneshea video yametapakaa kila kona. Pia unakutana na wauzaji wa filamu wakitembeza barabarani.

Na kwa tuliopata bahati ya kutembelea nchi jirani za Kenya, DR Congo, Rwanda, Burundi na kadhalika, tunathibitisha kuwa filamu hizi zilitesa sana maeneo hayo. Lakini sasa hali imebadilika!

Inawezekana filamu zinazotoka nje ya nchi zimechangia kuharibu soko la filamu za ndani, lakini kabla wasanii hawajaandamana kushinikiza kusitishwa kwa uuzwaji wa filamu kutoka nje ya nchi walipaswa kutoa kwanza boriti kwenye macho yao ndipo watazame kibanzi kwenye macho ya wengine.

Utoaji wa filamu zetu ndio umelifikisha soko la filamu hapa, maana ulikuwa ni kama soka bila refa, mkutano bila mwenyekiti, darasa bila mwalimu, au nyumba (familia) bila mzazi…

Wasanii waliwaamini sana wafanyabiashara, waliahidiwa milioni kadhaa kwa sinema; watengenezaji sinema wakawa wanalipua kazi; waigizaji hawalipwi vizuri; utengenezaji sinema ukafanywa haraka haraka. Sinema zikatengenezwa kwa siku tatu hadi wiki moja, na ndani ya mwezi mmoja tu ziko sokoni. Haraka haraka…

Wasanii wa filamu wakaigiza bila script wala mazoezi, baadhi ya watengenezaji filamu wakatumia mwanya huo kula uroda na wasichana warembo (na Umiss ukawa kigezo kikubwa cha kupata nafasi ya kucheza filamu, haijalishi ana kipaji cha kuigiza au la), baadaye wasanii wetu wakaanza kujilinganisha na Wanaijeria!

Sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa sinema za Nigeria zilitingisha katika nchi yetu, zilileta athari kubwa na kubadilisha tamaduni za Nigeria na Afrika. Sekta ya filamu ya Nigeria imesaidia kuleta mageuzi na kuhifadhi utamaduni wa Kiafrika pamoja na kuwepo nguvu za utandawazi.

Sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa sinema za Nigeria zinatumia lugha za asili za Nigeria kusimulia habari za Afrika. Ni kweli kuwa lugha na utamaduni wa watu ni muhimu katika utambulisho wao na matarajio yao kwa ajili ya kujitawala.

Aidha, sikatai na wala hakuna atakayebisha kuwa sinema za Nigeria zinaelezea maisha ya jadi, mchanganyiko na ya kisasa ya watu wa Nigeria.
Lakini kwanini wasanii wetu walizitumia kama kipimo chao cha filamu?

Kwanini waliamua kufuata nyayo za Wanaijeria katika kuzalisha sinema za Tanzania? Matokeo yake wakajikuta wameacha kusimulia hadithi zetu na kusimulia za Wanaijeria.

Sinema zetu zikawa zinasimulia uchawi, mapenzi au mikasa ya kijamii kama wanaijeria. Wasanii wetu wakawa wanaiga hadithi za Wanaijeria na namna yao ya uchezaji. Kwanini Watanzania wasizione sinema za Nigeria zinafaa kuliko za kwetu?

Sasa wasanii wanalalamika kuwa Watanzania hatununui sinema zinazotolewa na Watanzania wenzetu. Kwa kuwa sinema za nje zimejaa, zinauzwa bei chee na hazilipi kodi.

Wanaweza kuwa sahihi. Lakini, wakumbuke ni Watanzania haohao walioacha kuangalia sinema za nje na kuzipokea sinema za ndani, na sasa wameamua kurudi kuangalia sinema za nje. Kisa? Haziwavutii tena na zinatengenezwa kwa kulipuliwa.

Lakini nimekuwa najiuliza, kwanini hata zile zinazotengenezwa vizuri bado hazinunuliwi? Kwanini hazifurahiwi? Kwanini hazitolewi maoni na hazitangazwi? Tunachokiweza ni kuziponda tu!

Na  wasanii wasilalamike ti bali wakumbushane kwamba sinema ni sanaa inayochukua muda. Hawawezi kutengeneza sinema ikakamilika ndani ya wiki au mwezi mmoja tu. Wajipe muda katika kuifanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Wasiangalie kufanya kazi haraka haraka ili wapate pesa na kutatua matatizo yao. Wakumbuke kuwa ukitoa kazi nzuri yenye ubora hukaa na huuzika miaka nenda miaka rudi, tofauti na kazi ambazo baada ya wiki mbili zinakuwa hazina tena soko.

Wakumbushane kujipa muda katika uandaaji wa filamu: Mwezi mmoja wa mikutano kupanga mambo (wapi itapigwa picha, nani atafanya nini, waigizaji watatoka wapi, watafanya nini), mwezi mwingine kupanga usanii (mazoezi ya waigizaji, mazingira yao), mwezi mwingine wa kupiga picha. Baada ya miezi mitatu, mingine miwili ya kuhariri na kusahihisha makosa.


Kisha kifuate kipindi cha kuitangaza kusudi iuzwe. Ukichunguza sana utagundua kuwa sinema haiwezi kumalizika chini ya miezi sita kwa mazingira ya Tanzania. Ndiyo maana wenzetu wanatoa sinema moja tu kwa mwaka lakini pesa wanazopata wanakula kwa miaka kibao. Sisi tulikuwa tunatoa sinema kila mwezi lakini pesa yake ni ya kujikimu tu.

No comments: