Filamu ya Chalii wa Ngarenaro |
KIGEZO cha pili cha kusaidia soko la filamu ni
jukwaa la uwasilishaji; watazamaji wanahitaji majukwaa ya habari. Falsafa hii
ni muhimu wakati unaposhughulikia maudhui yanayowafaa watazamaji. Maudhui ya jukwaa la uwasilishaji katika dunia ya
kisasa ya filamu hayaishii tu kwenye kazi ya usambazaji, yanakwenda ndani zaidi
ya soko la filamu lilivyo. Jukwaa husaidia kuwasilisha mawazo kwa watu katika
njia itakayojumuisha mitazamo yao.
Jukwaa muafaka litampa urahisi mtengenezaji wa
filamu kuendana na ushindani wa soko. Watoaji filamu wanatakiwa kuandaa takwimu
ya watazamaji na kukutana nao katika dunia yao iliyostawi kwenye kundi la
teknolojia ya digitali.
Filamu ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine,
kuzitangaza na kuzisambaza ni vitu vyenye umuhimu sawa. Lazima kuwe na
mkakati wa kujitangaza kwenye mitandao ya intaneti. Hii itaongeza mipaka katika
utekelezaji wa kampeni ya kuzitangaza.
Filamu wa Hollywood ya The Notebook |
Lakini Tanzania bado tuna tatizo kubwa, Tanzania
bado ina kiwango cha chini cha watu wanaotumia intaneti ukilinganisha na nchi
zingine katika Afrika.
Taasisi ya Mawasiliano ya Kimataifa (ITU)
katika ripoti yake inaonesha kuwa kati ya watu 56,877,529
waliopo nchini, watumiaji wa intaneti ni 3,700,000. Watumiaji wa facebook 3,700,000.
Idadi hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne katika Afrika
Mashariki nyuma ya Rwanda yenye watu milioni 12,159,586
lakini ina watumiaji wa intaneti 3,724,678, watumiaji wa facebook 490,000.
Kenya yenye watu milioni 48,466,928
ina watumiaji wa intaneti 39,664,377,
watumiaji wa facebook 5,500,000.
Uganda yenye watu 41,652,938 ina watumiaji wa
intaneti 13,023,114,
na watumiaji wa facebook 2,200,000.
Sudan Kusini yenye watu 13,096,190 ina watumaji 2,179,963, na facebook 180,000. Na
Burundi yenye watu 11,936,481 ina watumaji 526,372, facebook 450,000. Takwimu
hizi ni za Machi 31, 2017 na
zinapatikana www.internetworldstats.com.
Ili tuweze kupiga hatua kwenye biashara ya filamu
tunahitaji nguvu kubwa kuwaelimisha wasanii na jamii faida za kutumia mitandao
ya jamii inayoweza kusaidia utoaji habari za filamu na kujenga jamii yenye
wafuasi, na humo, mijadala inaweza kujadilika, kipengele muhimu kabisa cha
kuleta ufahamu au kampeni ya kujitangaza.
Jumuiya hizi ni maeneo ambayo watu wanaotembelea
wanaweza kupata habari zaidi, kushiriki katika mijadala, kujiunga na majarida,
na kubadilishana ujuzi na mawazo na watu wengine, kwa lengo la kupanua wigo
mkubwa wa watazamaji.
Katika miaka michache iliyopita, mitandao
imesaidia sana kufanya uwepo wa gharama nafuu katika kutangaza na kuuza kazi
kwa watengeneza filamu na hata kwa studio.
Katika baadhi ya tasnia za filamu za nchi
zilizoendelea, ni nadra na kosa kubwa kutokuwa na tovuti ya kutangaza filamu
kabla haijaoneshwa.
Kwa takwimu za ITU ni ishara kuwa tunahitaji
kuelekeza namna nzuri mitandao ya jamii inavyoweza kusaidia na kufanya kampeni
yenye kuleta mwamko wa namna ya kujitangaza.
Njia ya haraka na madhubuti ya kujenga jamii ya
watazamaji kupitia vyombo vya habari za mtandao ni kutengeneza tovuti za filamu
ili kutoa makala, vipande vifupi vya filamu, kupakua picha, miziki, sauti (soundtrack),
mabango (wallpapers), n.k.
Pia kuwapa mashabiki fursa ya kupata habari kuhusu
stori, wasifu wa waigizaji, kuchangia maoni yao na hata kuonesha interest
zao katika filamu kwa jumla kutasaidia kuenea kwa taarifa au tetesi za
filamu.
Kuhodhi mitandao ya intaneti kama Facebook, Myspace, Youtube, Vimeo n.k., wadau wanaweza kuwa na
mawasiliano na watumiaji. Siku hizi, facebook-Twitter-youtube ni njia za
kujitangaza kwa haraka, watayarishaji lazima waangalie namna ya kuongeza tovuti
zao na kuongeza matangazo na taarifa zao muhimu.
Matangazo ya kulipia kwenye televisheni, radio,
magazeti, majarida, na majarida ya kitaaluma ni muhimu pia.
Mtayalishaji wa filamu anaweza kuwa na ukurasa
wake wa uchapishaji kwa habari za filamu, ambapo taarifa mbalimbali kuhusiana
na filamu na maendeleo yake zitapatikana kwa wasomaji kwa kipindi cha muda
fulani.
Kutokana na uwezo wake wa kuonesha filamu kwa
watazamaji wengi kwa haraka, kutoa habari za nyota wa filamu, vipande vya
filamu (trailers), mahojiano na muongozaji wa filamu na kadhalika,
vinaweza kuwekwa kwenye maonesho ya televisheni, au vipindi vya habari za
burudani.
Matangazo ya filamu yaliyoandaliwa vizuri (Advance
trailers) na picha zinazoonesha yaliyofanyika nyuma ya Kamera (behind-the-scene
footage) pia vinaweza kuwekwa kwenye vipindi maalum (documentary)
kwa ajili ya vituo vya televisheni na kuvutia watazamaji kuitafuta sinema
husika.
Katika jitihada za kibiashara, kutafuta masoko ni
kama uwanja wa vita, na biashara ya filamu haiwezi kukwepa hili. Baadhi ya njia
makini zinaweza kutafsiri upya mfumo na kuweka kiwango kipya.
Kwa mfano, filamu inaweza kutolewa kwenye vyombo
vyote vya habari kwa wakati huohuo, ikiruhusu watazamaji tofauti kuchagua lipi
jukwaa linalowafaa.
Naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment