Sridevi Kapoor |
TASNIA ya filamu ya India maarufu kwa jina la ‘Bollywood’ hadi sasa imekwisha tengeneza
mastaa wengi wakubwa waliojulikana duniani, wakatengeneza pesa nyingi na kupata
heshima kubwa ndani ya India na hadi nje ya mipaka ya India. Kwa mpenzi yeyote wa sinema, iwe ni sinema za Hollywood (tasnia ya sinema ya
Marekani), au Nollywood (tasnia ya
sinema ya Nigeria) bado atakuwa amekwishaziona filamu za India.
Nollywood mara nyingi wamekuwa wakiiga kutoka
Bollywood, tasnia ambayo imewatengeneza waigizaji maarufu duniani kama Amitabh
Bachchan, Shahrukh Khan, Aamir Khan, Salman Khan, Dilip Kumar, Raj Kapoor,
Dharmendra, Hrithik Roshan, Rish Kapoor na wengine wengi kwa upande wa wanaume.
Filamu ya English Vinglish |
Unapoongea na wapenzi wa sinema za Bollywood, mara
nyingi watakwambia kuwa Amitabh Bachchan ndiye supastaa wa kwanza halisi na
baba wa sinema za Bollywood, jambo ambalo japo si kweli lakini haliko mbali na
ukweli.
Hadi sasa, ni Dhundiraj Govind Phalke (aliyejulikana pia kwa jina la utani la Dadasaheb Phalke) ndiye ‘baba halisi wa
sinema za Kihindi’.
unapoongelea masupastaa
wa Bollywood, kuna mtu anaitwa Rajesh Khanna (1942-2012) ndiye
anaaminika kuwa supastaa wa kwanza halisi wa Filamu za Bollywood, akipata hadhi
hiyo kutokana na kazi zake zilizokubalika sana kwa wakosoaji wa filamu (film
critics) na kufanya vizuri sana sokoni kiasi cha kuweka rekodi kadhaa ambazo
nyingine mpaka leo bado hazijavunjwa.
Hata Amitabh Bachchan aliwahi kukiri waziwazi kuwa
Rajesh Khanna ni funga kazi. Mastaa wengine wa sasa wa Bollywood na hata
wanaochipukia mara nyingi humtaja Rajesh kama muigizaji aliyewapa msukumo kuwa
waigizaji.
Ila unapoongelea waigizaji wanawake wa Bollywood, muigizaji
Sridevi Kapoor (53) ndiye supastaa halisi wa kwanza wa kike wa filamu za Bollywood
kutokana na kuacha historia kubwa katika filamu hizo.
Hivi karibuni Sridevi alikaririwa akisema kuwa
ukiwa mtu wa watu (msanii maarufu) hupaswi kuishi kama mtawa, kwa maana ya maisha
ya kujifichaficha, bali unapaswa kuwa kioo cha jamii kwelikweli.
Kabla ya Sridevi alitanguliwa na waigizaji wa kike
wengi waliopata mafanikio makubwa: kama Madhubala, Waheeda Rehman, Sharmila
Tagore, Rekha, Hema Malini, Jaya Bachchan, Nargis, Mumtaz na wengineo lakini
ujio wa Sridevi aliyekuwa mrembo na msanii mwenye kipaji cha pekee, ikawa stori
mpya katika ulingo wa filamu za Bollywood. Umaarufu wake ulitokana na kazi na
siyo skendo.
Wandishi kibao walijaribu kutunga stori huku
akilini mwao wakimfikiria Sridev katika husika hizo. Sridevi amecheza filamu
nyingi sana za lugha mbalimbali na kufanikiwa sana kimauzo lakini lugha
nyingine alizotumia kucheza filamu hizo hazijui mpaka leo.
Baadhi ya filamu zilizompa umaarufu mkubwa ni
pamoja na Sadma, Chandni, Gumrah, Judaai, Lamhe, Khudah Gawah, Nagina na
English Vinglish iliyotoka mwaka 2012.
Sridevi alianza kuigiza tangu akiwa mtoto mwaka
1967 na ndiye mwigizaji wa kike aliyekuwa namba moja miaka ya 1980.
Sridev Kapoor katika filamu ya English Vinglish |
Anaaminika kuwa mmoja wa waigizaji waliotamba sana
katika sinema za kihindi kwa muda mrefu na kuwa na mfanikio makubwa hata baada
ya umri kuanza kumtupa. Na aliporudi tena kwenye ulingo wa sinema mwaka
2012 kama muigizaji mkuu katika filamu ya English
Vinglish alifanikiwa sana kuliteka soko la filamu za Bollywood japokuwa alikuwa
nje ya ulingo wa filamu kwa miaka 15 mfululizo.
Leo hii wapo masupastaa wakubwa wa kike wa
Bollywood, waigizaji kama Aishwarya Rai, Kajol, Kareena Kapoor, Rani Mukerjee
na wengineo, lakini wote hawa walitanguliwa na Sridevi ambaye ameendelea kuwa
juu, wengine wengi wameshindwa kufika level yake licha ya kupata umaarufu mkubwa
sana kwa kazi zao.
Hivi karibuni, Sridevi
alikaririwa akiwaasa waigizaji kuwa siri kubwa ya wao kufanikiwa si kujaribu
kuishi maisha ya ‘kuigiza’ na kuvikwepa vyombo vya habari, maana unapokuwa mtu
wa watu (kwa maana ya msanii staa) huwezi kuishi kitawa.
No comments:
Post a Comment