Aug 17, 2018

Tumeitupa misingi ya michezo kwa binadamu



MICHEZO si tu kwamba ina faida kubwa sana kwa mwanadamu na nchi, pia ni chombo cha kuwasilisha tunu msingi katika kuboresha ubinadamu na katika ujenzi wa jamii ya amani na ya kindugu.

Kwa kauli hiyo yatari tunapata wazo kuu juu ya michezo kwa ujumla ya kwamba michezo imekuwa na lengo kuu msingi tangu zamani za kale la kujenga undugu na amani.

Kama mchezo ni chombo cha kuwasilisha tunu ya binadamu mwenyewe, kujieleza mwenyewe, kukubalika mwenyewe na kujikubali, inamaana kwamba nchi yoyote haiwezi kutambulikana na utaifa wake bila kuwa na utamaduni wao, na mojawapo ya viungo vya utamaduni huo vinavyounganisha katika dunia hii ni michezo.


Mfano, kuna baadhi ya mataifa mbalimbali ambayo wameweza kujitambulisha kwa mavazi na alama mbalimbali… ukiona ‘vazi’ fulani tayari unajua ni kutoka nchi gani, hivyo basi hata michezo ni chombo muhimu sana katika kuendeleza jamiii.

Moja ya vitu muhimu sana vinavyoweza kuitambulisha nchi yoyote mbele ya jumuiya ya kimataifa ni michezo.

Aidha michezo huweza kuwa kielelezo kikubwa na utambulisho wa taifa katika kutoa burudani, kujenga nidhamu, kujitangaza kiuwezo na kukomaza afya, ya mwili na akili.

Uzuri wa michezo ni kwamba katika kufanikiwa inakuwa furaha ya wote, tuzo zinatoka za kimataifa, jina la nchi linang’aa na ndiyo inakuwa njia ya moja kwa moja ya kujitangaza kwenye utalii.

Faida ya michezo siyo kwa wachezaji tu bali hata mashabiki ambao kufurahi kwao huwa ni kinga dhidi ya maradhi, hasa inapokuwa michezo ya ushindani, kama soka, mpira wa kikapu, mpira wa pete, riadha, mbio za baiskeli, tenisi n.k.

Michezo ni mizuri kwa afya ya ubongo, ni njia ya pekee ya kuufanya ubongo kuchangamka na kufanya kazi vizuri, mwanadamu anapaswa kutenga angalau muda mchache wa mazoezi. 

Kucheza inatufundisha kutumia mawazo yetu na tunakuwa wabunifu wa mambo, kwa kutumia fikra zetu katika maisha.

Mara ngapi nchi fulani inatangaza vipaji vya wachezaji wake inaposhiriki michezo ya kitaifa na kimataifa, mifano ipo mingi, siku za karibuni tumesikia jinsi wachezaji wa soka wakihama kutoka timu moja hadi nyingine mara baada ya kombe la dunia, maana michezo imewaweka sokoni.

Kutokana na umuhimu wa michezo katika jamii kila kipindi cha kihistoria, binadamu amekuwa akishiriki michezo katika tamaduni, mila na sanaa. Tunajua michezo ya mila na desturi ilikuweko tangu zamani, imekuwepo mieleka, kuruka, kukimbia kulenga shaba ya mishale, kuogelea n.k.

Michezo hii ililenga kujiamini na kuwa na utambulisho wa kila jamii ambayo iliitwa michezo ya jadi, hata ndugu zetu waliopelekwa kwenye utumwa na kukutana na watu wa mataifa mbalimbali walieneza jadi zao katika michezo hiyo, iliyowasaidia sana kukabiliana na matatizo yaliyokuwa yanawakumba katika utumwa huo.

Lakini baada ya michezo ya kisasa kuingia kama mpira wa miguu, mpira wa meza, ndondi, mbio, baiskeli, magari ya mashindano, mashindano ya farasi na michezo mingine mingi, historia ya jadi ikalegeza thamani yake na kuanza kutawaliwa na mambo mawili: fedha na ushindani.

Si vibaya endapo michezo itatumika kama chanzo kikubwa cha kuingiza fedha na nchi zikaweka mikakati kwa kutumia mabilioni ya pesa kuweka msingi wa michezo, lakini hatupaswi kuuweka kapuni ubinadamu wetu kwa kuitupa historia ya jadi na kuegemea kwenye fedha na ushindani tu.

Hatupaswi kusahau kwamba michezo ya jadi kwanza ilikuwa inalenga undugu zaidi, urafiki zaidi, burudani zaidi, katika kushirikiana kwa pamoja na kuishi kwa amani.

Leo hii katika viwanja mbalimbali vya mipira (si tu uswahilini bali hata viwanja vikubwa), kuna uwoga wa kurudi salama au kutokurudi salama, hii ni hatari kubwa!

Karne hii inazo changamoto nyingi ambazo zimejitokeza kwenye michezo kama vile, kinachotangulizwa ni fedha na ushindani, au kuwepo na dharau na ubaguzi wa rangi, kutaka kushinda kwa kila njia, wakati mwingine hata watu wanaofanya michezo hiyo kupenda kutumia dawa za kuongeza nguvu ili washinde. 

Changamoto ni nyingi kwani mabadiliko ya jamii yetu wazazi wengi hawawafundishi tena watoto umuhimu wa michezo ni nini, kwa sababu watoto walio wengi ukiongelea mchezo, kitu cha kwanza kichwani ni kufikiria kushinda kabla ya burudani na furaha ya kushiriki na wengine.

Watoto walio wengi wanapokwenda kwenye michezo tayari wana wazo lazima washinde tu, na kumbe uwajibikaji wa jamii zetu kuanzia katika familia ni muhimu sana kuwafundisha tangu utoto umuhimu wa michezo ya pamoja kwanza ni kufurahi, kunyoosha viuongo kwa ajili ya kutunza afya bora na siyo tu kushinda na kupokea zawadi. 

Maana katika mchezo lazima mmoja tu ashinde, mfano wa hivi karibuni tumeona machozi, masikitiko na majonzi kwenye fainali za kombe la dunia nchini Urusi. 

Tukisimama katika misingi yake tutaweza kuifanya michezo kusimama katika kusudi lake ili baadaye ikuze uchumi, kwa sababu itakuwa imejengewa miundombinu mizuri, nchi ikawa na wachezaji wengi katika michezo tofauti, na kuwa chanzo kikubwa cha ajira.

Michezo ina utajiri mkubwa kwa binadamu si katika biashara au malumbano, bali utajiri wa kuunganisha watu, kabila, jamii, taifa na mataifa, nikitoa mfano wa changamoto zinazokabili nchi za Ulaya, ukimbizi na uhamiaji kupitia njia ya baharini.

Tumeshuhudia watu wengi, hasa vijana, wakipokelewa katika vituo mbalimbali katika nchi za Ulaya, wengine hata hawajui lugha ya mahali hapo, lakini kinachowaunganisha ni zile talanta zao walizo nazo za kucheza michezo mbalimbali.

Michezo izidi kuboreshwa katika tamaduni zetu ili iweze kutuunganisha badala ya kututenganisha, iboreshe utu kwanza kuliko kujali mali, ndipo tutaweza kujenga jamii ya utu yenye kupendana kama ndugu.

No comments: