WASANII wakongwe na
mahiri nchini wa sanaa ya maigizo, hususan wa vichekesho wanazidi kupukutika, na
kuwaacha wasanii wachanga wakiwa katika mkanganyiko.
Nawakumbuka wasanii
ambao walikuwa mahiri sana katika sanaa ya maigizo na vichekesho enzi za uhai
wao na sasa hatupo nao ni pamoja na Ibrahim Raha (Mzee Jongo), Fundi
Said (Mzee Kipara), Rajab Kibwana Hatia (Mzee Pwagu) na Ali Said Keto (Pwaguzi).
Wengine ni Hamis Tajiri (Janja au Meneja Mikupuo)
Tunu Mrisho (Mama Haambiliki),
Branco Minyugu, Bartholomew Milulu (Masawe), Said Ngamba (Mzee
Small), Said Maulid Banda (Max) na
wengine.
Wasanii hawa waliifanya sanaa ya maigizo, hususan
ucheshi (comedy) kujizolea umaarufu mkubwa nchini na hivyo kuwafanya vijana
wengi nchini kuingia kwenye sanaa ya vichekesho.
Rais John Magufuli alipokwenda kumjulia hali King Majuto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili |
Nakumbuka nikiwa mdogo tulizowea kusikiliza kipindi
cha Mahoka, na vichekesho vya Pwagu na Pwaguzi vikirushwa Redio Tanzania (RTD),
hakuna shaka kuwa hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi
walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu.
Na hata waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali za
burudani, hasa jijini Dar es Salaam na miji mikubwa, walishuhudia burudani
kutoka katika vikundi vya sanaa kama DDC Kibisa, Muungano Cultural Troup,
Mandela Theatre, Bima Modern Taarab, Super Fanaka, Reli Kiboko Yao, JWTZ,
Tancut Almasi, UDA, Urafiki n.k.
Kwa kweli kila mtu aliyekwenda kwenye kumbi za
burudani alifurahia sana vichekesho vya kina King Majuto, Mzee Small, Branco Minyugu,
Bartholomew Milulu, Mzee Jangala na wengineo.
Wiki hii tasnia ya
vichekesho imepata pigo, tena ni pigo kweli kweli kwa msiba uliowagusa na
kuwashtua wengi sana, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa sanaa ya vichekesho,
hasa kutokana na kifo cha gwiji wa vichekesho ambaye umahiri wake ulikuwa wa
hali ya juu.
Ni msanii mkongwe na maarufu nchini Tanzania na
Afrika Mashariki, Mzee Amri Athuman maarufu kama King Majuto, aliyefariki dunia
wakati akipokea matibabu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es
Salaam, majira ya saa 2 usiku wa Jumatano Agosti 8, 2018.
Mchekeshaji huyo veterani alikuwa amelazwa Hospitali
ya Taifa Muhimbili katika chumba cha wagonjwa mahututi kabla ya kufariki kwake.
Baada tu ya kifo chake watu maarufu ndani na nje
ya Tanzania walituma salamu za rambirambi kwa familia yake kupitia mitandao ya
kijamii, miongoni mwao akiwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuwa King Majuto atakumbukwa
kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na
uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na
kuunga mkono juhudi za Chama Cha Mapinduzi na Serikali katika kuhimiza
maendeleo.
Kwa kweli King Majuto alikuwa mfalme katika tasnia
ya maigizo ya uchekeshaji nchini Tanzania na Afrika Mashariki, aliweza
kujizolea umaarufu mkubwa kupitia namna ambavyo alikuwa akiigiza na kuwa
miongoni mwa watu wenye mvuto mkubwa miongoni mwa wasanii.
Niliwahi kufanya kazi na King Majuto, iliyotufanya
kuwa karibu sana kwa kipindi kirefu, ulikuwa mradi wa ‘Pamoko One Love’,
uliohusu uelimishaji kuhusu watu wanaoishi na ualbino ukisimamiwa na Shirika la
Under The Same Sun.
Katika kazi hiyo iliyowahusisha pia wasanii
Chausiku Salum maarufu kama Bi Chau, Mrisho Mpoto na wanamuziki Khadija Shaban
(K-Sha) ambaye wengi humwita Keisha na Faridi Kubanda maarufu kama Fid Q.
Katika mradi huo uliotufanya kuzunguka takriban
mikoa kumi na mbili tukielimisha, kuonya na kuburudisha, mimi nilifanya kazi
kama mtaalamu wa sauti.
Katika kipindi hicho nilijifunza mengi kutoka kwa
King Majuto, hasa ucheshi, busara na namna alivyoweza kucheza na hadhira kiasi
cha kuwa na mvuto wa aina yake.
Afya ya King Majuto ilizorota zaidi mwaka huu
ambapo alipelekwa nchini India kwa matibabu baada ya Rais John Magufuli na
wapenzi wa sanaa ya King Majuto kumchangia ili kunusuru uhai wake kabla ya
baadaye kurejea nchini Tanzania.
Wiki chache zilizopita taarifa za uongo za kifo
chake zilisambaa mitandaoni kabla ya familia yake kukanusha mara kwa mara.
Majuto aliyezaliwa mkoani Tanga Kaskazini mwa
Tanzania mwaka 1948 alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka tisa. Amecheza kwa
mafanikio makubwa kwenye filamu mbalimbali zilizozidi kumpa umaarufu mkubwa,
japo alikuwa maarufu hata kabla ya ujio wa televisheni nchini.
Kabla ya kifo chake tayari alikwisha wasamehe
baadhi ya waandaaji na wasambazaji ambao inasemekana walikuwa wamemdhulumu
mamilioni ya fedha baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison
Mwakyembe kutishia kuwashitaki watu hao.
Kwa kweli
nilistushwa sana na msiba wa nguli huyu wa sanaa ya vichekesho ambaye kwangu
alikuwa rafiki, nikiri kuwa japo binadamu tumeumbiwa kifo lakini mshtuko
nilioupata hauelezeki.
Umati uliojitokeza siku
ya Alhamis wakati wa kuagwa kwake pale katika ukumbi wa Karimjee na baadaye nyumbani
kwake Tanga wakati wa mazishi yake ni ushuhuda tosha kwamba mzee huyu alikuwa
kipenzi cha watu na alistahili kuitwa ‘King’, na tasnia ya filamu na maigizo ni
sekta yenye nguvu kubwa sana, kama ingetumiwa vizuri ingeweza kuchangia pato
kubwa mno.
Japo makala yangu
ya leo imetokana na kifo cha King Majuto lakini hailengi kuzungumzia jinsi
nilivyomfahamu nguli huyu bali kuangalia undani wa tasnia ya maigizo na
vichekesho na mustakabali wake.
Kwa kweli wachekeshaji ni wasanii wenye umuhimu wa
aina yake katika jamii. Ndiyo hutufanya tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi
ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni au
hata kukutana nao mitaani.
Miaka ya 1990 baada ya kuanzishwa vituo vya
televisheni nchini, viliibuka vipindi vya ucheshi vya kina Mzee Small, King
Majuto n.k. ambao nikiri kuwa walituburudisha sana.
Baadaye wakaibuka Max na Zembwela na 'Mizengwe'
yao na kuendelea kutupa burudani kulingana na wakati. Kisha likaibuka kundi la Ze
Comedy (EATV) lililosheheni wachekeshaji vijana waliouteka umma wa Watanzania
kwa vichekesho vyao na staili ya aina yake.
Kuanzia hapo kukaibuka wasanii na vikundi vingi walioanza
kuigiza kwenye runinga na kutoa filamu kila kukicha ingawa wengi wao
walichoigiza ilikuwa ni mizaha na wala si vichekesho kama walivyotaka
kutuaminisha.
Sanaa ya ucheshi ni sanaa yenye lengo la
kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, katika televisheni, filamu,
na kwenye majukwaa. Unapocheka ndivyo maisha yanavyokuwa bora zaidi!
Ucheshi ni mwanga unaouangazia moyo, ni igizo
lililobuniwa kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa
ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha,
matendo, na hata wahusika wenyewe.
Ucheshi huhoji na kufuatilia yalipo mapungufu, makosa
au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na
wasaa wa kufurahia maisha.
Sanaa ya ucheshi kwa kawaida imegawanyika katika
mifumo ya aina kuu mbili: comedian-led (wachekeshaji), kwa kutuletea vichekesho
vilivyopangiliwa vizuri, utani au michoro na situation-comedies (sit-com)
ambayo huelezea kisa kilichomo ndani ya hadithi inayosimuliwa.
Vipengele vyote vya ucheshi vinaweza kuonekana kwa
pamoja na/ au kuingiliana. Pia kuna mfumo wa ucheshi unaojulikana kama 'Comedy
hybrids' ambapo huenda pamoja na aina nyingine: musical-comedy (ucheshi kwa
njia ya muziki), horror-comedy (ucheshi wa kutisha), na comedy-thriller
(ucheshi wa kusisimua).
King Majuto aliweza kufiti kwenye aina zote hizi
za ucheshi, kuanzia ucheshi wa papo kwa papo jukwaani hadi ucheshi wa kwenye
runinga, kwa kuwa alikuwa na kipaji cha aina yake tofauti na wengine ambao
hulazimisha kutuchekesha badala ya kutufanya tucheke.
Kwa mfano, niliwahi kushuhudia jinsi wasanii
fulani wa vichekesho walivyokuwa wakihangaika kuchekesha papo kwa papo pale
kwenye ukumbi wa Starlight!
Aina hii ya ucheshi wa papo kwa papo inahitaji kipaji
na uelewa mkubwa sana wa jambo unalotaka kuliigiza ili lichekeshe, kwani
kichekesho kinategemeana sana na tukio la papo kwa papo au lililotokea!
Hii ni kwa sababu sisi Waafrika kwa sehemu kubwa
hutumia ishara, mifano katika hadithi na matukio ya kuchekesha. Ucheshi kwa
kawaida huwa na mwisho wenye kufurahisha, ingawa wakati mwingine unaweza
kuegemea mambo yanayosisimua au mabaya.
Sikatai, bado tunao baadhi ambao ni wachekeshaji
wazuri sana lakini wengi wao wamekosa mwongozo na sidhani kama walipata nafasi
ya kujifunza kwa hawa wakongwe ambao sasa wametutoka.
Wachekeshaji wetu walipaswa kujifunza kwa King
Majuto ili kujua kilichomfanya abaki kwenye chati kwa miaka yote tangu
alipoanza kuchekesha, na pia waongeze wigo wa ubunifu na kujifunza zaidi kama
wanataka kuendelea kutusisimua.
Aidha nawashauri wajifunze kwa wenzetu,
wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu,
wazame ndani ya akili za watazamaji kujua mahitaji yao na wasome alama za
nyakati.
Kinachoua sanaa ya ucheshi ni pamoja na kukosa
ubunifu, dharau, kukosa malengo, kutojua watazamaji wanataka nini, na kulewa
umaarufu.
Ndiyo maana nasema kuwa King Majuto atabaki kuwa
nembo ya tasnia ya uigizaji wa vichekesho nchini Tanzania hata baada ya kifo
chake.
No comments:
Post a Comment