Jul 18, 2017

Sonam Kapoor: Kufanya kazi nyuma ya Kamera kumenisaidia

Mwigizaji maarufu wa Bollywood, Sonam Kapoor

FILAMU zimepitia hatua kwa hatua zikianzia kwenye mawazo hadi kuwa nyenzo muhimu ya burudani na mwasilisha taarifa muhimu wa karne hii. Kutengeneza sinema nzuri inahitaji gharama kubwa. Na kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao huwezi kutabiri watapendezwa na nini. Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua.

Mara nyingi, matayarisho yanayofanywa kabla ya upigaji picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo huchukua muda mrefu katika utengenezaji wa sinema. Kama tu ilivyo kwa mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana matayarisho.


Mwigizaji Sonam Kapoor wa Bollywood ni mmoja wa watu waliopata nafasi ya kufanya kazi nyuma ya kamera, kwa maana ya kushiriki mchakato matayarisho kabla ya upigaji picha na wa utengenezaji wenyewe.

Sonam Kapoor

Alianza kama muongozaji msaidizi kwenye filamu ya ‘Black’ ya Sanjay Leela Bhansali mwaka 2005, kisha akaingia katika uigizaji akiigiza drama ya mapenzi ya Saawariya mwaka 2007, ambayo ilimfanya kuteuliwa kwenye tuzo za Filmfare akiwania Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike aliyecheza kwa mara ya kwanza.

Alipata mafanikio yake ya kwanza kibiashara miaka mitatu baadaye katika komedi ya kimapenzi ya ‘I Hate Luv Storys’ (2010). Sonam anasema uzoefu wake wa nyuma ya kamera umemsaidia sana kuelewa dhana ya ufanisi wa filamu na kuhusu mifumo.

Anasema: “Imesaidia sana. Mchakato wa utengenezaji filamu sio tu kuandaa mchezo kuhusu mwigizaji. Ni ushirikiano wa kila mmoja katila timu ya uzalishaji.”

Sonam mwenye umri wa miaka 32, anasema uzoefu huo umemsaidia kufanya filamu ya ‘Neerja’ vizuri na kuteuliwa katika Tuzo za Taifa za Filamu.

Kwa sasa anashiriki filamu ya ‘Padman’ ya R. Balki. Pia ataonekana katika filamu ijayo ya ‘Veere Di Wedding’ ambayo pia inawahusisha mastaa Kareena Kapoor Khan na Swara Bhasker.

Sonam Kapoor alizaliwa tarehe 9 Juni 1985, ni binti wa muigizaji maarufu, Anil Kapoor. Ni mmoja wa waigizaji wanaolipwa zaidi Bollywood na ameshinda tuzo kadhaa, zikiwemo za Filmfare na Tuzo za Taifa za Filamu.

Kuanzia mwaka 2012, alikuwa mmoja wa Watu 100 Mashuhuri wa India wa jarida la Forbes kutokana na mapato na umaarufu wake. Sonam amesomea Sanaa ya Maonesho United World College of South East Asia nchini Singapore.

Kwa sasa Sonam anasaidia kampeni mbalimbali, ikiwemo kuelimisha juu ya saratani ya matiti n.k. Anajulikana katika vyombo vya habari kwa utu wake, na mara nyingi hujulikana kama mmoja wa mastaa wa Bollywood wanaopenda mitindo (fashionable).

No comments: