· Wengi hawana sifa zinazohitajika na hawataki kujifunza
UKWELI tuna tatizo kubwa kwenye tasnia ya filamu Tanzania
kwa waongozaji wengi kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby...
action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza
muigizaji aweze kuuvaa uhusika ipasavyo kwa kutegemea script ilivyo. Kama
muigizaji atashindwa kuvaa uhalisia, mara nyingi hilo siyo kosa lake bali ni
kosa la muongozaji kwa kushindwa kumtengeneza, na hutafsiri uwezo wa muongozaji
ulipokomea.
Mtazamo wangu, mtu yeyote
anayetaka kuwa muongozaji mzuri wa filamu katika tasnia yetu anapaswa kujifunza
kwa makini hatua kwa hatua kwa kusoma machapisho na kuhudhuria warsha na
mafunzo ya muda mfupi — si kwa ajili ya kujifunza njia nzuri ya utengenezaji wa
filamu, bali kwa ajili ya kupata msukumo wa kufuatilia masuala muhimu ya
uumbaji wa kisanii kwa bidii na kwa umakini.
Miezi
michache ijayo nitazindua vitabu viwili nilivyoandika, kimojawapo kikiwa ni “Uongozaji
wa Filamu – Sifa, Misingi na Kanuni za Uongozaji.” Nimeandika kitabu hiki
nikijaribu kutoa mchango wangu kwa kile ninachokijua ili kuwasaidia waongozaji
wa filamu katika nchi hii, nikiamini kuwa tatizo kubwa kwenye filamu zetu ni
kukosa uongozaji makini.
Methodolojia ya kitabu changu
ipo katika msingi mkuu wa pendekezo ambalo kitabu hiki ni kama mwongozo wa
filamu unaoelezea kile ambacho muongozaji anatakiwa kukifanya. Nikilenga zaidi kwenye
maeneo ya lugha ya filamu, mbinu za kuwaongoza waigizaji, misingi ya uongozaji,
na maswali ambayo muongozaji anapaswa kujiuliza.
Kuna dhana sababishi nyingi
ambazo ni za lazima sana kwa muongozaji mzuri wa filamu: ubunifu, msimamo, elimu/ufahamu
kuhusu sanaa, ufahamu kuhusu watu, uwezo wa kufanya kazi na wengine, utayari
katika kuyakubali majukumu, ujasiri, ustahimilivu, na nyingine nyingi. Lakini
dhana sababishi iliyo kuu kabisa, ambayo ikikosekana itatangua mengine yote, ni
ubayana (clarity) — ubayana kuhusu hadithi na jinsi kila kipengele ndani
yake kinavyoweza kuchangia kwenye hadithi nzima, na pia ubayana kuhusu kile
kinachowasilishwa kwa watazamaji.
Kwa waliosoma lugha ya filamu
watakubaliana name kuwa filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na
vitendo zaidi, hivyo, haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili
afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu, ndiyo maana
kuna watu wanaangalia filamu za Kihindi au Kikorea na wanaburudika na kuelewa
kinachoendelea.
Msingi mkuu wa hadithi katika
sinema ni kuwa, filamu ni zaidi ya kiwanda (sekta), ni zaidi ya onesho
linalowakutanisha nyota. Filamu ni lugha. Utengenezaji wa filamu una lugha
yake. Kwa hiyo, filamu ni lugha inayotumika kusimulia hadithi, na sauti
inayotumika kusimulia hadithi hiyo ni kamera, wakati muongozaji wa filamu ndiye
msimuliaji wa hadithi hiyo.
Muongozaji wa filamu ni mtu
ambaye huwa anaongoza utengenezaji wa filamu. Kwa ujumla, muongozaji wa filamu
hudhibiti masuala ya kisanii na kimchezo katika filamu, na kutengeneza taswira
kutoka kwenye script wakati wa kuwaelekeza watendaji wa kiufundi na
waigizaji katika kutimiza dira ya filamu. Muongozaji huwa ana jukumu muhimu
katika kuchagua waigizaji, wabunifu wa uzalishaji, na masuala ya ubunifu katika
utengenezaji wa filamu. Katika baadhi ya nchi za Ulaya, muongozaji hutazamwa
kama ndiye mtunzi (author) wa filamu au mmoja wa watunzi.
Muongozaji wa filamu hutoa
mwelekeo/maelekezo kwa waigizaji na watendaji katika kutengeneza dira (vision)
kwa njia ambayo filamu hatimaye itaonekana. Waongozaji huhitaji kuwa na uwezo
wa kupatanisha panapokuwa na tofauti katika ubunifu na kusimamia katika mipaka
ya bajeti ya filamu. Kuna njia nyingi ya kuwa muongozaji wa filamu. Baadhi ya
wongozaji wa filamu walianza kama waandishi wa filamu (screenwriters),
wahariri wa filamu au waigizaji. Waongozaji wengine wa filamu wamesoma katika
shule za filamu.
Waongozaji hutumia mbinu
mbalimbali. Baadhi huelezea kwa muhtasari (outline) kisa chote na
kuwaachia waigizaji kufanya faraguzi kwenye mazungumzo yao, wakati wengine
hudhibiti kila nyanja, na kuhitaji waigizaji na wafanyakazi wengine kuyafuata
maelekezo kwa usahihi. Baadhi ya waongozaji pia huandika miongozo (screenplays)
yao wenyewe au kushiriki katika kuandika na washirika wao wa muda mrefu katika
uandishi. Baadhi ya waongozaji hupenda kuhariri au kuonekana katika filamu zao,
au kutunga muziki kwa ajili ya filamu zao.
Muongozaji wa filamu ana kazi
nyingi zisizokuwa na mwisho, lakini kazi iliyo muhimu zaidi ni ile ya
kuwaongoza waigizaji na kuhakikisha kuwa anapata zao bora kabisa litakaloonekana
kwenye televisheni. Kumekuwa hakuna ushauri wa kutosha unaotolewa kuhusu jinsi
ya kuwaongoza waigizaji wanapokuwa kwenye eneo la upigaji picha. Binafsi
nimewahi kusoma vitabu na machapisho kadhaa kuhusu uongozaji, na kitabu
kimojawapo kikiwa ni ‘Directing Actors’ (Kuwaongoza Waigizaji),
kilichoandikwa na Judith Weston.
Pengine hiki ni kitabu kilichowahi
kunivutia zaidi ambacho kinaelekeza nguvu katika kipengele hiki maalum cha
namna ya kuwaongoza waigizaji. Hata watu wengi waliokisoma niliowahi kukutana
nao wanakisifia kitabu hiki, lakini kwa mtazamo wangu nadhani kuwa kinayafanya
mambo haya kuwa ngumu kwa kuwa hakijikiti zaidi katika jinsi ya kuongoza – pale
unapozungukwa na shinikizo au matatizo mengine mengi – nimegundua kwamba
ushauri ambao machapisho na watu wengi wamekuwa wakiutoa kwenye kuwaongoza
waigizaji ni ule ambao mara nyingi usiotekelezeka.
Muongozaji wa filamu ni
kiongozi wa timu katika uzalishaji wa filamu na msimulizi wa hadithi kwa kutoa
picha halisi. Muongozaji mzuri ni yule anayehakikisha kwamba sehemu zote za
filamu zimeandaliwa katika hali ya ubunifu na kuletwa pamoja: ndiye mbunifu na
kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji, anayeutafsiri mwongozo wa filamu
kutoka kwenye karatasi na kuuhamishia katika taswira halisi yenye sauti kwenye
video, na ndiye anayeiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa
taswira hiyo. Pia ana wajibu katika masuala ya masoko na kuelewa changamoto za
filamu katika muda na bajeti.
Nafasi ya muongozaji katika
mchakato wa filamu kijadi inatofautiana sana na ni ngumu sana. Muongozaji wa
filamu huonekana kama kiongozi wa timu ya wafanyakazi wengine, na hutoa aina
fulani ya nguvu ya kuongoza. Kwa mujibu wa mtazamo huu, matokeo ya mwisho
hayaamuliwi na mahitaji ya mwongozo wa filamu, upigaji picha, uigizaji, au
uhariri; muongozaji wa filamu ndiye huandaa mazingira ya picha kwa ajili ya
matokeo ya mwisho.
Ikiwa waongozaji wanataka
kuijua misingi na kanuni za kuwa muongozaji wa filamu lakini hawana elimu rasmi
ya uongozaji, wanapaswa kuwa watu mwenye nia ya dhati ya kupenda kujifunza na
kufuatilia sinema na wenye kipaji kikubwa cha sanaa kama sharti kuu.
Inavyoonekana, kila sinema
inayozalishwa ina muongozaji wa filamu nyuma yake. Huyu ni mtu anayesimamia
masuala ya ubunifu na ya kiufundi ya uzalishaji wa sinema, kama vile usaili,
usanifu, na taa. Mtu yeyote mwenye shauku katika masuala ya sinema na mwenye
kujitoa kwa dhati anaweza kuongoza filamu, lakini tu atafanya vizuri zaidi kama
ana jicho la kisanii katika kuyaona matukio yenye kusisimua katika mchezo. Ili
kufanikiwa katika sekta hii yenye ushindani, unapaswa kuthibitisha kwamba una
utaalam unaotakiwa ili kutengeneza sinema itakayofanya vizuri sokoni.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment