Jun 25, 2014

USHINDI WA SHOESHINE FESTICAB: Kwanini hatutilii maanani filamu fupi?

 Amil Shivji


TAKRIBAN wiki mbili zilizopita nilikuwa mjini Bujumbura nchini Burundi kwa mwaliko wa Shirika la Kijerumani la GIZ, ambapo Mtandao wa Wanafilamu wa Afrika Mashariki ulikuwa ukizinduliwa rasmi, sambamba na Tuzo za filamu kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu la Burundi (Festicab) 2014, linalofanyika jijini Bujumbura.



Kabla ya safari yangu hii, nilipata bahati ya kupitia nchi zingine kama mbili ambapo nilipata nafasi ya kukutana na watengeneza filamu wa nchi hizo, na kwa kweli nilijifunza mengi kutoka kwao.



Katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Burundi (Festicab 2014) kulikuwa na kazi nyingi nzuri kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na hata nje ya ukanda huu. Katika kila kipengele ni sinema moja tu iliyoshinda, huku Tanzania ikipata tuzo moja kutokana na sinema fupi ya “Shoeshine (2013)” iliyotengenezwa na kuongozwa na Mtanzania, Amil Shivji.



Kwa kuwa ndugu Amil hakuwepo kwenye tamasha hilo, mimi kama Mtanzania mwenzake na kiongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania, niliipokea tuzo hii kwa niaba yake, kwa furaha tele, nikiami kuwa ameitangaza nchi yetu kwa njia moja au nyingine kutokana na ushindi wake.



Sinema hii fupi yenye dakika 24 imetengenezwa katika mazingira ya mitaa yenye pilikapilika jijini Dar es Salaam, ikielezea mitazamo mbalimbali kuhusu vijana wasafisha viatu, vijana wanaomaliza vyuo vikuu na hata wanasiasa na kadhalika.



Hadi sasa sinema hii fupi imeshampatia ndugu Amil Shivji heshima kubwa kimataifa kiasi cha kumfungulia njia ya kufanya kazi kimataifa. Hata hivyo, mwanzoni wakati akiiandaa kazi hii ambayo ni ya kwanza kwake alikuwa na wasiwasi hasa ikizingatiwa kuwa walio wengi na hata soko letu limejikita katika filamu ndefu tu, hivyo anayetengeneza sinema fupi kuonekana kama anapoteza muda wake tu.



Sinema hii hadi sasa imeshashinda tuzo kadhaa kama hii ya “Best East African Short Film” katika tamasha la Festicab 2014 nchini Burundi, nyingine ni “Best African Short Film” kwenye Tuzo za African Film Development Awards 2014, “People’s Choice Award” kwenye tamasha la 16 la Zanzibar International Film Festival 2013.



Pia imeingia kwenye mchujo wa kuwania tuzo ya “Best Short Film” kwenye Africa Magic Viewer’s Choice Awards 2014; “Best Director” kwenye Africa Magic Viewer’s Choice Awards 2014; “Official Selection” kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu Rotterdam 2014; “Official Selection” kwenye Tamasha la Filamu la Luxor African 2014; “Official Selection” kwenye Tamasha la 36 la Kimataifa la Filamu la Durban 2013; “Official Selection” kwenye Tamasha la Film Africa 2013.



Pia “Official Selection” kwenye Tamasha la Filamu la Euro African 2013; “Official Selection” kwenye Tamasha la Filamu la Africa In Motion 2013; “Official Selection” kwenye Tamasha la Filamu la 44 la Tampere 2014, na “Official Selection” kwenye Tamasha la Filamu la 33 la Verona African 2013.



Kupitia kazi yake hii, Amil amepata pesa kupitia mfuko maalum wa kuwawezesha watengeneza sinemaa fupi wa Afrika, Africa First Focus Features grant, baada ya script yake kushinda kipengele cha 2013, kwa sasa yupo mbioni kumalizia kazi yake mpya iitwayo Samaki Mchangani, anasema kuwa amehamasika mno kutokana na kazi yake ya kwanza kukubalika, ingawa bado kuna dhana ya kwamba sinema fupi hazina soko hapa nchini.



Kwa kweli utengenezaji wa filamu fupi fupi ni njia nzuri sana ya kupata uzoefu kabla mtu hajakimbilia kutengeneza filamu ndefu, hufuata misingi yote, zina soko kubwa mno kimataifa na hazina presha kubwa katika kuziandaa kama hizi ndefu ambazo zinategemea soko lililodhibitiwa na watu wachache.



Soko la filamu fupi limejengwa katika misingi imara, hasa mtengenezaji anapaswa kuipeleka filamu yake kwenye matamasha ya filamu ambako huwa hawaangalii majina ya watu bali wanazingatia misingi na weledi. Kupeleka filamu fupi katika tamasha la filamu kwa ajili ya kuonekana ni jambo zuri sana hasa baada ya kazi ngumu ya kuitengeneza ambapo mtengenezaji hutaraji watu waione.



Matamasha ya filamu yamekuwa ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa, na ukibahatika kuwa mmoja wa washindi wa tuzo, jua itakuwa rahisi kwako kupata pesa (funds) za kutengeneza kitu kikubwa unachohitaji siku zote kwa kuwa utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa, na hapo ndo’ washindi hujua kuwa wapo katika mstari sahihi.



Siku zote soko la filamu fupi limekuwepo na si la ubabaishaji kama hili la hapa kwetu, kwani ukitengeneza kazi nzuri ujue itapata soko tu. Kuna matamasha zaidi ya elfu tano katika sehemu mbalimbali duniani, na idadi huongezeka kila mwaka. Matamasha mengi hutoza malipo ya ada ya kuingia, chochote kuanzia dola 10/ na 50/.



Kabla ya kuingia kwa undani katika kuziangalia sinema fupi, uchunguzi wa tabia ya falsafa unahitajika. Watu wengi wamekuwa wakitumia mamilioni ya pesa kutengeneza filamu ndefu ambazo hata hivyo soko lake bado ni la mashaka makubwa, kwani mtengenezaji hulazimika kwenda kwa msambazaji akiwa mikono nyuma japo ametumia pesa na muda wake mwingi katika kuifanikisha kazi yake hiyo. Na mwisho wa siku anaambulia mikono mitupu au kupewa masharti yasiyomsaidia chochote.



Tusidanganyane, thamani ya filamu nchini inaendelea kushuka siku hadi siku, hii inatokana na wasambazaji wa filamu waliolihodhi soko hili kutozingatia weledi wala misingi na hivyo kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizo na ubora. Pia kukosekana kwa tafiti na kumbukumbu (data) zinazowekwa kutusaidia katika kutambua thamani halisi ya tasnia na soko la filamu nchini imekuwa sababu nyingine kubwa.



Soko ya filamu nchini limejikita katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism) kitu ambacho ni hatari kwa taifa, kwa sababu pia muundo wa soko letu umekuwa ukishusha hadhi ya utamaduni na sanaa zetu huku serikali ikionekana kulala usingizi wa pono.



Umuhimu wa sinema fupi unaonekana sasa hasa kutokana na ile dhana ya filamu kusemwa kuwa hazifanyi vizuri sokoni kinyume na ukweli ulivyo, tatizo ni kutokuwepo uwazi katika biashara kati ya mtayalishaji na msambazaji. Wamekuwa wanadurufu nakala nyingi zinazofurika sokoni wakati huohuo wakidai eti filamu haziuziki.



Kuna matatizo mengi katika soko la filamu nchini, ugumu na makosa yanayofanya utengenezaji wa filamu kuwa wa gharama kubwa zaidi na kutumia muda mwingi kuliko inavyotakiwa kuwa huku mtengenezaji akiwa hajui atakachopata. Katika kutengeneza Filamu Fupi kuna mambo ya kitaalam yanayoweza kusaidia kutengeneza filamu hizi.



Kwanza kabla hujaamua kutengeneza unatakiwa kutafuta hadithi nzuri. Kumbuka, kama mtengenezaji wa filamu unasimulia hadithi, hakikisha kuwa unacho cha kusimulia ambacho jamii mbalimbali zitapenda kukifuatilia. Pia elewa kuwa unatengeneza filamu kwa ajili ya soko la kimataifa – kwa ajili ya watu wanaojali zaidi misingi – hivyo simulia hadithi zetu; za Kiafrika ambazo zitawavutia watu wa mataifa mengine kuzifuatilia.



Kama utatumia muda vizuri ukiisuka script yako kwa kufuata misingi, utengenezaji wa filamu unaweza kuwa rahisi na kwenda vizuri zaidi. Ni rahisi kuhariri stori ikiwa bado katika ukurasa, kuliko kutumia muda mwingi na fedha nyingi kwa kupiga picha vitu ambavyo hutavihitaji baadaye. Na katika utengenezaji wa filamu tunapaswa kuelewa kuwa muda ni fedha. Hivyo tunapaswa kutoa visivyotakiwa kabla ya upigaji picha. Inapendeza pia kuwa na script fupi yenye kueleweka.



Ili kumudu bajeti, jaribu kuwa na eneo (location) moja au mawili ya kupigia picha – huhitaji kuwa na maeneo mengi yasiyoleta tija. Kama huwezi kupata eneo zuri unalohitaji, unaweza kufikiria namna ya kuhariri script yako ili iendane na maeneo uliyopata lakini angalia isiharibu mtiririko wa hadithi.



Katika filamu fupi, huhitaji kuwa na wahusika wengi, kumbuka kuwa kila mhusika na kila tukio lazima viwe na sababu kwenye stori yako, hivyo unapaswa kuwa nao wachache. Jaribu na endelea kuifanya stori yako iwe rahisi na ya kuburudisha zaidi. Kumbuka wazo lako litakusaidia kuonesha kipaji chako na kuonesha namna unavyoweza kuwahadithia wengine kwa kufuatia mtiririko wa kitaaluma: mwanzo, kati na mwisho.



Alamsiki.

No comments: