Jun 16, 2014

HARAKATI ZA TAFF: Serikali, sikieni kilio chetu kwa mustakabali wa Taifa



Katibu Mkuu wa TAFF, Bishop Hiluka, akitoa ufafanuzi katika warsha ya wadau wa sanaa nchini, iliyofanyika kwenye hoteli ya Chichi, Kinondoni B, jijini Dar es Salaam hivi karibuni
 
HEBU jaribu kupata picha: umelima shamba lako na kupanda mahindi ambayo umeyatunza vizuri na yako tayari kuvunwa… unaamka siku moja na kukuta kuna mtu kayavuna na ameanzisha biashara inayompatia fedha nzuri wakati wewe uliyelima huna hata fedha ya kula! Au umenunua suti nzuri akaja mtu akaivaa harusini, kesho yake anakuja kukutaarifu jinsi walivyomsifia harusini kwa kupendeza na suti yako. Hiyo ndio picha ilivyo katika shughuli za sanaa Tanzania. Na haswa katika mambo ya filamu.

Katika mifano hii midogo moja kwa moja unapata picha halisi ya kile kinachoendelea kwenye tasnia ya filamu na hata sanaa zingine hapa nchini, ambayo tunaweza kuiita kuwa ni shamba la bibi, kwani kila anayejisikia anaingia, anavuna tani yake na kufaidi mazao pasipo kulima.

Japo sekta ya filamu ni sekta tajiri sana lakini imekuwa haipewi kipaumbele sana na serikali ingawa Tanzania ni moja ya nchi chache zenye maeneo mazuri ya kuvutia yanayofaa kabisa kwa kutengenezea filamu. Soko la filamu za Tanzania kwa sasa limekua mno hadi kufikia nchi zaidi ya nane ikiwa ni pamoja na Tanzania yenyewe, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo DRC, Malawi, Zambia, na Msumbiji, hivyo kufanya idadi ya watazamaji kuwa zaidi ya milioni 180.

Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), mnamo mwezi Februari lilishawasilisha mapendekezo ya tafiti ya Sera ya filamu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo baada ya kubaini kuwepo kwa mapungufu maakubwa katika mfumo uliopo sasa wa sekta hii, na kama hiyo haitoshi, viongozi wake walikwenda mjini Dodoma wakati Wizara ya habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ikisoma bajeti yake ya mwaka 2014/15, tarehe 29 Mei 2014 kufanya ushawishi kwa wabunge ili angalau Serikali isikie kilio chao.

Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba aliiambia safu hii ya ‘Mbiu ya Ijumaa’ kuwa TAFF inapigania kuondoa kasumba iliyojengeka ya kuendelea kuitambua sekta ya sanaa (copyright-based industries) kama ni sehemu ya utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential) jambo linaloifanya serikali ikose mapato.

TAFF inasimamia miradi miwili (Sera ya Filamu na Sera ya Miliki Bunifu) ambayo imefadhiliwa na Taasisi ya Best-AC, ili kuhakikisha sekta ya filamu inapata sera yake kama mwongozo, na pia kuhakikisha ulinzi wa kazi za sanaa kupitia Sera ya Miliki Bunifu. Wiki iliyopita TAFF kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanamuziki (Tamunet) waliandaa warsha ya wadau wa sanaa kwa ajili ya kukusanya maoni yatakayowasilishwa Wizara ya Viwanda na Biashara ili tuwe na Sera ya Miliki Bunifu.

Hata hivyo, imebainika kuwa kutokuwepo kwa sera ya filamu (au sanaa kwa ujumla) ambayo ndiyo muongozo, serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imekuwa haiyapi kipaumbele Mashirikisho ya Sanaa yaliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na 23. ya 1984 iliyounda Baraza la Sanaa la Taifa. Kwa kweli mashirikisho haya yamenyimwa mamlaka na uwezo (kwa makusudi) ya kuwa vyombo vya juu vya wadau vya kusimamia masuala ya sanaa, jambo ambalo limekuwa likisababisha kupotea kwa mapato, kupungua kwa maadili, na kuongezeka kwa skendo miongoni mwa wasanii.

Inaonesha wazi kuwa huenda watendaji serikalini waliopewa dhamana ama hawajitambui au wameamua makusudi kutoipa kipaumbele sekta hii, kwani Sera ni muhimu sana kwani ndiyo mfumo wa kuwatambua wanaoendesha sekta ya filamu, husaidia kuandaa mazingira mazuri ya uzalishaji wa filamu, na husaidia uandaaji wa takwimu za kina. Sera pia huangalia mazingira na ubora wa elimu inayohitajika, na huangalia masoko.

Kila mara tumekuwa tukijaribu kujilinganisha na Nigeria lakini tunasahau kuwa mafanikio ya Nigeria katika sekta ya filamu yalitokana na uwepo wa sera ya filamu iliyopatikana mwaka 1991 wakati Shirika la Filamu la Nigeria (NFC) lilipoandaa jopo kuangalia kanuni zilizokuwepo kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera ya filamu. Nigeria kwa sasa ndiyo Taifa lenye uchumi mkubwa barani Afrika ikiwa na Pato Ghafi la Ndani (Gross Domestic Product ‘GDP’) la Dola Billion 509.

Nollywood ndiyo sekta ya pili kwa kutoa ajira katika nchi ya Nigeria baada ya sekta ya kilimo, na mchango wake kwa Taifa ni mkubwa sana kwani ina thamani ya Naira bilioni 853.9 (Dola za Marekani bilioni 5.1). Hii ni ishara ya jinsi gani sekta ya filamu inavyoweza kukuza na kubadili uchumi wa nchi yoyote, kwa njia ya utoaji wa ajira kama itachukuliwa kwa umakini mkubwa.

Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Nigeria, Nigeria imekuwa Taifa lenye uchumi mkubwa Afrika baada ya wanauchumi wa nchi hiyo kuziongeza sekta za Mawasiliano na Filamu (Nollywood) kwenye takwimu. Ni dhahiri kuwa soko la Filamu la Nigeria linatoa mchango mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Nigeria ilionekana kama taifa linalotegemea zaidi uuzaji wa mafuta na ilikadiriwa kuwa pato la mafuta lilichangia asilimia 32 kwenye GDP lakini ripoti ya wanauchumi ya hivi karibuni imeonesha sasa pato la mafuta huchangia asilimia 15 tu ya pato ghafi la ndani.

Katika kuhakikisha kazi za sanaa linawafaidisha wasanii na kuleta tija kwa taifa, Rais wa TAFF, Mwakifwamba, aliiambia ‘Mbiu ya Ijumaa’ kuwa TAFF kwa kushirikiana na Tamunet wameshafanya mikutano kadhaa ya wadau wa sanaa na kukusanya maoni ambayo watayawasilisha Wizara ya Viwanda na Biashara, ambapo Sera ya Miliki Bunifu inaandaliwa.

Hii ilikuwa ni baada ya safari ya Dodoma walikofanya ushawishi mkubwa kwa Wajumbe wa Bunge la Katiba ili kuwashawishi kuingiza vipengele kulitambua kundi la wasanii katika Katiba mpya kuwa ni kundi rasmi kutokana na ukubwa wa kundi hili nchini, kama yalivyotajwa makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na kadhalika, ambalo mchango wake katika ajira ya vijana ni mkubwa na pato linalotokana na kundi hili ni kubwa, na pia ubunifu ulindwe kwa ulinzi wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uweko kama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine.

Kwenye Rasimu ya Katiba imetajwa ulinzi wa kazi zinazohamishika na zisizohamishika lakini mali zisizoshikika (zinazotokana na ubunifu) hazikutajwa.

Katika changamoto zote zinazoendelea kwenye tasnia ya sanaa hapa nchini, Serikali haiwezi kukwepa lawama kwa kuwa ndiyo yenye mchango mkubwa wa kuhakikisha marekebisho ya sheria za filamu ya 1976 iliyopitwa na wakati, na sheria hakimiliki na hakishiriki kwa wasanii wa Tanzania ya mwaka 1992 ambayo imekosa meno ya kuwanasa wezi wa sanaa inapitiwa upya na kuboreshwa, kisha kuhakikisha watendaji waliopewa dhamana wanaisimamia ipasavyo na adhabu kali inatolewa kwa watakaokiuka.

Haiwezekani katika kila nyanja ya burudani Tanzania tukaendelea kuwa wa mwisho siku zote, tumeshindwa kwenye kandanda, riadha na michezo mingine mingi, hata kwenye sanaa wakati tuna rasilimali na vijana wenye vipaji lukuki? Ni wakati sasa tukaanza kusaka maendeleo ya sanaa, jambo litakalotuweka pia katika mfumo bora wa soko la pamoja la Afrika Mashariki badala ya sasa tunapoonekana tumelala usingizi wa ‘pono’ pasipo kujipanga vilivyo kwa maendeleo yanayopigiwa kelele.

Naomba kuwasilisha.

No comments: