Marehemu Said Ngamba maaruf kwa jina la Mzee Small
KWANZA
naomba nianze kwa kutoa pole kwa familia nzima ya
wasanii na wadau wa filamu nchini kufuatia vifo mfululizo vya wasanii
wa filamu ndani ya wiki tatu; Adam Kuambiana, Rachel Haule, George Otieno “Tyson)
na Said Ngamba maarufu kama Mzee
Small. Mfululizo wa vifo hivi umeambatana na uvumi au dhana potofu inayosambaa
kwa kasi, eti vifo mfululizo vya wasanii vinatokana na kafara inayofanywa na
baadhi ya wadau (wasanii) ndani ya tasnia ya filamu kwa lengo fulani lenye
maslahi kwao.
Uvumi huu
umejitokeza hasa baada ya kushuhudia kundi la watu fulani likiwa ndiyo kinara
wa kukumbatia misiba ya wasanii nyota, kuunda kamati mbalimbali na kuchangisha
fedha nyingi ambazo baadhi yake zimekuwa zikitumika kununulia majeneza ya bei
mbaya, vyakula vya gharama (utadhani kuna sherehe) na shughuli zingine ikiwemo
ukodishaji wa magari ya kusindikiza msafara wakati wa mazishi. Lakini kama hiyo
haitoshi, kumeripotiwa pia kufanyika kwa ubadhirifu wa pesa.
Sekta ya filamu
nchini ni sekta kubwa sana, yenye nguvu kubwa na ushawishi mkubwa mno, lakini
ndiyo sekta isiyopewa kipaumbele kama sekta muhimu (kwa kuwa inachukuliwa kama
utamaduni na burudani na si biashara) inayoweza kuchangia pato kubwa kwa
maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Ikumbukwe
kuwa kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa
wadau wengine wa sanaa wameendelea kutoa sinema hapa Tanzania ili kujipatia
riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio. Ingawaje sekta ya filamu ni sekta
yenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wengi wameishi na kufa maskini.
Hali hii ya
umasikini kwa wasanii nchini itaendelea kuwa hivi kama wasanii wenyewe
hawataonesha mshikamano na kupigania maslahi yao kwa kuwa kuwategemea wanasiasa
itakuwa ni ndoto ya alinacha kwani wamekuwa wakiahidi sana hasa katika kipindi
cha uchaguzi, lakini wakishapata huwapa visogo. Haki za wasanii na
watayarishaji wa filamu zitaendelea kuporwa, kwa kutumia unyonge wao na
umasikini wao wataendelea kutumika kwa maslahi ya wachache, na mwishowe watakufa
wakiwa masikini lakini wenye majina makubwa, tena bila hata kuwaachia
wategemezi wao urithi unaoeleweka.
Nimekuwa
nikiandika sana kuhusu suala hili, na niliwahi kuwaandikia Rais Kikwete na
Waziri mwenye dhamana wakati fulani kuwataka waiokoe tasnia hii kwa serikali kuelekeza
nguvu nyingi katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wasanii na watengeneza
filamu. Lakini baada ya kuona kuwa sekta ya filamu si moja ya vipaumbele vya
serikali nikawahimiza wasanii kupigania uwepo wa sera ya filamu (kama
mwongozo).
Kama nchi, tunahitaji
sekta hii ichukuliwe kama sekta nyeti sana kupitia kamati za mipango, na Bunge
la Jamhuri. Tunahitaji Rais, Mawaziri, Wabunge, na Wakuu wa Idara ambao
hawataishia tu kusifia kazi zetu kwenye hotuba zao, kuuza sura kwenye misiba
yetu tunapokufa na kutoa ahadi ambazo wanajua kabisa hawawezi kuzitekeleza.
Bado naamini
kuwa Serikali kama kweli wameazimia kwa dhati kusaidia tasnia ya filamu, inapaswa
kuandaa mwongozo (roadmap) utakaotuongoza kwenye mafanikio ya soko letu. Tunahitaji
kuwa na vyombo madhubuti katika kusimamia kazi zetu.
Inashangaza
sana kuona kwenye nchi za wenzetu jinsi wasanii wanavyoweza kutengeneza pesa nyingi
hata pale msanii anapokuwa amefariki dunia, hii ni kutokana na nchi hizo kuwa na
sera nzuri na sheria nzuri za miliki bunifu na hakimiliki, huku serikali ikiithamini
sekta ya filamu na kuwasimamia watu wake na viongozi kutimiza wajibu wao
ipasavyo.
Chukuliwa
wasanii kama Kurt Cobain, Elvis Presley, Charles M. Schulz, John Lennon, Albert
Einstein, Andy Warhol, Dr. Seuss (Theodor Geisel), Ray Charles, Marilyn Monroe,
Johnny Cash, J.R.R. Tolkien, George Harrison, Bob Marley, Michael Jackson,
Whitney Huston na wengine wengi, ambao wamekuwa wakivuna mapesa hata baada ya
vifo vyao na hivyo kuwafanya wategemezi wao kuendelea kujipatia pesa kupitia
kazi zilizoachwa na wapendwa wao.
Hapa kwetu,
chukulia mfano wa aliyekuwa msanii nguli, Steven Kanumba, hadi mauti yanamfika alishatoa
zaidi ya filamu 40, je, sinema zake zimeisaidiaje familia yake iliyobaki? Hadi
leo wategemezi wake, akiwemo mama yake “wanalia njaa” huku tukiambiwa kuwa kazi
alizoacha kanumba zinaendelea kufanya vizuri sokoni.
Naamini kwa
mtu aliyefanya kazi nzuri, kufariki siyo mwisho. Anaweza kuendelea kuishi hata
baada ya kifo, kwani kazi zake, pamoja na nembo zake zinaweza kuendelea kuvuna
mashabiki ambao wanamkumbuka, na wale waliozaliwa muda mrefu baada ya kufa, na
kuingiza mapesa kibao kama inavyotokea kwa mastaa niliowataja hapo juu.
Wasanii katika
nchi za wenzetu waliofariki miaka mingi sana iliyopita wameendelea kuchuma mamilioni
ya dola. Wameendelea kukusanya fedha katika mikataba mbalimbali waliyoingia
enzi za uhai wao ikishirikisha vyote; kazi zao na haki za kutumia majina yao kibiashara
na kampeni za masoko.
Vipi kuhusu wasanii
wa Tanzania? Wana mpango gani kuhakikisha yanawekwa mazingira mazuri
yatakayowahakikishia wategemezi wao baada ya vifo vyao? Wanatumiaje nguvu ya
sekta ya filamu kuibana Serikali ili iweke mipango na mazingira mazuri
yatakayowahakikisha wasanii waliopo na waliofariki kuendelea kuvuna pesa na
kuzifaidisha familia zao na wategemezi wao waliobakia? Au ndo’ ule msemo wetu
wa ‘Asiyekuwepo na lake halipo?’.
Watengezaji
wa filamu nchini wamekuwa wanalalamika kila mara kuwa wanaibiwa au kuwekewa
masharti magumu na wasambazaji ambayo yanadumaza tasnia ya filamu ikiwemo kuuza
haki zao, lakini wamekuwa wakionekana wendawazimu.
Kwa sasa
imekuwa ni jambo la kawaida kusikia kuwa mtayarishaji wa filamu kauza kazi zake
kwa msambazaji, jambo linaloshangaza sana hasa kwa nchi kama hii inayoanza
kupiga hatua katika tasnia ya filamu. Sababu za kushangaza ni nyingi; ya kwanza
kubwa ni kuwa majukumu ya msambazaji yanajulikana wazi kuwa yeye kazi yake
inapaswa kuishia kwenye kusambaza kazi husika tu, sasa anaponunua haki zote
ndipo inapotia shaka kubwa! Kwa nini anunue haki ya msanii? Kwa nini msanii amuuzie
haki yake? Je, wasanii wanalitafakari jambo hili?
Hakuna jambo
kubwa kama kujifunza kwa waliotutangulia, hasa kwa kuangalia makosa
waliyoyafanya ili sisi tusije tukayarudia. Mfano marehemu Kanumba alikuwa mmoja
wa wasanii waliojiona ni washindi kwa kuingia mikataba inayowafanya kuuza haki
zao kwa msambazaji na kuishia kupewa gari na pesa zinazowasaidia kwa miezi
michache, masikini hakujua kabisa kuwa atakapoaga dunia haki yake itakuwa imeishia
hapohapo. Hivyo, hawa waliobaki wanapaswa kujifunza kupitia wasanii kama
Kanumba na wengine walioaga dunia.
Sheria ya
Hakimiliki ya nchi yetu inasema wazi kuwa hakimiliki hudumu kwa mwenye haki kwa
maisha yake yote na miaka hamsini baada ya kifo chake. Kwa nchi kama Marekani
wameongeza hadi miaka sabini. Ndiyo maana utaona kuwa kuna kazi nyingi ambazo
zinaendelea kuwa maarufu miaka mingi baada ya wenye kazi kufariki, huku
zikiwanufaisha warithi wao.
Kwa kawaida
kazi za filamu (kama ilivyo kwenye muziki) zina haki zipatazo kumi ambazo
zimetajwa katika kifungu na 9(1) cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya
1999.
Haki hizo
ni: (i) Kurudufu kazi, (ii) Kusambaza kazi, (iii) Kukodisha, (iv) Kuonesha
hadharani, (v) Kutafsiri, (vi) Kubadili matumizi ya kazi, (vii) Kufanya
maonesho ya hadhara, (viii) Kutangaza kazi katika vyombo vya utangazaji, (ix)
Kutangaza kwa njia nyingine zozote, na (x) Kuingiza kazi nchini.
Kwa hiyo
ukiangalia haki hizo kama zilivyoainishwa utaona wazi kuwa msambazaji anahitaji
haki mbili tu za mwanzo, haki nyingine zinamruhusu mwenye mali (mtayarishaji)
aendelee kufaidi matunda ya kazi yake kwa maisha yake yote na kuwaachia warithi
wake miaka hamsini mingine baada ya kifo chake.
Inapotokea ukauza
haki zako kwa msambazaji basi ujue unauza hata zile haki nane zilizobakia
ambazo kimsingi huwezi tena kuzitumia, kwa kuwa tayari utakuwa umeshazipoteza.
Hivi ukiamua kuuza kazi zako kwa maana ya kumuachia haki zote msambazaji,
unatarajia kuwaachia nini warithi wako, au unataka kubaki na ile sifa tu ya
kuwa uliwahi kuwa na kazi?
Hivyo,
badala ya kuanza kutafuta mchawi kwa vifo vya wenzao, nadhani wasanii
wangetumia nafasi hii kujitafakari upya hasa katika kupigania umoja wenye nguvu
kwa ajili ya maslahi yao, ya sasa na ya baadaye, hasa baada ya kifo.
Alamsiki.
1 comment:
HAKIKA NDUGU UMESEMA NI JAMBO MUHIMU WASANI WAJIPANGE NA HATA KUANZISHA COMPANY YA USAMBAZAJI BADALA YA KUTUMIA PESA ZAO KWENYE MAMBO YASIYO NA MAANA KAMA HARUSI MILION 70 HII FAIDA GANI NI MUHIMU KUANZISHA COMPANY YA USAMBAZAJI WENYEWE MAANA WANA SIASA WOTE DUNIANI HUANGALIA MASLHAI YAO NASIYO VINGINEVYO
Post a Comment