MICHEZO ni chombo cha kuwasilisha tunu
msingi katika kuboresha ubinadamu na katika ujenzi wa jamii ya amani na ya
kindugu.
Michezo ina faida kubwa sana kwa
mwanadamu, siyo kwa wachezaji tu bali hata kwa wanaoshabikia ambao kufurahi
kwao huwa ni kinga dhidi ya maradhi, hasa inapokuwa michezo ya ushindani.
Ni wazi kuwa matatizo mengi ya kiafya kwa
wanadamu yanaongezeka siku hizi kutoka na mfumo mpya wa maisha tunayoishi
ukilinganisha na miaka ya nyuma. Ingawa kwa wale wanaoshiriki michezo
mbalimbali mara nyingi imewasaidia kuepuka matatizo hayo.
Miongoni mwa wanamichezo siyo rahisi
kupata magonjwa ya kisukari, shinikizo la juu la damu n.k., na pia hujengeka
katika hali ya afya njema ya viungo mbalimbali vya mwili, afya ya akili
huimarika, ambapo yote hayo husababisha kuwa na jamii ya watu wenye afya na
furaha.
Michezo pia imesaidia watu kufahamiana,
kuwaepusha (hasa watoto na vijana) wanaoshiriki katika michezo mbalimbali
katika shule za msingi, za sekondari na hata vyuo vikuu, kutojihusisha kwa
wingi katika matumizi ya dawa za kulevya, pombe, sigara na vitendo vya ngono
ikilinganishwa na wale ambao hawajihusishi au kushiri katika michezo
mbalimbali.
Kwa kauli hiyo tunapata wazo kuu juu ya
michezo kwa ujumla ya kwamba michezo imekuwa na lengo kuu msingi tangu zamani
za kale la kujenga undugu na amani.
Kama mchezo ni chombo cha kuwasilisha
tunu ya binadamu mwenyewe, kujieleza mwenyewe, kukubalika mwenyewe na
kujikubali, inamaana kwamba nchi yoyote haiwezakani kutambulika na utaifa wake
bila kuwa na utamaduni wao, na mojawapo ya viungo vya tamaduni hiyo
vinavyounganisha katika duniani hii ni michezo.
Mfano, kuna baadhi ya mataifa ambayo
wameweza kujitambulisha kwa mavazi, na ishara mbalimbali kiasi kwamba ukiona
vazi fulani tayari unajua ni kutoka nchi fulani.
Hivyo basi, michezo ni chommbo muhimu
sana katika kuendeleza jamiii. Aidha, michezo huweza kuwa kielelezo kikubwa na
utambulisho wa taifa katika kutoa burudani, kujenga nidhamu, kujitangaza kiuwezo
na kukomaza afya, ya mwili na akili.
Mara ngapi nchi majirani zetu wameonekana
kujivunia vipaji vya wachezaji wao kila wanaposhiriki michezo ya kitaifa na
kimataifa?
Mifano ipo mingi, mfano wa karibu zaidi
katika Michezo ya Jumuiya ya Madoa inayotarajia kumalizika kesho Jumapili huko
Gold Coast, Australia, tunasikia ni jinsi gani wanamichezo wan chi jirani
wameng’aa wakati wanamichezo wetu wamebung’aa.
Pia tumekuwa tukisikia jinsi wachezaji wa
mipira wanahama kutoka timu moja hadi nyingine mara baada ya kombe la dunia,
maana sasa hivi wako katika soko.
Kutokana na umuhimu wa michezo katika
jamii kila kipindi cha kihistoria, binadamu amekuwa akishiriki michezo katika
tamaduni, mila na sanaa, tunajua michezo ya mila na desturi tangu zamani
imekuwepo; mieleka, kuruka, kukimbia kulenga shaba ya mishale, kuogelea nk.
Ni michezo iliyokuwa inalenga kujiamini
na kuwa na utambulisho wa kila jamii ambayo iliitwa ya jadi, hata ndugu zetu
waliopelekwa kwenye utumwa na kukutana na watu wa mataifa mbalimbali walieneza
jadi zao katika michezo hiyo, iliyowasaidia sana kukabiliana na matatizo
yaliyokuwa yanawakumba katika utumwa huo.
Lakini baada ya michezo ya kisasa kuingia
kama mipira ya miguu, mipira ya meza, ndondi, mbio, baiskeli, magari ya
mashindano, mashindano ya farasi na michezo mingine mingi historia ya jadi
ikalegeza thamani yake, na kuanza kutawaliwa kwanza fedha na ushindani.
Hatuwezi kusahau kwamba michezo ya jadi
kwanza ilikuwa inalenga undugu zaidi, urafiki zaidi, burudani zaidi, katika
kushirikiana kwa pamoja na kuishi kwa amani.
Leo hii katika viwanja mbalimbali vya
mipira, kuna uwoga wa kurudi salama au kutokurudi salama, ni hatari kubwa.
Karne ya leo inazo changamoto nyingi
ambazo zimejitokeza kwenye michezo kama vile, kinachotangulia ni fedha, na
ushindani, au kuwepo na dharau, kutaka kushinda kwa kila njia, wakati mwingine
hata watu wanaofanya michezo hiyo kupenda kutumia hata dawa za kujiharibu mwili
hili wawe na guvu za kushinda.
Hata hivyo, changamoto ni nyingi kwani
mabadiliko ya jamii yetu wazazi wengi kutowafundisha watoto umuhimu wa michezo
ni nini, kwa sababu watoto walio wengi ukisema mchezo kitu cha kwanza kichwani
ni kufikiria kushinda kabla ya burudani na furaha ya kushiriki na wengine.
Ndiyo maana utakuta watoto wengine
hawapendi kushiriki michezo kama ngoma au muziki wakisema mimi siwezi maana
mwenzangu ndiyo aliye na uwezo.
Watoto walio wengi wanapokwenda kwenye
michezo tayari wana wazo kuwa lazima washinde tu, na kumbe uwajibikaji wa jamii
zetu kuanzia katika familia muhimu sana kuwafundisha tangu utoto umuhimu wa
michezo ya pamoja kwanza ni kufurahi, kunyoosha viuongo kwa ajili ya kutunza
afya bora na siyo tu kushinda na kupokea zawadi.
Ili tupige hatua, michezo ifundishwe kwa
watoto wetu na iboreshwe katika tamaduni zetu, ili iweze kutuunganisha badala
ya kututenganisha, iboreshe utu kwanza kuliko kujali mali, ndipo tutajenga
jamii ya utu wa kweli na yenye kupendana kama ndugu. Baada ya hapo tutaweza kupiga
hatua kimichezo kama taifa.
No comments:
Post a Comment