Wakati
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) ikizidi kuimarika na kuchukua
nafasi ya njia kongwe za mawasiliano, tasnia ya ubunifu nayo inajikuta kwenye
changamoto ya kuakisi mabadiliko hayo ya wakati.
Tasnia ya ubunifu (Sanaa)
ni hazina muhimu sana inayohifadhi kazi ya uumbaji; ambapo wabunifu (wasanii)
wanayo dhamana ya kueneza ujumbe na elimu kwa jamii.
Tasnia hii ni
mjumuiko wa hakimiliki bunifu ambazo zinapaswa kulindwa ili jamii iendelee
kunufaika na kazi hizi za ubunifu, ambazo sasa zimeenea duniani kote.
Sifa kuu maalumu ya sanaa ni kwamba inatoa athari
zake kwa mbunifu na mtazamaji/msikilizaji, hata kama katika mambo mengi mbunifu
hatalizingatia hilo, na ijapokuwa katika aghlabu ya wakati,
mtazamaji/msikilizaji hatalihisi hilo.
Kwa mfano, athari za tungo za kishairi, filamu,
michoro na aina nyingine za sanaa, sauti ya kuvutia na muziki mzuri – ambapo
yote hayo ni katika sanaa – huziathiri nyoyo za wanaofuatilia au kusikiliza
bila wenyewe kujua.
Sanaa si kama utajiri ambao unapatikana mara moja
kwa kutoka kijasho cha uso na girisi mikononi. Madhali mtu hana kipaji cha
sanaa, hata akijitahidi vipi bado ataendelea kubakia katika asili yake ile ile
ya kimaumbile.
Pia kipaji cha kisanii si kitu ambacho mtu anaweza
kukichuma kama utajiri bali huwa ni kipawa maalumu anachotunukiwa msanii na
Mungu.
Mungu ndiye humpa mwanaadamu neema zote hata kama
njia ya kumfikia neema hizo huwa ni kupitia jamii, baba, mama, mazingira
anayoishi na vitu vingine kama hivyo.
Vivyo hivyo, msanii hufanya juhudi zake, lakini
hiyo fursa na hima ya kufanya juhudi nayo hupewa na Mungu. Msanii anapaswa
kufanya juhudi za kukuza kipaji chake cha usanii ndani ya nafsi yake.
Kila msanii peke yake ni kama dunia nzima na sifa
hiyo maalumu ya msanii imo ndani ya nafsi yake. Na kama mtu angelipata fursa ya
kudiriki dhati ya wasanii angeliweza kuona shani za dunia na maajabu yake.
Ndani ya dunia iliyojaa furaha na majonzi,
matumaini na wasiwasi ndani yake, ni sanaa pekee yenye uwezo wa kutibu majeraha
na hata kuifanya jamii iwe na furaha.
Si hivyo tu, kwa
sasa tasnia ya ubunifu ina nguvu sana duniani, hasa filamu na muziki, na
imeenea duniani kote na kusaidia katika ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.
Hata hivyo, japo tasnia
hii inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na kuingia katika zama za
dijitali (teknolojia) lakini pia imeanza kukumbana na changamoto kubwa na
mkwamo.
Kwa upande mmoja,
maendeleo ya haraka ya teknolojia yameiletea sekta hii fursa nzuri ya
kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina ya uenezi wa sanaa hizi zimekuwa
nyingi, kwa mfano televisheni za kwenye mitandao ya intaneti (online tv); simu
za mkononi n.k., zimeingia kwenye soko la televisheni na imekuwa shinikizo
kubwa kwa sekta ya ubunifu.
Lakini hiyo
ingeweza kuwa habari njema kama teknolojia hii isingekuwa inatumika vibaya
kurahisisha ukwapuaji wa kazi hizo adhimu. Ukuaji wa teknolojia
umefanya maharamia wa kazi za sanaa kukwapua kwa urahisi kazi za sana na hivyo
kuzidi kuwafukarisha wasanii.
Utakuta
watu wanapakua filamu na miziki kwenye mitandao, kurudufu na hata kutembea nazo
kwenye flashi diski, huku wasanii wakibaki fukara! Kwa kweli hii si haki, hasa
ikizingatiwa kuwa Mungu ametoa neema ya kipawa kwa msanii ili aweze kuishi kwa
kutumia kipawa chake.
Ukitazama hali ya wasanii wenyewe katika upande wa
maisha yao kwa kweli si nzuri sana (japo wanaishi maisha ya kuigiza), na mara
nyingi hata huwa si nzuri kabisa.
Hata watu ambao wanawekeza katika masuala ya sanaa
huwa mara nyingi wanashindwa hata kurudisha fedha walizowekeza.
Ni vyema tukatambua hali zao kuwa wanahitaji sapoti
ili waendelee kueneza ujumbe na elimu kwa jamii, utakapotizama filamu au
kusikiliza muziki, wakati mwingine fikiria wabunifu wote walioandaa filamu hiyo
na kumbuka kuna hakimiliki inayowawezesha kupata kipato chao.
Na
pili fikiria changamoto za teknolojia, kwa kuwa huu ni wajibu wa kila mtu na
wala siyo wa watunga sera pekee.
Ni
vipi tunaweza kutumia fursa hii ya kipekee ya intaneti ya kueneza utamaduni na
wakati huo huo kuhakikisha wabunifu wanaendelea kubuni na wanapata kipato chao
kwa kuandaa filamu na video zinazoboresha maisha yetu?
Kwa kweli inabidi kuwasaidia wasanii na kama
hawakusaidiwa wanaweza kuamua kufanya jambo lolote lile litakaloweza kuwadhaminia
fedha za kuweza kuendelezea kazi zao.
Ndiyo maana mara nyingi tumeshuhudia wakitumika katika
biashara haramu kama ya dawa za kulevya. Wasiwasi wangu tu wasije wakatokea
watu wasioitakia mema nchi yetu na kuwatumia kuleta machafuko, kueneza fikra za
maingiliano haramu ya kijinsia na mambo kama hayo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Sanaa la Taifa
ya mwaka 2006, nchini Tanzania kulikuwa na wasanii milioni 6, ingawa kwa
vyovyote watakuwa wameongezeka kwani imekwishapita miaka kumi na mbili na hata teknolojia
imekua.
Sanaa ni biashara kubwa ambayo ripoti ya Shirika
la Hakimiliki la Kidunia (WIPO) ya mwaka 2012 inaonesha kuwa mchango wa mapato
uliotokana na shughuli za Hakimiliki ulikuwa zaidi ya mchango wa Sekta ya
Madini.
Pia mchango wa ajira katika kazi zilizotokana na
Hakimiliki ulikuwa ni zaidi ya madini, umeme, gesi, maji, usafirishaji,
mawasiliano, ujenzi, afya, na ustawi wa jamii. Pia wasanii ndiyo wamekuwa
wakilipa jina na utambulisho Taifa hili.
Pia kwa mujibu wa utafiti wa WIPO wa Septemba 2012, sekta ya sanaa inachangia kwenye pato la Taifa asilimia 4.275. Hivyo, ni vema tukahakikisha teknolojia haitumiki kukwapua haki za wasanii, kwa mustakabali wa taifa na jamii yetu.
No comments:
Post a Comment