Wanamuziki Nandy na Bill Nass katika pozi |
KAMA mtafiti, mchambuzi, mdau wa sanaa na
mwananchi wa nchi hii nimekuwa nikiitahadharisha jamii yangu kuhusu vita
vinavyoendelea duniani kati ya mataifa makubwa na mataifa machanga.
Lakini hivi si vita kama vile vinavyoendelea huko
Syria, wala si vita vya kupinga ugaidi n.k. la hasha! Bali ni vita vya kiutamaduni, vya
kutawalana kiakili.
Vita vya utamaduni huenezwa kupitia vyombo vya
habari ikiwemo mitandao, televisheni, redio, magazeti, sinema, muziki n.k. ambavyo
ni jukwaa muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi
husika.
Mataifa
kama ya India, China n.k. siyo wajinga kuruhusu tamthilia na filamu zao
zitafsiriwe Kiswahili (tena kwa gharama zao) na kurushwa bure kwenye vyombo
vyetu vya habari. Ni kwa sababu wanajua kuwa dunia sasa ipo kwenye vita ya
utamaduni, vya kutawalana kiakili.
Katika
kipindi cha wiki mbili wasanii wa muziki wametawala kwenye ‘headlines’ nzito za
vyombo vyetu vya habari baada ya kuvuja kwa video zao mtandaoni zinazoelezewa
kuwa zinadhalilisha utu wao na wa watu wengine.
Wiki iliyopita video ya utupu ya mwanamuziki nyota
wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu kama Nandy, ilisambaa kwenye mitandao
ya kijamii ikimuonesha akiwa na mwanamuziki wa kiume, Bill Nass,
wakiwa kwenye nguo yake ya ndani sambamba na mwenza wake kitandani.
Inasemwa kuwa video hiyo ya utupu iliaza kusambaa mtandaoni siku moja
baada ya Nandy kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Bill Nass na kuachia picha hizo
ambazo hazikuwahi kuonekana hapo awali zikiwaonesha wakiwa karibu zaidi.
Kama hilo halitoshi, wiki hii mwanamziki mwingine
maarufu wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul maarufu kama Diamond Platnumz ameingia
matatani baada ya video zilizosambaa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya
kijamii zikimuonesha akiwa kitandani akicheza na mzazi mwenzake, Hamisa Mobetto,
pia na mwanamke mwingine ambaye hajajulikana, zinazoelezwa kuwa hazina maadili.
Awali serikali ilitaja changamoto kubwa
inayolikabili taifa kuwa ni athari ya utamaduni wa nje katika maadili, mila na
desturi za Mtanzania kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu duniani.
Hili la wasanii kujitokeza hadharani (mitandaoni) wakiwa
nusu watupu linaendeleza kile ambacho nimekuwa nasisitiza kuwa ‘wasanii ni kioo
cha jamii’ japo baadhi ya watu wanadhani kuwa kwa sasa wamekuwa si kioo cha
jamii tena.
Maneno ‘wasanii ni kioo cha jamii’ yanayotokana na
tafsiri ya maneno ya Kiingereza ‘Artists are the mirror of the society’, usemi
uliozoeleka sana katika vyombo vya habari na hata baina ya wasanii wenyewe, na
ninaamini kuwa msanii asiyeitafsiri jamii yake hujikuta yuko peke yake akiwa
hana wapenzi wala washabiki.
Naamini siku zote wasanii wataendelea kuwa ‘kioo
cha jamii’ na haya yote yanayoendelea katika vyombo vya habari, kwenye miziki, filamu
na hata kwenye video za muziki yanaonesha zao halisi la jamii yetu ilivyo kwa
sasa.
Kitendo chochote cha kuukana ukweli na kuwatupia
lawama wasanii peke yao huku tukiwabeza kwa maneno haya na yale ni sawa na
kukataa kutumia kioo jambo ambalo si njia ya kubadili ubaya wa sura zetu.
Naamini kuwa tatizo tulilonalo hapa si wasanii
kupiga picha chafu wala kazi zao, kwani wao ni sehemu tu ya jamii hii, tatizo
lililopo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima, kwa kuwa tumeruhusu
utamaduni wa nje uingie na kutawala maisha yetu, kwa kisingizio cha utandawazi.
Tumeshafika hatua ya wasanii wengine kuamini kuwa
jamii haina tatizo na jambo hilo kiasi cha mtu kukaa mtupu katika jukwaa wakati
akiangaliwa na maelfu ya watu, na kwa vile teknolojia imekua, wanapokaa katika
hali ya utupu ni sawa na kukaa utupu kwenye macho ya ulimwengu mzima!
Hivi tunaandaa taifa lijalo (kizazi) la aina gani?
Kwa mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani wa utamaduni? Tuamke
sasa, tusipojipanga basi dunia itatupanga, kwani huu ni mkakati maalumu wa kujenga
jamii itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje, na hivyo
kutawaliwa kiakili.
Tusipojipanga
tutajikuta tunaishia kujenga jamii ya watu waliochanganyikiwa. Tunaweza
tusilione sasa ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na
mustakabali wa nchi yetu.
Inashangaza
pale tunapowafungia wasanii wetu kwa kurusha video zisizo na maadili lakini
tunaruhusu vichupi kwenye video za miziki zinazotoka nje kuoneshwa kwenye vituo
vyetu vya televisheni. Utalindaje maadili kwa kuzuia picha za ndani wakati unarusha
video za nje zenye vichupi?
Ukiangalia
kwa makini, utagundua hata mfumo wa utangazaji katika baadhi ya vituo vya Redio
na Televisheni umeigwa kutoka Magharibi, kitu kinachotoa taswira ya kuua suala
la ubunifu na kubaki watupu tusio na kitu chochote.
Bahati
mbaya sana katika dunia hii ya vita vya utamaduni, ukitaka kupata fedha nyingi
kwa urahisi basi fanya jambo linalodhalilisha utamaduni wako au taifa lako na kutukuza
utamaduni wa mataifa ya Magharibi.
Haya
yanayoendelea sasa ya kina Nandy, Bill Nass. Diamond na wengineo ni ‘alamu’ kuwa tusipojipanga basi vita vya
kiutamaduni havitatuacha salama.
Kutoa wito kwa wasanii kuwa mitandao siyo kokoro
la kupeleka uchafu, bila kuweka mikakati thabiti ya kulinda kizazi hiki dhidi
ya utandawazi haitatusaidia.
Ni kweli sasa tunayo Sheria ya makosa ya mtandao
ya mwaka 2015 iliyotungwa ili kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao, kama
inavyoainishwa katika kifungu cha 14.-(1) (a) na (b) lakini tusipojipanga dunia
itatupanga.
No comments:
Post a Comment