Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel, akikata utepe kuzindua Tamthilia ya 'Doudou na Wakwe Zake' katika Viwanja vya TBC mwaka 2014 |
SEKTA ya Televisheni nchini kwa sasa imekuwa ni sehemu
muhimu sana ambayo haiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya mwananchi,
iwe mwananchi huyo anamiliki seti ya televisheni au la. Kwa kutazama vipindi
mbalimbali vya televisheni mtu huweza kufahamu mambo mengi makubwa yanayoendelea
nchini na hata nchi za nje, na kwa kutazama televisheni unapata burudani za
kila aina.
Japo sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na fursa
nzuri ya maendeleo kutokana na dunia kuingia zama za dijitali lakini pia ina
changamoto kubwa. Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya dijitali yameiletea
sekta hiyo fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina za uenezi
wa habari zimekuwa nyingi, kwa mfano, televisheni kwenye mtandao wa internet,
simu za mkononi zinaendelea haraka na makundi mengi ya televisheni ya nchi za
nje yameingia kwenye soko la televisheni nchini, hali kama hiyo imekuwa
shinikizo kubwa kwa sekta ya televisheni na filamu nchini.
Ili kuongeza nguvu za ushindani sekta ya televisheni na
filamu nchini lazima iendeleze ubunifu bila kusita ndipo inapoweza kukidhi
mahitaji ya watazamaji yanayoongezeka siku hadi siku, na kuwavutia wawekezaji
wa matangazo ya biashara.
Pamoja na aina mbalimbali za uenezi wa habari
zinavyoendelea haraka na kuwa nyingi, sekta ya televisheni nchini inakabiliwa
na shinikizo kubwa la ushindani. Hivi sasa nchini tuna vituo vingi va
televisheni, kikiwemo kituo cha televisheni cha taifa na vituo vingine vya
kitaifa vya binafsi. Pia kuna vituo mbalimbali vya televisheni za mikoa.
Vituo vikubwa vya televisheni kama TBC1, ITV, Star TV,
Channel Ten, EATV na vingine vilikuwa vinashikilia uenezi wa itikadi muhimu na
utamaduni katika miaka yote tangu nchi hii iliporuhusu urushaji wa matangazo ya
televisheni mwanzoni mwa miaka ya 1990, na vipindi vyake kadhaa kama ‘Taarifa
ya Habari’, ‘Mazungumzo kuhusu Matatizo Yanayofuatiliwa’, ‘Tamthilia’,
‘Burudani na Michezo Mbalimbali’ nk, vilikuwa ni vipindi vinavyotazamwa na kila
familia.
Vipindi vya televisheni hutiliwa maanani sana kwa kuwa
taarifa zake huambatana na picha hai za matukio, hivyo katika hali ya ushindani
kama huu vipindi vyote vinavyotangazwa katika vituo vya televisheni lazima viwe
na mvuto mkubwa na wakati wote na vinapimwa kwa ‘idadi ya watazamaji’ ili
kuhakikisha vipindi vinavyorushwa ni bora.
Ndiyo maana mara kwa mara hutokea ushindani mkubwa sana
kwa vituo vya televisheni kugombea kurusha matangazo ya mashindano ya soka ya
kombe la dunia au ligi za soka za ulaya, kwa kuwa matangazo haya hupata
watazamaji wengi kuliko matangazo mengine.
Vipindi vya burudani ni vipindi vinavyovutia watazamaji
wengi na matangazo mengi ya biashara. Kwa sasa vituo vyote vya televisheni
vinajitahidi kuwa na vipindi vya michezo, drama na ucheshi (comedy) ili kuwavutia
watazamaji. Lakini kutokana na athari ya vipindi vya televisheni vya nchi za
nje, sekta ya televisheni nchini iliyoanza kujitafutia uhai na maendeleo, imejikuta
ikiingia kwenye shinikizo la mazingira ya utandawazi wa duniani, na taratibu
imeanza kumezwa na utamaduni wa kigeni.
Katika miaka ya karibuni, sekta ya televisheni nchini
imekabiliwa na ushindani mkubwa zaidi, vituo vya televisheni nchini
vinakabiliwa na changamoto kubwa kutoka vipindi vya televisheni vya nje. Watu sasa
wametekwa kuangalia vipindi mbalimbali kutoka nje, kwa mfano, matangazo ya moja
kwa moja ya mashindano ya ligi ya soka nchini Uingereza, filamu, na picha za
katuni na maonesho ya mambo mbalimbali. Hivi sasa matangazo ya vituo vya nje,
kutoka China, Korea, India, Ufilipino nk. yametawala nchini.
Kwenye stesheni zetu sasa hivi kumejaa tamthilia za
kutoka China, Ufilipino, Mexico na Korea. Na sasa wasambazaji wakubwa wa filamu
nchini wanaanza kuachana na sinema zetu na badala yake wanaanza kusambaza
filamu kutoka Bollywood zenye tafsiri za Kiswahili.
Tunasahau kuwa sekta ya televisheni na sinema ni chombo
muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika.
Ndiyo maana nchi za China, Korea au India zinaingia gharama kubwa za kutafsiri filamu
na tamthilia zao kwa Kiswahili kisha kuzitoa zioneshwe bure katika vituo vyetu
vya televisheni.
Kwa mfano, China kupitia Idhaa ya kiswahili ya CRI,
ilifanya kazi ya kutafsiri tamthilia ya ‘Doudou na Mama Wakwe zake’ na kutia
sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthiliya hii kwa zaidi ya miezi 10,
kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na nchi za Afrika ya mashariki.
Pia kwa miaka mingi nchi kama Ufaransa, kwa mfano, imefanikiwa
sana kuitumia sekta ya televisheni na filamu kutangaza utamaduni wao duniani. Ufaransa
imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa bajeti za kutengenezea filamu na vipindi vya
televisheni kwa nchi zinazoongea Kifaransa (Francophone countries). Kama hiyo
haitoshi, wamepanua wigo na sasa wanatoa pesa hata kwa nchi zingine kama
Tanzania.
Ndiyo maana, si ajabu kwa yeyote atakayeandika script yake
ya filamu au kipindi cha televisheni na kuitafsiri kwa Kifaransa, atapewa
udhamini wa maelfu ya Yuro na ubalozi wa Ufaransa ili atengeneze filamu au
kipindi chake cha televisheni.
Kwa sababu vipindi na tamthilia zetu hazivutii na hazina ubora unaokubalika kimataifa, vituo vya televisheni nchini vimechukulia hili kama fursa ya kuonesha vipindi vilivyotafsiriwa kutoka China, Korea na India kwa kuwa tu wanavipata bure (au kwa kulipia pesa kiduchu) lakini wanashindwa kubaini kuwa hii ni vita ya utamaduni na ya kutawalana kiakili.
Hivi tunaandaa taifa (kizazi) la kesho la aina gani? Kwa
mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani kwenye sekta ya
utamaduni? Au huu ni mkakati maalum wa kujenga jamii (watoto wetu) itakayobadilisha
tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje? Je, serikali imebariki hilo? Kwa
kweli maswali haya na mengine yanahitaji majibu.
Nahisi kama tunajenga jamii ya watu waliochanganyikiwa! Ndiyo maana haishangazi sasa kuona Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, viongozi wengine na hata wasomi wetu wakiwa ni watu wa kulalamika tu pasipo kutafuta njia sahihi ya kutatua matatizo yetu. Kwa sasa inawezekana hatulioni hili ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu.
Yote haya ni
sababu ya Serikali kutoipa Sekta ya Utamaduni umuhimu mkubwa. Wakati Tanganyika
inapata mwaka 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana,
mwaka 1962. Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na
roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa
watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.
Kupuuzwa kwa
tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila
na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo
binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na
tamaduni za jamii yake.
Tangu mwaka
1962 shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini
zimekuwa hazithaminiwi. Kwa sasa utamaduni pekee tuliobakiwa nao kama nchi ni
lugha ya Kiswahili. Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri
jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo
kikuu cha ndani cha jamii yetu. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi
ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni
alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.
Bahati mbaya hata lugha yenyewe wengi wetu hatuijui vyema,
nadhani kutokana na kutaka kuiga uzungu na mambo mengine yasiyo yetu, ndiyo
maana pamoja na kujidai kuwa Tanzania ndiyo kitovu cha Kiswahili lakini walio
wengi wanachanganya ‘r’ na ‘l’, ‘dha’ na ‘za’ n.k.
Wakati nikitafakari haya ninakumbuka maswali nililowahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja: “Sisi Watanzania values (maadili) zetu ni zipi? Kama tunazo je, tunazikuza kadri muda unavyopita au bado tunaendeleza status quo (hali
Tafakari.
No comments:
Post a Comment