Abdulrazaq Sinnan, maarufu kama Bond Bin Sinnan |
Wasanii wa Bongo Movie wakiwasalimia wananchi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, wakati wa kutangaza nia ya kugombea Urais kupitia CCM |
Jina
langu naitwa Abdulrazaq S.H. Sinnan ingawa asilimia kubwa ya Watanzania
wananifahamu kwa jina la Bond Bin Sinnan kwa takribani miaka 15 sasa
najishughulisha na masuala ya tasnia ya filamu nikiwa kama mtunzi, muigizaji,
mzalishaji na muongozaji wa filamu. Hivyo nina upeo na uzoefu mkubwa wa tasnia
ya filamu Tanzania. Naijua faida yake, matatizo yake na mengine mengi
yanayoihusu tasnia hii.
Kwanza
nianze kwa kuwapongeza sana wasanii wenzangu wa filamu nchini kutokana na
kujituma kwetu mpaka tumefanya tasnia hii kuwa ajira kubwa kwa watanzania wengi
sana. Vilevile tasnia hii imekuwa ni burudani kubwa kwa wana Afrika Mashariki
na Kati kwani zaidi ya watu milioni kumi wanaangalia filamu za Kitanzania.
Tasnia ya filamu imeajiri zaidi ya watanzania 500,000 ambao wanaitegemea tasnia hii ya filamu katika maisha yao ya kila siku: kuishi kwao kunategemea filamu tu na si vingine kuanzia chakula, kodi, ada za shule, usafiri na vinginevyo. Ukianza na waigizaji, waandaaji, waongozaji, watendaji wengine (camera, sounds, lights, art directors, location managers, makeup artists, editors, graphics designers, nk.) wasambazaji, video libraries, machinga, radio programs, tv programs n.k.
Dhumuni
la kuandika barua hii ni kuwakumbusha kuwa tasnia yetu inachungulia kaburi na
tukumbuke kuwa tasnia hii tumeitengeneza sisi, ikifa tutataabika sisi na wa kuipa
uhai iendelee kuwepo ni sisi wenyewe pia. Nasema yote haya kwa sababu hiki ni
kipindi cha uchaguzi na sisi wanatasnia tuna ushawishi mkubwa sana katika mambo
ya nchi yetu na ndio maana tumeweza kuona baadhi ya wasanii wenzetu kwenye
majukwaa ya wanasiasa ili kuwashawishi wananchi kusogea eneo la tukio na kuwaonesha
wagombea ni wa kweli kwa wayasemayo.
Tasnia
ya filamu ina matatizo mengi sana na kwa asilimia 60 yanasabishwa na serikali
yetu na ni kutokana na kutokuwa na sheria madhubuti za kulinda haki zetu
zisipotee na hapa nazungumzia Hakishiriki na Hakimiliki, filamu imekuwa ni
shamba la bibi yaani bibi yuko hoi na uzee na wanaovuna na kula ni wengine
ambao hawajui hata bibi alipanda vipi shamba hilo.
Serikali
ilitamka kuwa tasnia ya filamu iko rasmi na inatambulika lakini cha ajabu hakuna
sera ya filamu ya Tanzania sasa huu ni urasimishaji gani? Tunajiita tuko rasmi
wakati haturuhusiwi hata kupiga picha majengo ya serikali yaani hata kwa nje
tu, haturuhusiwi kuvaa nguo zinazofanana na za majeshi yetu huku tunaambiwa
hatuna uhalisia ndani ya filamu zetu na haohao. Haturuhusiwi hata kupiga picha
kwenye mbuga zetu za wanyama ili kuzitangaza ndani na nje ya nchi wakati kila
siku wizara inahangaika kutangaza utalii. Je ni kweli tuko rasmi au kiini
macho?
Sheria
hazijielezi waziwazi na wala hazisaidii kuleta haki hata kidogo. Ingawa tunakubali
kuwa chombo cha kusimamia haki za filamu na wanafilamu wote kipo na kinaitwa
COSOTA lakini kiukweli COSOTA haina msaada wowote na tasnia hii. Kwani imekuwa
ikitoa vibali vya kukodisha filamu bila idhini ya wenye filamu, kuonesha Filamu
kwenye vibanda bila idhini ya wenye filamu, kurusu kudurufu filamu bila idhini
ya wenye filamu na kuchukua mirabaha ya filamu katika mahoteli, mabaa, mabasi
vituo vya televisheni na cable network.
Ukitizama
kwa uchache mianya ya utengenezaji pesa inayotumiwa na COSOTA utagundua kuwa
ndio mianya mikubwa inayofanya wizi wa kazi za filamu za Kitanzania na
kuwafanya waishi kimasikini na mifano hai tunayo kabisa ya waigizaji
waliotangulia mbele za haki na hata walio hai maisha yao yalikuwa vipi na yako
vipi mpaka sasa?
Niseme
ukweli wa kutoka moyoni kuwa asilimia 95 wanaishi nyumba za kupanga na wasiopanga
basi wanaishi kwa wazazi wao au nyumba za urithi. Ni asilimia 5 ndio wenye
usafiri ingawa ndani ya hao pia hawajapata usafiri huo kupitia filamu bali ni
njia nyingine.
Hivi
wanatasnia wenzangu hatuoni matatizo yetu kweli? hatuoni serikali inatula tu na
hairudishi wala kutusaidia chochote? Hatuoni kuwa hakuna sheria madhubuti kwani
sheria zilizopo ni za bodi ya ukaguzi wa filamu na zimetungwa mwaka 1976. Je
mwaka huo kulikuwa na filamu ngapi ukilinganisha na sasa? Kulikuwa na
utandawazi kama sasa? Mbona sheria za kodi zimetungwa mpya lakini sheria za
kuhusu filamu hazijabadilishwa?
Je
tunatakiwa kuendelea kuwa shamba la bibi? Serikali inavuna kodi kiasi gani
kupitia vifaa vyote vya utengenezaji filamu kuanzia ushuru wa uingizaji wa
vifaa kutoka nje kama Camera, computer, taa, vifaa vya sauti, empty cd, cd
printers, papers printers, papers, Dvd covers? Pia katika malipo ya film Board
kwa ukaguzi, Cosota kwa ajili ya usajili na manispaa kwa ajili ya vibali vya
kubandika matangazo n.k? Jaribu kupiga hesabu ya filamu moja serikali inaingiza
shilingi ngapi na msanii au producer anaingiza shilingi ngapi utalia machozi.
Chombo
ambacho wanatasnia wengi tulitegemea kuwa kinaweza kutukomboa, TAFF, lakini uongozi
wake ndio umekuwa cha kwanza kutumiwa na wanasiasa, wasanii wamejiunga na Team-nani
sijui na kimekuwa hakina usaidizi wa ufumbuzi wa matatizo ya tasnia ya filamu
bali kuwagawa wasanii na kuwatafutia ugomvi ili pasiwe na umoja sababu aendelee
kutawala.
Mpaka
mwaka huu taasisi hii imetumia nguvu kubwa kuandaa Tuzo za Filamu ambazo pia
inashutumiwa kuwa tuzo wamegawana viongozi wa ndani ya taasisi hiyo kupitia
kazi walizozifanya. Kilio kikubwa kama cha pirates, kodi na hakimiliki
wameshindwa kufanya lolote. Je hili nalo hatulioni kuwa tunahitaji mbadala wa
Taff? Au tunahitaji kuibomoa Taff na kuiunda upya?
Wanatasnia
wenzangu hiki ni kipindi cha sisi kuangalia yupi atakayekuwa tayari
kutusikiliza na kutatua matatizo yanayotukabili. Tusihadaike na pesa ndogondogo
za kusafiri na wagombea majimboni na kuwanadi, wakiingia madarakani wanafanya kilicho
katika mipango ya serikali. Hebu basi kwa pamoja tuache upinzani wetu nyuma na
tuungane katika kutetea haki yetu. Hivi kweli tunazidiwa ushawishi hata na madereva
kwani tumeona hivi karibuni waligoma na matatizo yao yakatatuliwa.
Hatuoni
kuwa tunastahili kutengenezewa sheria madhubuti za ulinzi wa kazi zetu?
Hatuoni
tunahitaji misamaha (exemption) ya kodi za kuingiza vitu kama wakulima na
wafanya kazi wa serikalini?
Hatuoni
tunahitaji kupunguziwa makato ya kodi za ndani katika ufanyaji kazi wetu?
Hatuoni
kuwa tunahitaji mirabaha ya ukodishwaji na uoneshwaji wa filamu zetu kupitia
libraly, video shows, vingamuzi, mahotel, mabaa, mabasi, mashirika ya ndege,
kwenye meli, mitandaoni na cable netwok?
Je,
hatuoni serikali inatakiwa kuturuhusu kupiga picha majengo ya serikali hata kwa
nje tu kwani kama leo inachukua kodi katika biashara zetu basi inatakiwa
itambue uhitaji wetu wa matumizi ya picha za Magereza, Jeshi la polisi, Jeshi
la Wananchi, Airport, Bandari, Mabenki nk?
Je,
hatuoni tunahitaji kuhamishia kesi zetu katika mahakama ya biashara? Kwa sababu
tunalipa kodi na makato yote wanayolipa wafanyabiashara wengine? Je, hutuoni
umuhimu wa kuanzishwa kwa mahakama ya hakimiliki na hakishiriki? Je, hatuoni
tunapaswa kupigana ili filamu kutoka nje nazo zikaguliwe Bodi ya filamu na pia
zilipiwe stika kama ilivyo kwa biashara nyingine iwe bidhaa za ndani au nje
zote hupewa stika na TRA?
Wanatasnia
wenzangu kwanini tunashindwa kuungana pamoja na kuhakikisha tunatimiziwa haya kama
baadhi walivyoungana na kupinga ushushwaji wa bei za filamu? Je ni kweli
hatumjui adui yetu? Haya ni baadhi ya maswali tunapaswa kukaa chini na
kujiuliza kabla ya kuanza kupokea vijisenti vya wanasiasa na vikatupa raha za
muda mfupi huku miaka mitano ijayo tukaendelea kutaabika. Tusikubali kufunikwa
na vivuli vya wasanii wachache wanaoonekana kurandaranda kwa wagombea eti
wakaonekana kuwa wanaiwakilisha tasnia hii ya filamu.
Wanatasnia
wenzangu kama kuna kitu tunahitaji basi tuungane na tusimame pamoja kuona
tunashinda vita hii na kujikomboa katika dimbwi la mateso ya tasnia yetu na
tusifanywe shamba la bibi.
Na
tufahamu kuwa sanaa ina mashiko makubwa kuliko siasa na wanasiasa ni watu ambao
wanaajiriwa na wananchi kwa kupiga kura lakini sisi tunawaburudisha wananchi.
Mfano wangu mdogo ni kuwa nilimfahamu Michael Jackson, Arnold Schwarzenegger, Sylvester
Stallone na wengine nikiwa simjui Rais wa Marekani, Nilimfahamu Bob Marley
nikiwa simjui Rais wa Jamaica, pia nilimfahamu Pele nikiwa simjui Rais wa
Brazil bila kusahau niliwafahamu Bruce Lee na Jacky Chain nikiwa simjui Rais wa
China.
Naomba
niwahakikishie hata leo kuna watoto wanawafahamu Vincent Kigosi, King Majuto,
Wastara, JB na wengineo wengi lakini hawawajui hao wanasiasa wote waliochukua
fomu za kugombea iwe urais au ubunge. Kama tuna akili basi tutafahamu nini cha
kufanya lakini kama tunataka kuendelea kusemwa na hao wanasiasa kuwa sisi ni
ombaomba kwao na kila wakituona wanatamni kujificha basi tunyamazeni kimya tena
tusibiri kusemwa bungeni au tusubiri malaika ashuke na kutusaidia kama hilo
linawezekana.
Asanteni
kwa kusoma na nina imani kuna kitu tunaweza kujifunza kupitia niliyoyaandika
hapa. Ndimi Mwanatasnia Mwenzenu.
Bond Bin Sinnan
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment