Wasomi kama hawa ni tegemeo katika jamii yetu, wanapokwepa majukumu yao kama wasomi ni hasara kwa taifa
NILIPOKUWA mdogo, moja ya
sababu kubwa iliyonifanya nipende sana
kwenda shule ni kusoma na kusikia hadithi na visa mbalimbali, ama kwa kuvisoma
kwenye vitabu (wakati huo kila shule ilikuwa na maktaba yenye vitabu vya
kutosha), au masimulizi kutoka kwa walimu wenye kupenda kufundisha kwa mifano. Hadithi
nilizozisikia na kuzisoma zilijaa mafunzo ya kila aina, hadithi kama zile za
kina Juma na Roza, Bulicheka na mke wake Elizabeth
na Wagagagigikoko, au ile hadithi maaruf ya ‘Heri mimi sijasema’.
Hii ni hadithi iliyohusu
vita katika ufalme fulani, ambapo wapiganaji watatu wakiwa vitani waliamua
kujificha kwa kujifunika na nyasi, bahati mbaya adui akawa anapita eneo lile na
kuwakanyaga bila kujua. Mmoja wa wapiganaji hao akalalamika; “kwanini
unawakanyaga wenzio kama nyasi?” Yule adui
akashtuka kuwa pale kuna mtu kajificha akamchoma mkuki na kumuua.
Mpiganaji wa pili akamuonya
mwenzake; “kwanini wewe unasema, je, tukigundulika?” Adui akamchoma mkuki na
kumuua pia. Yule wa tatu kwa kujiamini akiamini kuwa yeye yuko salama akasema;
“heri mimi sijasema”. Naye akachomwa mkuki na kufa. Huo ukawa mwisho wa
wapiganaji wale watatu.
Kipindi kile cha utoto niliifurahia
sana hadithi
hii japo sikuwa nikielewa hasa undani wa kisa hiki na mafundisho yake kwa
jamii. Baadaye nilipokuwa nikisomea utabibu, nilianza kugundua kuwepo baadhi ya
mafundisho yanayotokana na visa kama hiki
nilivyovisoma: hasa pale nilipozama kusoma somo la matatizo ya akili
(psychiatry).
Katika psychiatry, kuna
kitu kinaitwa ‘mental mechanism’, huu ni mfumo wa ulinzi wa kisaikolojia na
mbinu inayotumika kujifariji ili kukidhi mahitaji ya mtu kijamii, kiutamaduni
na kihisia kwa madhumuni ya kupunguza msongo wa mawazo, wasiwasi au
kuchanganyikiwa. Kwa maana nyingine, mtu huutumia mfumo huu katika kujifariji
kuwa matatizo anayoyaona si yake, hayakusababishwa na yeye bali ya watu wengine
kabisa.
Zipo aina nyingi za mental
mechanism; kama Repression, Denial, Displacement, Projection, Introjection,
Conversion, Dissociation, Provocation Behaviour, Counter-Phobic Behaviour, Compensation,
Overcompensation, Rationalisation, Identification, Fantasy, Regression, Suppression,
Isolation na nyingine nyingi.
Nitatoa mifano michache ya
hizi mental mechanisms na jinsi zinavyofanya kazi kabla sijajikita kuelezea
nilichokusudia: mfano, Repression: hii ni aina
ambapo mtu hujaribu/hujifanya kuuondoa kabisa ukweli mchungu ndani ya fahamu
zake, ili imsaidie kusahau kabisa mambo ambayo hayamletei amani ya moyo/akili.
Mfano mtu hujifanya kulisahau tukio aliloshuhudia la kumuona jirani/ ndugu yake
akiliwa na mamba mbele ya macho yake.
Denial: mtu
hukataa kuukubali ukweli au ukubwa wa baadhi ya mazingira, ili kupunguza au
kuzuia simanzi na hisia zisizoepukika, kama
vile hasira, hatia, kuchanganyikiwa, aibu, nk.
Displacement: Baadhi ya mambo
ya kukera (kama mashambulizi ya kimwili au matusi) au hisia (kama
vile hasira, chuki, dharau, nk) kwa mtu au kitu yanaweza kuhamishiwa kwa mtu au
kitu kingine, ili kuepuka wasiwasi au hofu isiyoepukika. Kwa mfano; mwalimu wa
kike aliyegombana na mumewe, huhamishia hasira zake kwa wanafunzi.
Projection: Mtu
hujitahidi kuelekeza lawama au mapungufu kwa mtu mwingine ili
kujaribu kuzuia hisia ya wasiwasi au hatia au upungufu uliojitokeza. Mfano
rahisi ni pamoja na mwanafunzi aliyefeli mtihani kusingizia kuwa ‘mwalimu
alitunga mtihani mgumu ili kumkomoa’, au hulaumu kutokana na 'muda aliopewa haukutosha'.
Rationalisation
(sizitaki mbichi hizi): Hii mbinu hutumika wakati mtu anataka kufanya kitu lakini
anahisi aibu au hofu kuhusu kufichua nia ya kweli, au aliyepigania jambo
akashindwa, hivyo huibua sababu ya uongo. Mfano wa kijana aliyemfukuzia binti
akamkosa, hutafuta sababu ili kujifariji; “kwanza mwanamke mwenyewe miguu yote
ya kushoto”.
Fantasy
(Alinacha): fikra za matukio ambayo hayajawahi kutokea au hali ambayo wala
haipo. Fantasies imekuwa moja ya mental mechanism pale watu wanapoitumia kama chanzo cha kuwaletea furaha na faraja, kwa ajili ya
kupunguza msongo wa akili unaosababishwa na matakwa ambayo hayawezi
kushughulikiwa. Ni hali ya kawaida sana
kwa watoto na watu ambao bado wana akili za kitoto, au kwa mgonjwa wa schizophrenia.
Sasa nirudi kwenye mada
niliyokusudia leo, nimejikuta nikiyakumbukia yote haya kutokana na hali hali
halisi iliyopo sasa kwenye tasnia ya filamu nchini, hasa kutokana na ukweli
kwamba sinema za Tanzania
zimekuwa zikilalamikiwa kwa kutokuwa na ubora, hadithi za kuiga na kukosa
mvuto.
Hivi karibuni kupitia
mtandao wa kijamii wa facebook kulikuwa na mjadala mkali kuhusu tasnia hii ya
filamu nchini, huku kundi moja la watu wanaojiita “wasomi” kuonekana kukosoa sana huku wakilitupia
lawama kundi jingine la “wasiokwenda shule”.
Mmoja aliandika hivi kwenye
mtandao: “mimi sitazami kabisa huu utumbo unaoitwa Bongo Movie, kwanza hawa
jamaa hawashauriki, aidha utengenezaji filamu imekuwa sawa na ushabiki wa mpira
ambao hauhitaji utalaamu. Hawa ni waongozaji (director) uchwara ambao wanafanya
kazi kwa kubahatisha na kubabaisha. Tasnia imeingiliwa na wahuni.”
Baada ya kuambiwa
watengeneze za kwao zitumike kama mfano
‘Msomi’ mwingine akaandika: “Binafsi nimesomea sanaa na si kwa kubahatisha
lakini nimejitoa katika utendaji, nafanya criticism, natoa maelekezo na
mafunzo. Juzi niliitwa na Curious Pictures Afrika Kusini, kufanya mapitio ya
kazi zao zitakazoanza kutoka mwezi Januari, hapa kwetu nikishauri naambiwa ya
kwangu iko wapi...”
Nilijitumbukiza kwenye
mjadala huo na kuwalaumu wanaojiita wasomi kuwa wao ndiyo chanzo cha kuporomoka
kwa tasnia ya filamu nchini, kwa kuwa hawakusoma ili wabaki kujisifia kwenye mitandao
na vijiwe vya kahawa bali kuyafanyia kazi waliyoyasomea, msomi mmoja akanijibu kama ifuatavyo:
“Bishop Hiluka, tunakuwa
wakosoaji kwa sababu mnachofanya huko kwenye field ni pumba, nataka niwaeleze
kinagaubaga; ninakiri na niko tayari kutukanwa kwa hilo , hakuna filamu katika bongo movie ila watu
waliokaa mbele ya kamera wapo. Mtu anayeelewa ugumu wa kazi na gharama
hawezi kuingia ila kama ni mwenye njaa. Ndio
maana wasomi tunajitenga kuingia kwenye uwozo. Utamwambia msomi aingie kwenye
movie ya gharama ya laki nane? Ndio maana tunaona madudu. lazima mfike mahali
muone wasomi wanachokosoa ni cha kweli…”
Maneno haya na mengine
mengi ndani ya mitandao, kwenye vyombo vya habari na hata kwenye vijiwe imekuwa
ni sehemu ya kawaida kwa watu wanaojiita wasomi kuwaponda watengeneza filamu
wetu, wamekuwa mafundi wa kuponda kila kukicha pasipo hata kutoa ufumbuzi wa
nini kifanyike ili kuboresha kazi zetu.
Kuendelea kuponda (kukosoa)
bila wao kujitoa kwa dhati katika kuonesha njia ya namna sinema zinavyopaswa
kuwa ni kujaribu kukwepa majukumu kwa kutumia mental mechanism aina za ‘projection’
na ‘denial’ kwa kujaribu kuwasukumia lawama wengine. Hivi kama wewe umesoma na
una elimu nzuri tu ya taaluma, unasubirije kwanza mazingira ya tasnia
yaboreshwe na hao wanaotengeneza pumba ili wewe uje ufanye kazi? Sekta ya
filamu itaborekaje kama ‘wasomi’ watabaki
mtaani wakilalamika na kuponda?
Hivi unapoponda bila
kutumia usomi wako kuboresha mazingira siku ukitoka nje ya Tanzania , utajitofautishaje na Watanzania
watengeneza sinema wengine ilihali hata wewe ni Mtanzania?
Ni kweli tuna matatizo
mengi kwenye sinema zetu, watunzi wa filamu hawana mafunzo ya uandishi wa
miongozo ya filamu na michezo ya kuigiza (Script), ndiyo maana tatizo kubwa
lililopo kwenye filamu (nyingi) za Kitanzania ni uwezo mdogo wa uandishi wa
miongozo, kitu ambacho kinasababisha filamu na michezo mingi ya kuigiza
kuonekana kuwa haina muelekeo.
Pia waigizaji wa Kitanzania
wengi ni wazuri katika uigizaji lakini si katika kuandaa miongozo ya filamu, na
kwa kuwa lengo ni kuzifanya filamu za Kitanzania kuwa na ubora, hawa wanaojiita
wasomi kwa pamoja wangejikita katika kuwaelimisha waandaaji na kutengeneza
mazingira bora ya kufanyia kazi yenye kuendana na soko la ushindani kimataifa.
Badala yake tumekuwa na kundi kubwa la ‘wasomi mbumbumbu’ linaloishia kuponda
tu na kujitoa (projection na denial) kwenye lawama za sisi hatutengenezi pumba.
Hii haina tofauti na kile kisa cha ‘heri mimi sijasema’.
Nimalizie kwa kuwapongeza baadhi
ya wasomi (kwangu hawa ndiyo wasomi): Dk. Vicensia Shule, Dk. Mona Mwakalinga, Prof.
Martin Mhando, Amanzi Ali Katindi, na wengineo kwa kujitoa kwa dhati kuwa
karibu na wasanii hawa wanaopondwa na kuwapatia mafunzo watengeneza sinema
wetu.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment